Sunday, August 19, 2012

KUJIKUWAMUA KWA UHIFADHI MAZINGIRA ENDELEVU

Thursday, 28 June 2012   (Mwananchi)

Mkazi wa mkoani Lindi akipokea fedha za majaribio ya kuhifadhi misitu
Midraji Ibrahim
KATIKA kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, Serikali imekuwa ikifanya juhudi mbalimbali kwa kushirikisha sekta binafsi na mashirika yasiokuwa ya kiserikali.

Miongoni mwa mashirika yasiyo ya Serikali ni Mpango wa Kupunguza Uzalishaji Hewa Ukaa inayotokana na kukata miti ovyo na uharibifu wa misitu (Mkuhumi).
Ofisa Mfuatiliaji na Mtathmini wa Mkuhumi, Emmanuel Lyimo, anasema mradi huo wa majaribio wa miaka mitano unatekelezwa kwa ubia kati ya Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG) na Mtandao wa Jamii wa Usimamizi Misitu ya Asili Tanzania (Mjumita).
Lyimo anasema mradi unatekelezwa kwenye wilaya tatu katika vijiji 39 vya Lindi Vijijini (17), Kilosa(16)na Mpwapwa(6).
“Lengo la mradi huu ni kuunga mkono juhudi za Serikali za kupambana na mabadiliko ya tabianchi, ambayo madhara yake yako wazi kwa kila Mtanzania. Imefikia  wakati Serikali haiwezi kuvumilia uharibifu wa misitu kwa kuwa athari zake ni kubwa na zimeonekana dhahiri.

“Sehemu mbalimbali nchini tunashuhudia uharibifu huo kama kuyeyuka kwa theluji ya mlima Kilimanjaro, mafuriko kama yaliyotokea Kilosa mwaka juzi na madhara mengine kwa mfano, magonjwa ya malaria na kupotea kwa baadhi ya fukwe,” anasema Lyimo.

Anasema lengo siyo kuhifadhi tu, bali ni kupunguza ukataji miti ovyo na uharibifu wa misitu kwa kutoa motisha wa fedha wenye usawa kutoka soko la kimataifa la hewa ukaa (Carbondioxide), kwa ajili ya jamii zinazosimamia au kuhifadhi misitu kwa njia endelevu.

Anafafanua kwamba Mkuhumi ni mchakato mrefu mpaka kufikia hatua mwanajamii kupata motisha wa fedha.
“Moja ya motisha ni kusaidiana na jamii husika kuandaa mipango shirikishi ya usimamizi wa misitu, vijiji tisa vya Lindi vimetenga hekari 33,488.32, vijiji vinne vya Kilosa, vimetenga hekari 29,638.4.

“Maeneo haya ni kwa ajili ya misitu ya hifadhi ya kijiji ambayo tunayatumia kwa matumizi mbalimbali (isipokuwa kwa  kilimo) kwa njia endelevu. Pia, ni mwongozo mzuri wa kuzuia migongano ya matumizi ya ardhi,”anasema.
Ofisa huyo anasema mradi umeandaa mipango ya kupunguza uharibifu wa misitu kwenye vijiji hivyo,kuboresha kilimo nakuajiri wataalamu wawili waliyobobea kwenye kilimo.
Pia anasema wanakijiji wameunda vikundi vya wakulima, safari ya mafunzo ya kilimo hifadhi na kwamba wakulima 30 kutoka Lindi na30 Kilosa wametembelea maonyesho ya kilimo ya Nanenane.

Wakulima hao wamefundishwa jinsi ya kukabiliana na wanyama waharibifu.
“Wamefundishwa jinsi ya kutengeneza na kutumia majiko banifu ambayo hayatumii kuni nyingi. Majiko haya yanaokoa muda mwingi ambao mama angetumia kuni kupika badala ya kufanya shughuli nyingine za maendeleo,” anasema.

Mbali na hayo anasema vijiji vingi havina majengo ya ofisi ya kijiji na kusababisha mikutano na vikao mbalimbali vya maendeleo kufanyika kwenye madarasa ya shule.

Wanafunzi wamekuwa wakilazimika kupunguza muda wa masomo kutokana na madara yao kutumika kama kumbi za mikutano.

“Kwa kulitambua hilo, mradi ulikubaliana na vijiji vya Lindi na Kilosa kuchangia ujenzi wa ofisi ya kijiji ambayo itakuwa na ukumbi wa mkutano, chumba cha mtendaji, mwenyekiti, kamati ya maliasili na masjala ya kijiji,” anasema Lyimo.

Mpaka sasa mradi umejenga ofisi tano Kilosa kwenye vijiji vya Chabima, Dodoma Isanga,Munisagara, Nyali na Kisongwe ambazo zimeanza kujengwa.

Pia kuna vijiji vya Ibingu na Mfuluni ambavyo vimeanza ujenzi. Kwa upande wa Lindi vijiji vinne vya Moka, Mkanga 1, Kikomolela na Nandambi vimekamilisha ofisi zao.
Mradi huo unashughulikia suala la utawala bora kwakushirikisha kila kundi. Kuthibitisha hili, mradi umetoa mafunzo kwa halmashauri za vijiji, kamati za maliasili na kamati za matumizi bora ya ardhi.
Anasemawametoa elimu ya mazingira kwa walimu wa shule za msingi zilizopo vijiji vya mradi, kwa lengo la kupanda mbegu bora za kuhifadhi mazingira kwa watoto.

Fedha za majaribio
Lyimo anasema uvunaji wa hewa ukaa umekuwa ukifanywa kwa kupima eneo, ambalo hutengwa kwenye sehemu mbalimbali ambako wataalamu  wanapima kiwango cha hewa ukaa iliyomo kwenye miti.
Anasema baada ya kubaini kiwango hicho, wanarudian kupima kwa vipindi tofauti na baadaye wanatathimini kiwango cha fedha ambazo zinatolewa na mradi kwa ajili ya jamii husika.
Mradi umefanya majaribio ya kulipa wananchi ambao kwa juhudi zao binafsi wamehifadhi mazingira. Vijiji viwili vya Wilaya ya Kilosa; Dodoma Isanga wamepata zaidi ya Sh13 milioni na  Kijiji cha Chabima zaidi ya Sh23 milioni.
Kwa upande wa Wilaya ya Lindi vijiji vitatu vimepata fedha za majaribio; Mkanga 1 kimepata Sh8.4 milionin Likwaya Sh7.3 milioni na Ruhoma Sh21.8 milioni.
Uzoefu kuhusu mradi
Lyimo anasema miaka miwili ya mradi huo, wamejifunza kwamba kuwahamasisha wananchi kuanzia  mpakamkutano mkuu wa kijiji, ni njia mojawapo ya kuwafanya wanakijiji kupata mafunzo yaliokusudiwa.

“Mkuhumi utawezekana kama wanakijiji watapewa njia mbadala ya kujipatia kipato, ushirikishaji makundi yote ndiyo njia pekee kufanya mpango huo kuwa endelevu,” anasema.

Lyimo anasema licha ya mafanikio hayo, mradi unakumbana na matatizo ya aina mbalimbali kama ushawishi unaofanywa na watu wachache ambao wanataka wananchi wasitunze misitu kwa maslahi yao binafsi.
Anasema watu hao wanawashawishi wananchi kukataa kutenga maeneo ya hifadhi ya msitu kwa kuwa wakifikiri kwamba hawatavuna mbao na mkaa.
Pia, anasema uchomaji moto misituni tatizo ambalo liko wazi kwa kila mtu, kwani moto ni adui wa miti.
“Unaharibu uoto wa asili, wanyama wanakosa makazi, wanyama na mimea mingine inateketea kwa moto na unachangia kuzalisha hewa  ukaa badala ya kupunguza,” anasema.
Lyimo anasema wananchi wanatakiwa kuchukua Mkuhumi kama fursa ya kuboresha mazingira yao na wasichukulie kama ni sehemu ya motisha wa fedha.

No comments:

Post a Comment