KATIBU
Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod
Slaa, ameibua tuhuma nzito dhidi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), akidai
kimeingiza silaha nchini bila ya vibali ili zitumiwe na vijana wao
kukabiliana na wapinzani.
Dk. Slaa alisema kuwa wanazo nyaraka zinazoonesha namna CCM
walivyoingiza silaha hizo nchini kwa ajili ya kuwapatia vijana wao
waliowekwa kwenye makambi maalumu wakipatiwa mafunzo.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana mjini Morogoro, kuelezea tathmini ya
Operesheni Sangara, maarufu kama Vuguvugu la Mabadiliko (M4C)
inayoendelea mkoani humo, Dk. Slaa alisema mbinu hizo zimekuwa
zikitumiwa muda mrefu na viongozi wa CCM.
Alitolea mfano kauli ya Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama, aliyoitoa
wakati wa uchaguzi mdogo jimboni Igunga akidai kuwa CHADEMA imeingiza
askari wenye mafunzo maalumu nchini.
“Nilikuwa ninajiuliza hawa
CCM wana ujasiri gani wa kusema uongo kwa vyama vingine juu ya kuingiza
silaha, sasa nimejua dhamira yao baada ya kupata nyaraka zinazoonesha
mpango mkakati wao wenye lengo la kuwatumia vijana walio katika makambi
yao kwa ajili ya kufanya vurugu kwa kutumia silaha wanazowapatia,”
alisema.
Aliongeza kuwa kudhihirisha CCM hawatanii katika kutaka kufanya
vurugu, msafara wa CHADEMA mkoani humo umekuwa ukiandamwa na watu
tofauti kwa kutumia magari tofauti.
Dk. Slaa alibainisha kuwa juzi
wakiwa wanatoka katika Jimbo la Gairo, gari lenye namba za usajili T
886 AVS aina ya Prado lilikuwa likiwafuatilia hadi wilayani Mvomero na
taarifa hizo walizitoa kwa askari waliokuwa wakilinda mikutano yao
katika Wilaya ya Mvomero.
“Juzi walifanya hivyo tukiwa Mvomero, tukatoa tarifa polisi na leo
asubuhi tumepata taarifa ambazo hatuwezi kuzipuuza kuwa kuna vijana kati
ya 10-20 wakiwa na sumu, sindano na visu wanawawinda watu walio katika
operesheni kwa ajili ya kuwadhuru na nimewaagiza vijana wangu wa idara
ya usalama wakatoe taarifa polisi,” alisema Dk. Slaa.
Hata hivyo, wakati Dk. Slaa akisema taarifa za msafara wao
kufuatiliwa wakiwa wanatoka Gairo kuelekea Mvomero, waliziwasilisha
polisi ili zifanyiwe kazi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustine
Shilogile, alisema hana taarifa hizo.
Nape akanusha
Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC)
Taifa wa CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alikanusha tuhuma za Dk.
Slaa, akidai kuwa mwanasiasa huyo anazeeka vibaya na kwamba ni bora
akawaachia vijana siasa.
“Maneno haya hayapaswi kusemwa na mtu kama Dk. Slaa lakini nikwambie
kuwa CCM haina makambi hayo anayoyasema, naomba Watanzania wampuuze,”
alisema.
Nape aliongeza kuwa CCM haijawahi kuwaza kuwa na mawazo
ya kutumia silaha na haitakuwa nayo kama alivyodai Dk. Slaa, akibainisha
kuwa hata wakati wa kudai uhuru silaha hizo hazikutumika.
Alisema kuwa anachokiona ni kwamba CHADEMA inasambaratika na hivyo
inaanza kutafuta sababu za uongo, huku akikumbushia madai aliyoyatoa Dk.
Slaa mwaka juzi wakati wa Uchaguzi Mkuu kuhusu wizi wa kura.
“Utakumbuka
mwaka 2010 wakati wa Uchaguzi Mkuu, Dk. Slaa alisema kuna kontena lina
kura mkoani Mbeya, lakini hadi leo hajawahi kuthibitisha uongo wake,”
alisema Nape.
Pinda abanwa
Katika hatua nyingine, Dk. Slaa
amemtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuweka hadharani michango
iliyokusanywa kwa ajili ya waathirika wa matukio ya mabomu ya Gongo la
Mboto na Mbagala; na mafuriko ya Kilosa na Dar es Salaam.
Dk. Slaa alisema waziri mkuu anapaswa kutoa maelezo ya kina ndani ya
siku 30 ili Watanzania wajue michango waliyochanga kwa ajili ya
kuwasaidia ndugu zao ni kiasi gani na imetumikaje.
Alisema baada
ya waziri mkuu kutoa hesabu ya vitu vilivyokusanywa pia anapaswa
kumuagiza Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuvifanyia ukaguzi
ili kujua namna vilivyotumika na kwamba kama hilo litashindikana,
wabunge wa CHADEMA watakuwa na wajibu wa kuandaa hoja binafsi na
kuiwasilisha bungeni.
“Tumeshuhudia namna waathirika wa mafuriko ya Kilosa walivyochangiwa
na Watanzania kutoka sehemu tofauti ya nchi, sasa leo wamefikia kulazwa
chini chumba kimoja kwa familia nzima pasipo kujali umri wala jinsia na
mbaya zaidi, vyoo wanavyotumia havina milango, huku ni kufedhehesha utu
wa Mtanzania,” alisema.
Wavuna wanachama 31,337
Wakati huo huo, Mkuu
wa Operesheni Sangara wa CHADEMA katika mikoa mitano ya Morogoro,
Singida, Manyara, Dodoma na Iringa, Benson Kigaila, alisema baada ya
kupita katika majimbo sita ya mkoani Morogoro wamefanikiwa kuvuna
wanachama 31,337.
Kigaila alisema wanachama hao ni baada ya CHADEMA kufika katika kata
137 na vijijji 471 kwenye majimbo sita ya mkoa huo. Kwamba alipokea kadi
7,603 kutoka katika vyama vingine.
Alisema
katika operesheni hiyo, wananchi walichangia kiasi cha sh 17,895,650,
ndizi mikungu 831, magimbi 73, mayai trei 17 na mchele kilo 148.
Kigaila alifafanua kuwa kadi zilizouzwa ziliingiza kiasi cha sh 15,768,500.
No comments:
Post a Comment