Tuesday, August 28, 2012

TUHUMA ZA KUHAMASISHA JAMII KUTOSHIRIKI SENSA TANZANIA

Mbaroni kwa tuhuma za kuhamaisha jamii isishiriki sensa

Na Salome Kitomary WA NIPASHE  - 16th August 2012.

 Jeshi la Polisi Mkoani Kilimanjaro linawashikilia watu watano akiwemo mfanyabiashara na baadhi ya viongozi wa dini la kiislamu kwa tuhuma ya kugawa vipeperushi na vitabu vyenye ujumbe wa kuhamasisha watu wasishiriki sensa ya watu na makazi 2012. Taarifa za kukamatwa kwa watu hao zimethibitishwa na Kamanda wa Polisi mkoani humo, Robert Boaz na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, Leonidas Gama.

Akizungumza na waandishi wa habari, Gama ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, alisema wapo watu kwenye wilaya za Mwanga, Same na Moshi wamekuwa wakisambaza vipeperushi na vitabu vyenye ujumbe wenye lengo la kukwamisha zoezi la sensa. “Serikali itawachukulia hatua za kisheria wote ambao watathibitika kuzuia zoezi la sensa kufanikiwa ikiwa ni pamoja na kushawishi watu wasihesabiwe…katika wilaya hizo kuna dalili mbaya kwani elimu chafu inaenezwa sana, vyombo vya usalama vipo macho na wote wanaohusika watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria za nchi” alisema Gama.

 Alisema watu hao wamefika hadi hadi kwenye taasisi za waislamu na kuwahamasisha wasishiriki zoezi hilo na kuonywa kwamba serikali ipo macho katika kukabiliana na watu wanaoendesha harakati za kukwamisha zoezi hilo. Akionyesha vipeperushi hivyo vyenye vichwa vya habari visemavyo; Ujumbe wa Ramadhani –Waislamu hawatashiriki sensa na vitabu vyenye vichwa vya habari visemavyo; Ujumbe wa kamati maalum ya maandalizi ya makongamano ya waislamu dhidi ya mfumo kristo Tanzania na Waraka wa waislam kutoshiriki sensa ya mwaka 2012.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment