MAONI
YA KATIBA NA. MOJA – 20/8/2012
Ibara
Na. 1 ya Katiba ya 1977:
Napendekeza Tanzania
iwe nchi ya mfumo wa “Federation” rasmi ili kuondoa kero na manunng’uniko yote
ya pande zote mbili za Muungano. Kwamba
nchi ya Tanganyika ipatikane kama
ilivyokuwa zamani kabla ya tarehe 26/4/1964, na iwe nchi kamili. Zanzibar tayari ipo na iendelee kuwa nchi
kamili.
Nchi hizi mbili
zipige kura ya Maoni [Referendum] ili watu wake waseme endapo wanataka
waendelee kuwa katika Muungano au waachane na mfumo huo. Ili endapo zitakubaliana kuwa na Muungano,
nchi hizi zikutane katika Federation ya Tanzania [TZ] (au jina lolote
litakaloamuliwa na wananchi). Binafsi napendekeza jina hilo hilo libaki lakini
tukiwa katika Federation.
Kwa hiyo Dola ya TZ iwe ni muungano wa nchi mbili
zilizo huru za Tanganyika na Zanzibar.
Hata nchi nyingine yoyote itakapo kujiunga na TZ ruhsa; endapo tu itakubaliana na matakwa
ya watu wa TZ, huenda hilo likawa ndio chimbuko la Muungano wa Nchi za Afrika
(United States of Africa).
Mtindo huu wa DOLA
utasaidia kuzihamasisha nchi nyingine za jirani Barani Afrika kutamani kujiunga
katika Federation yetu; endapo tu tutaendesha mambo yetu kwa kufuata HAKI na
UTAWALA WA SHERIA.
Kwa wakati huu
niandikapo maoni haya (20/8/2012), nchini Tanzania hakuna haki tangu tupate
UHURU tarehe 9/12/2012. Hii ni kwa
sababu sehemu moja ya jamii ya Watanzania imejilimbikizia haki ya kuamua nchi
iendeshwe vipi na hivyo kuwafanya watu wa sehemu ya pili kuwa kama raia wa Daraja
la Pili ndani ya nchi yao.
Mifano ya
kuthibitisha jambo hili ni mingi mno na kwa uchache niliyowahi kuithibitisha
binafsi (kwa kunitokea mimi mwenyewe au kwa kuisoma katika maandiko ya
kitaaluma) ni kama ifuatayo:
1.
Hulka ya wafuatao imani ya Kikristo ya
kufundishana chuki dhidi ya watu wenye imani za dini nyingine; hasa Waislam. Hili linathibitishwa na mifano kadhaa
ifuatayo.
2.
Tabia ya ukiristo kujikita katika
mamlaka za utumishi wa umma na kulazimisha nembo zao kutumika maofisini na
hivyo kuwafanya watu wa dini nyingine kujisikia kubaguliwa kwa makusudi; jambo
linalopingana kabisa na Ibara ya 13 (1)
ya Katiba ya 1977. Mfano dhahiri wa
jambo hili ni kupamba Maofisi ya Umma wakati wa sikukuu kwa alama za Krismasi
[Miti mikubwa Sebule za Ofisi na kuipamba kwa “Chrismas Carols” na kutoa zawadi
za pombe kwa maofisa mbalimbali maofisini]; kuweka “Compact Disks” [CD] za
miziki ya dini ya Kikristo wakati wote maofisini na kuiliza kana kwamba
wawekaji miziki hiyo wako Kanisani au wako majumbani kwao badala ya Ofisi za
Serikali ISIYOKUWA NA DINI.
3.
Nyimbo hizi na alama nyingine kuwekwa
wazi maofisini kunakiuka kwa uwazi Ibara ya 3(1) inayotamka kwamba Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi isiyokuwa na
Dini.
4.
Ndani ya Katiba Mpya, mambo haya yaandikwe
na yapigwe marufuku kwa sababu yanawabagua Watanzania kutokana na imani zao.
5.
Mwezi Mei, 2012 usahihishaji wa
mitihani ya Wanfunzi wa Kiislam ulichakachuliwa na wanafunzi hawa wote
wakaonekana wamefeli somo la “Islamic Knowledge” ili wasipate sifa za kuweza
kuomba kuendelea na masomo ya juu zaidi.
