Sunday, August 5, 2012
STEVEN WASSIRA NA UWAZIRI WA MAHUSIANO NA URATIBU (MWANAMASUMBWI T Y S O N)
Wassira unafaa kuwa Waziri wa Mahusiano?
Na Ratifa Baranyikwa
Source “Tanzania Daima”, Tanzania: 16 Juni, 2012)
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu, Steven Wassira, wadhifa anaouvaa hauendani na mwenendo pamoja na utendaji wake.
Yasemekana lengo kuu la wizara anayoiongoza, ni kushughulikia mahusiano kwa maana ya kuhakikisha migogoro inayojitokeza kwenye jamii inadhibitiwa.
Kwa bahati mbaya sana, kiongozi kama Wassira aliyepewa wizara inayoshughulikia mahusiano, sijui kama anafahamu kwamba anapaswa kutambua mafanikio binafsi na yale ya kitaaluma, ukichanganya pia na malengo ya wizara yanayotegemea mahusiano mazuri kati yake na wale anaowaongoza.
Nitaangazia matukio machache tu kati ya mengi ambayo yanamvua Wassira sifa ya kutofaa katika wadhifa wa wizara aliyopewa.
Kwanza, ni hasira ambazo amekuwa akishindwa kuzidhibiti wakati anapokuwa akijibu maswali, hata yale ya kukera.
Kwa mfano, hivi karibuni alipozomewa na wananchi wa jimbo lake la Bunda, kiongozi huyu alishindwa kujibu vizuri maswali aliyoulizwa na wananchi wake, na badala yake aliruhusu hasira.
Maswali ya wananchi hao ni pamoja na lile la kumtaka aeleze ni kwa nini eneo la Shule ya Msingi Balili limechukuliwa na aliyekuwa mkuu wa wilaya, Chiku Galawa, ambaye sasa ni mkuu wa mkoa wa Tanga, na wananchi walishalalamika, lakini yeye hajawahi kulizungumzia.
Katika majibu yake, Wassira alijibu swali hilo kwa mkato kuwa hawezi kulisemea hilo, kwamba ni la watu wa ardhi.
Inawezekana kabisa Wassira akawa sahihi katika majibu yake hayo, na pia asiwe sahihi kwa upande mwingine, hoja nitajenga baadae.
Swali jingine ambalo linamvua sifa Wassira katika Wizara ya Mahusiano, ni pale alipoulizwa kuwa, katika mkutano huo alikuwa anahutubia kama mbunge, waziri au kada wa CCM, kwani alitakiwa kufahamu kuwa Bunda ina wanachama wa vyama vingi.
Lakini katika majibu yake, alihoji kwa ukali: “Kwani Wenje (Mbunge wa Jimbo la Nyamagana-CHADEMA) alikuja kuhutubia hapa hivi karibuni kama nani?” Na hapo ndipo tunaelezwa kuwa wananchi walianza kumzomea.
Mfano mwingine ni huu wa juzi, ambako Waislamu wametangaza kuisusia sensa na sababu wanayoitoa ni kutoridhishwa na majibu ya Wassira, kadhalika ubabe aliowaonesha.
Inawezekana kabisa ndugu zangu Waislamu hoja zao zikawa si za msingi, lakini katika kujibiwa, kuna mambo ambayo Wassira alitakiwa kuyaangalia kwa makini.
Kwa mifano hiyo michache, namuona Wassira amekosa sifa muhimu zifuatazo:
1. Kwa mfano nikianza na swali aliloulizwa kuhusu ardhi, ni kweli jambo hilo linawahusu watu wa ardhi, lakini yeye kama kiongozi na mwakilishi wao, alisahau jambo moja kubwa la wajibu. Pengine kwa majibu rahisi alipaswa kulisemea hili.
2. Jambo la pili, ambalo linamgusa Wassira ni hili la kutosikiliza na kuchukua muda wa kutafakari kujibu hoja kwa kuangalia aina ya watu anaowajibu, badala yake amekuwa akitumia hasira zaidi.
3. Tatu, anatumia nguvu kubwa kusukuma hoja zilikotoka na kujitetea hata katika hali ambayo hana hoja ya kujitetea.
Kiongozi huyu namuona ni mtu wa kukosa uvumilivu, anashindwa kufahamu umuhimu wa kukumbuka kwamba hata kama kile watu wanachokisema ni ukweli kwao, haijalishi ni jinsi gani atajisikia.
4. Nne, Wassira anashindwa kutambua kwamba kazi yake ya mahusiano kuna kitu kinaitwa msamaha.
Katika somo zima la mahusiano ya kikazi, inaelezwa bayana kuwa; omba msamaha pale inapotakiwa. Kama kile wanachokisema ni sahihi na umekosa, omba msamaha.
Katika hili, narejea mfano wa Waislamu ambao wanadai kuwa katika vikao walivyokutana na Wassira kuna wakati alichelewa, na pia kuwatolea majibu waliyoyaita kuwa ni ya kibabe.
5. Tano na mwisho, Wassira si mtu wa kumshukuru mtu anayeongea kwa uwazi na ukweli, na hivyo suala la mahusiano kwake kumpa wakati mgumu.
Namshauri Wassira apime hayo juu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment