Sunday, August 5, 2012

ALIYEMTEKA DR. STEVEN ULIMBOKA HUYU HAPA !!!

Aliyemteka Ulimboka huyu hapa Saed Kubenea's picture Na Saed Kubenea - Imechapwa 25 July 2012 Ni Ighondu wa Usalama wa Taifa Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Rashid Othman RAMADHANI Ighondu, afisa wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS), ndiye ametajwa kuwa mtekelezaji wa mkakati wa utekaji wa Dk. Steven Ulimboka, MwanaHALISI limegundua. Afisa huyo, licha ya kutambuliwa na Dk. Ulimboka mwenyewe, ndiye simu yake ilitumika kuandaa kikao ambako daktari alitekwa. Ni afisa huyohuyo wa usalama ambaye alikutana na Dk. Ulimboka dakika chache kabla ya kutekwa. Uchunguzi umegundua kuwa Ramadhani Ighondu (34), ni mfanyakazi wa ikulu aliyekuwa akifanya mawasiliano ya mara kwa mara na Dk. Ulimboka. Ni mfanyakazi huyuhuyu ambaye Dk. Ulimboka amenukuliwa akisema, “...alinipigia simu na kuniita kwenye kikao ambako muda mfupi baadaye nilitekwa.” Nyaraka nyeti ambazo mwandishi ameona zinaonyesha kuwa Ramadhani ndiye pia huitwa “Rama” – jina ambalo hutumia katika kujitambulisha na katika baadhi ya mawasiliano. Rekodi katika simu ya Dk. Ulimboka: Na. 0713731610 zinaonyesha Rama ndiye alifanya mawasiliano ya mwisho na daktari huyo muda mfupi kabla ya kutekwa. Aidha, ni Rama ambaye alikutana na kiongozi huyo wa Jumuia ya Madaktari Tanzania, maeneo ya Leaders Club, jijini Dar es Salaam, muda mfupi kabla ya kutekwa. Dk. Ulimboka alitekwa usiku wa 26 Juni, kusukumizwa kwenye gari, kupigwa, kufungwa mikono na miguu, kunyofolewa kucha na kutolewa meno; na hatimaye kutupwa katika msitu wa Mabwepande. Rama alifanya mawasiliano ya mwisho na Dk. Ulimboka saa 5: 52 kupitia simu yake Na. 0713 760473. Dokta alitekwa “muda mfupi” baadaye. Rais Jakaya Kikwete aliliambia taifa kwa njia ya televisheni, mwishoni mwa Juni, kuwa serikali yake haihusiki na kuteka, kutesa na kutupa daktari porini. Naye Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliliambia bunge kuwa serikali yake haihusiki na utekaji na utesaji; na kuuliza, “...serikali imteke ili iweje?” Mawasiliano katika simu ya Dk. Ulimboka yanaonyesha mtiririko wa simu za Rama wa ikulu hadi muda wa kutekwa katika eneo la Leaders Club. Vyanzo vya taarifa ndani ya idara ya usalama wa taifa vinasema, kwa sasa Rama “amehifadhiwa” kwenye jengo moja la kificho linalotumiwa na idara hiyo lililopo eneo la Ada Estate, Kinondoni, Dar es Salaam. MwanaHALISI limeweza kuthibitisha, kupitia vyanzo vya taarifa na nyaraka mbalimbali kuwa, simu Na. 0713 760473 iliyokuwa ikifanya mawasiliano ya mara kwa mara na Dk. Ulimboka, ni mali ya Rama. Huyo ndiye Ramamadhani Ighondu (Rama). Mzaliwa wa Makole, Dodoma. Mfanyakazi wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS). Idara hii iko chini ya Ofisi ya Rais (Utawala Bora) inayoongozwa na Rashid Othman. Gazeti hili limepitia nyaraka mbalimbali, likiwamo daftari la kudumu la wapigakura lililoandaliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ili kupata fununu zaidi juu ya tuhuma za Dk. Ulimboka kwa Rama. Katika daftari hilo ambalo limetumika kwenye uchaguzi mkuu uliopita, Rama anaonekana kujitambulisha kama ifuatavyo: Ramadhani Ighondu, Nickname: Rama Born: 28.08.1978 Place: Makole – Dodoma Voter Registration Card: 49406879 Mobile Number: 0713 760473 Dk. Ulimboka ambaye anaendelea na matibabu nchini Afrika Kusini, amethibitishia MwanaHALISI kuwa mtu ambaye alikuwa anawasiliana naye mara kwa mara na kumuita kwenye mkutano maeneo ya Leaders Club, 26 Juni 2012, anatumia simu Na. 0713 760473. Akizungumza kwa kujiamini Dk. Ulimboka amesema, “Ndiyo. Hiyo namba naikumbuka vizuri. Ni 0713 760473. Mwenye namba hiyo alikuwa akijitambulisha kwangu kwa jina la Abeid. Huyo bwana ndiye niliyekutana naye Leaders Club muda mfupi kabla ya kutekwa.” Alipoulizwa anawezaje kukumbuka namba iliyokuwa inafanya mawasiliano na yeye