Jambo hili lilipogunduliwa ETI likarekebishwa
na srikali. Tangu UHURU 9/12/2012 mchezo
huu umeendelea kuchezwa na Wakristo dhidi ya Waislam kwa sababu huko nyuma
Mwalimu Lila alithibitisha hili. Yeye
akiwa kama mmoja wa wasahihishaji wa mitihani ya wanafunzi wa sekondari,
aligundua watahiniwa wa Kiislam wanakatwa maksi zao na kufelishwa kwa makusudi
mazima na alipouliza wenziwe katika jopo la Wasahihishaji alijibiwa kuwa “hivyo ndivyo tunavyofanya katika kipindi
cha misimu yote ya kusahihisha mitihani, kwani wewe hujui?”. Alipolalamika hakuna kilichofanyika.
6.
Waislam walipolalamikia hili, Rais
aliyepita Benjamin William Mkapa (1995 -2005) aliwahi kusema kwamba zipo sababu
za kihistoria kwamba wasomi wengi zaidi nchini Tanzania ni Wakristo kuliko
Waislam na kwamba anataka apelekewa ushahidi (empirical evidence) kama kweli
Waislam wanafanyiwa madhila haya makusudi ili wafeli. Je, ni ushahidi gani
zaidi alioutaka Mkapa zaidi ya ule wa Mwalimu Lila? Serikali haikufanya lolote
baada ya kugunduliwa hili. Imelipalilia
na kulikubali liendelee.
7.
Jambo la kuwa Watanzania tunapendana
binafsi; Watanzania tuna umoja wa kwenye damu kwa kuoleana kokote nchini
Tanzania; Watanzania tunaoana japo kuwa tuko katika dini tofauti; yote ni kiini
macho cha kupendezesha baraza; mapenzi haya hayako moyoni mwa Watanzania. Watanzania hatupendani kama makundi tofauti
ya imani tofauti. Ukweli huu wa
kubaguliwa kinaga ubaga (kwa kufelisha Waislam) kunawafanya Waislamu wajisikie
ni raia wa Daraja la 10 na wala sio la Pili nchini mwao.
8.
Kusutwa kwa nafsi ya Rais Benjamin
William Mkapa na kuruhusu kutolewa majengo
ya Umma ya Chuo cha Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mjini Morogoro, mwaka 2004 kuwa Chuo Kikuu cha Waislam, hakusaidii kufuta
makovu ya madonda ya madhara na madhila yanayowapata Waislam ndani ya nchi
yao.
9.
Kitendo cha Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kushindwa kuwa na asasi zake yenyewe za kuhudumia Umma wa Watanzania wote na
badala yake kutoa RUZUKU (zitokanazo na
kodi za Watanzania wote) maradufu kwa Wakristo kujijengea huduma hizo na kuwa
ni mrija wa utajirisho wao; kwa kuwa huduma hizi ni za kibiashara; ni ubaguzi mwingine unaohisiwa kwa uchungu
sana na Waislam.
10.
Katika Baraza la Maulid la mwaka 2012,
kauli ya Rais wa sasa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais Jakaya Mrisho
Kikwete mjini Dodoma kwamba ETI Waislam hawajaomba RUZUKU hizo ni tusi kubwa
kwa sababu ushahidi upo dhahiri wa maandishi wa Waislam kuomba Ruzuku hizo
mwaka 1961. Jambo hili alilofanya Rais
Kikwete kwa Waislam linafanana na kauli ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Andrew
Chenge alipotamka mwaka 2010 kwamba shilingi zaidi ya bilioni mbili ni
vijisenti tu. Tofauti ni kwamba Kikwete
katukana Asasi nzima ya Uislam (kama mfumo wa maisha); wakati Chenge alitukana
Watanzania kwa ujumla wao; masikini na matajiri pia.
11.
Katiba mpya iweke ibara zitakazotoa
usawa katika kutoa ruzuku au ifute ruzuku zote husika. Isiegemee upande
mmoja.
12.
Habari zote chanya za Waislam
kufumbiwa macho na vyombo vyote vya habari nchini – Viwe vya umma au vya
binafsi. Kinachotangazwa kuhusu Waislam
ni upotoshaji wa habari zao, sana sana kwamba Waislam ni waanzilishi wa vurugu na
kwamba hawataki maendeleo.
13.
Habari zote chanya za Wakristo
kupambwa kwa vichwa vya habari vilivyokoloea (screaming headlines) na kuzificha
zile zilizo hasi kwa wasomaji ili ionekane kwamba Wakristo ndio wapenda
maendeleo na hawana matatizo wala migogoro baina yao katika Dhehebu mojamoja au
kati ya madhehebu tofauti.
14.
Tabia ya Asasi nyingi za Umma kupanga
mikutano yao muhimu sana ya maamuzi (Kama ya Bodi, ya Mabaraza ya wafanyazi, ya
Wadhamini, n.k.) siku za Ijumaa ili AIDHA Waislam wasiihudhurie; au muda wa saa
moja watakapokuwa na udhuru wa kwenda kusali, ndio maamuzi
yatayowaathiri vibaya; au maamuzi mazito yawahusuyo yachukuliwe. Huu ni ubaguzi mbaya wa kumuengua mjumbe Mkutanoni
kwa sababu ya imani yake. Yaani Muislam achague abaki mkutanoni ili atetee
masilahi yake ya kidunia au akaabudu Mola wake na aachane na mambo yamhusuyo
yeye na jamii yake duniani. Huu ni
ubaguzi USIOONEKANA. Lugha waitumiayo
wajumbe wa imani nyingine katika mikutano kama hii ni kwamba “Sacrifice Ijumaa
hii tu” maana yake “fuata njia na utamaduni wangu na achana na huo wa
kwako”. Mikutano hii muhimu isipangwe
siku za kuabudia dini yoyote katika sala za pamoja (congregational
prayers). Huu ni ubaguzi wa kimya kimya
dhini ya Ibara ya 13 ya Katiba ya 1977 kwa ujumla wake.
15.
Walimu wa Kikristo toka Chekechea,
Msingi, Sekondari hadi Vyuo Vikuu kuwa na tabia ya kuwanyanyasa, kuwabagua,
kuwatweza, kuwadharau, kuwapuuza, n.k. wanafunzi wasio wa dini yao. Siku hizi hata wanafunzi wa shule za misingi
huliongelea jambo hili. Maana yake ni
kuwa wanafanyiwa ubaguzi huo kwa dhahiri na sio kisiri tena. Watoto wanajengewa chuki baina yao yaani wa
dini moja na wa dini nyingine, dhidi ya Ibara ya 13 ya Katiba ya 1977.
16.
Shule za Kikristo zinakaribisha maombi
toka kwa wanafunzi wa dini zote kwa kigezo cha kuziendesha kibiashara bila
ubaguzi wowote. Kivitendo; shule hizi;
kama ilivyokuwa shule za Mkoloni na za Makanisa toka kabla ya Uhuru; zinalazimisha
Waislam kula nguruwe na kutowahudumia wakati wa hitajio maalum la mwezi wa
Mfungo wa Ramadhani, na kuwapiga mafuruku kushiriki katika ibada ya pamoja ya
Ijumaa. St. Scholarstica (iliyopo
Moshi) ni mfano mzuri sana wa hili kwa sababu jirani yangu aitwaye Abdulrazak Luwinzo
watoto wake wawili wanasoma huko na wamemsimulia hili lililowakuta mwezi wa
Ramadhani ulioishia tarehe 20/8/2012 (kwa kuwa watoto wamerudi wamekondeana kwa
likizo ya Sensa ya 2012), na yeye amenisimulia mimi jana tarehe 19/8/2012.
17.
Tabia ya Ukristo kung’ang’ania kuwa
siku ya mapumziko ni Jumapili tu wakati watu wa dini nyingine wana siku zao za
mapumziko ambazo hazitambuliwi kama siku za mapumziko kama Ijumaa kwa
Waislam. Na wala haitoshi kutoa muda wa
kwenda kuabudu/sala kwa pamoja kwani hiyo hailingani na kutoa mapumziko kwa
siku nzima. Wakristo na wapumzike
Jumapili na Waislam wapumzike Ijumaa.
18.
Katiba mpya iseme wazi uhuru wa kuchagua siku
ya mapumziko kwa imani zote.
19.
Tabia ya Wakristo kukataa katakata uanzishwaji
wa Mahakama ya Kadhi nchini Tanzania kwa mujibu wa imani ya Dini ya
Kiislam. Wakati nchi ya Tanzania
imerithi mfumo wa sheria za Kikoloni za Dola la Uingereza ambalo sheria zake
zimetokana na chimbuko la Kanisa (Ecclesiastical courts) na ndizo zitumikazo
kwa watu wote; lakini Dola kwa shinikizo la Wakristo, linapuuzia dai la Waislam
la kuwa na Mahakama yake ya Kadhi iliyokuwepo huko nyuma (kabla ya kuvunjwa miaka ya sitini – 1960s)
na ikigharimiwa na Dola. Usawa wa kuhudumia watu wake unapotea wakati
sheria za Tanzania zimerithi mfumo wa sheria za Kanisa na Waislam wanakataliwa
Dola yao isigharimie Mahakama yao kana kwamba hawachangii kodi zao.
20.
Katiba mpya iandike kuruhusu kuwepo
kwa Mahakama ya Kadhi itakayogharimiwa na Dola kama ilivyokuwa huko nyuma na
mambo yalikwenda vizuri kwa imani zote.
21.
Tabia ya Wakristo wengi kukasirikia
Vazi la Stara la Kiislam kana kwamba wameligharimia wao linawakera sana
Waislam. Wengine wanafikia hata kuwaita
Waislam hao (pamoja na mimi) na “kuwanasihi” waache au wabadilishe vazi
hilo ili wavae kama wanavyovaa wao. Kwa Waislam vazi hilo ni sehemu ya
Ibada. Wasijisikie vibaya watu wa dini nyingine kutimiza amri za Mola
wao ili mradi hawavunji sheria hizo za Dola za urithi wa Kikanisa.
22.
Kuruhusu MAPAMBIO [nyimbo za kidini ya
kikristo] hata katika shughuli/tafrija za umma zilizoandaliwa na serikali
ambako haitakikani kuwa hivyo kwa sababu serikali haina dini. Badala yake pasiwepo hata nyimbo kama hizo
zinazoingiza hisia ya kubaguliwa kwa watu wa imani nyingine.
23.
Katiba mpya iseme kwamba jambo hili ni marufuku.
24.
Pendekezo la kuingiza katika Katiba
Mpya jingine ni kuwa midhali Tanzania kwa mahesabu ya sense ya sasa ya “kusadikika”
ni kuwa tuko wananchi wa imani kuu mbili wenye asilimia sawa (asilimia 32 kwa 32), basi Katiba Mpya iseme
kwamba katika kila Nyanja ya Utumishi wa Umma pawepo na uwakilishi wa 50-50 ili
kuondoa hizi hisia za kubaguliwa,
kubaguana, chuki za dhahiri na za siri dhidi ya Waislam wa Tanzania.
25.
Mambo yote haya yana haki zote za
kuwekwa wazi na kuzungumzwa na kujadiliwa kinaga ubaga, bila ya kuficha kitu
ili kila mtu ayafahamu na ajue kisa na sababu ya watu wa imani moja katika
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanadai
haki zao kila uchao; haki ambazo hazitimizwi na serikali yao.
26.
Historia inatufahamisha fika kwamba hakuna
haki inayopatikana hivi hivi tu bila ya kudaiwa. Na hivyo mimi ni Muislam wa Tanzania na
ndio natumia haki hii ya: KUTOA MAONI JUU YA KATIBA MPYA KUTOA DUKUDUKU
NA MADAI YA HAKI ZANGU ZA MUDA MREFU ZISIZOTEKELEZWA na serikali.; kwa kudai
haki zangu katika njia hii. This is a
priceless opportunity for Tanzanian Muslims to ventilate their grievances in
full to the Constitutional Review Commission for consideration and
implementation (hopefully at last).
No comments:
Post a Comment