wakati kipigo alichokipata kutoka kwa watekaji kilikuwa kikubwa hadi kupoteza fahamu, Dk. Ulimboka alisema: “Ninafahamu ninachokisema. Huyo bwana nilikuwa ninawasiliana naye mara nyingi na niliwahi kukuta naye katika mgogoro ule wa kwanza wa madaktari.” Kauli hii ya Dk. Ulimboka inafanana na ile aliyoitoa kabla ya kupelekwa Afrika Kusini kwa matibabu, 30 Juni 2012. Katika mahojiano yake yanayopatikana kwenye mtandao wa kijamii wa You Tube, Dk. Ulimboka anasema, “Huyu bwana kwa muda wa siku tatu mfululizo alikuwa anajaribu kuwasiliana na mimi lakini kwa bahati mbaya ratiba yangu ilikuwa haiwezekani kumuona. “Nilishawahi kukutana naye kwenye mgogoro ule mwingine, lakini this time of course (mara hii) alikuwa serious (makini) akinitafuta…Huyu bwana anafanyakazi ikulu.” Katika mahojiano hayo, Dk. Ulimboka anasisitiza kuwa wakati anatekwa alikuwa na akili timamu na hivyo anamfahamu aliyemteka kuwa ni mtu kutoka ikulu. Dk. Ulimboka anasimulia “mtu wa ikulu” alivyoingia kwa gari pale walikomwambia wameketi na kumuuliza iwapo alikuwa na Deo (Dk. Deogratias Michael) na kwamba walianza majadiliano yaliyohusu hali ya mgomo na jinsi wao walivyokuwa wakiona unaweza kutatuliwa. “Sisi tukasema mambo yote yanafahamika. Tukaongea naye kwa muda mfupi tu; akawa anaandika… kwa hiyo pia alikuwa very busy communicating, (akionekana kujishughulisha zaidi na mawasiliano ya simu). Unaona?” MwanaHALISI limegundua kabla ya Dk. Ulimboka kutekwa, Rama alianza kufanya mawasiliano naye saa 12: 25 jioni. Mawasiliano hayo yaliendelea 3:29 usiku, saa 4: 52, saa 5: 27, saa 5:40 na mwisho ilikuwa saa 5:52 usiku. Haya ndiyo mawasiliano ambayo Dk. Ulimboka aliishasimulia kuwa yalielekea katika kukutana kwake na mwenye simu Na. 0713 760473. Ni mwenye simu hii aliyeandaa mkutano, anakumbuka Dk. Ulimboka. Kabla simu ya Rama kumwita Dk. Ulimboka kwa mara ya kwanza siku hiyo, saa 12:25, ilifanya mawasiliano na Buruani Ntilongwa, mmiliki wa simu Na. 0712 359533. Mawasiliano hayo yalifanyika kati ya saa 2: 08 na 2: 24 usiku. Aidha, nyaraka zinaonyesha kila pale Rama alipowasiliana na Dk. Ulimboka, alifanya mawasiliano pia na Moshi Marungu Shabani anayemiliki simu Na. 0761 132663 na 0655 162663. “Nakwambia ndugu yangu, kila pale ambapo Rama alifanya mawasiliano na Dk. Ulimboka, utaona hapohapo alifanya mawasiliano na Abdallah Kunja na Ntilongwa. Hawa ni watu muhimu sana kwenye sakata hili,” taarifa zimeeleza. MwanaHALISI limegundua kuwa siku mbili kabla ya Dk. Ulimboka kufanyiwa unyama huo (24 Juni 2012), simu ya Rama iliingizwa salio la Sh. 252,849. Hili ni salio kubwa pekee kuingizwa kwenye simu hiyo tangu mwanzo wa mwaka huu. Nyaraka zinaonyesha tarehe 4 Mei 2012 simu ya Rama iliwahi kuishiwa salio kabisa hadi kufikia kiwango cha Sh. 1. Kwa mujibu wa nyaraka hizo zilizosambazwa na kituo cha sheria na haki za binadamu sehemu mbalimbali duniani, Rama kila alipomaliza kumuita Dk. Ulimboka, haraka alipiga simu kwa Kunja, Ntilongwa na Marungu. Wengine ambao walikuwa na mawasilino ya mara kwa mara na Rama kabla ya kutekwa kwa Dk. Ulimboka ni: Mohammed Hassan Na. 0655 524444 Shomari Kondo Na. 0714 666304 Optat Jacob Marandu Na. 0716 611625 Mbega Hisbert Na. 0715 222778. Kwa mujibu wa kumbukumbu zilizopo kwenye daftari la wapigakura la NEC, Mohammed Hassan, ni mkazi wa Ilala, Dar es Salaam. Amezaliwa 12 Agosti 1980. Mbali na kumiliki namba hiyo, anatumia pia namba nyingine: 0717 242789. Naye Shomari Kondo amezaliwa 1 Januari 1976. Ni mkazi wa Dar es Salaam. Anamiliki simu nyingine Na. 713 671640. Marandu ametambuliwa kwenye daftari hilo kuwa amezaliwa 1979 mkoani Dodoma; huku Mbega akionyeshwa kuzaliwa 16 Mei 1978 na mkazi wa Tabata, jijini Dar es Salaam. Taarifa nyingine kutoka ndani ya idara ya usalama wa taifa zinasema, tangu 26 Juni 2012, pale jaribio la kumteka Dk. Ulimboka lilipofanikiwa, Rama aliacha kutumia simu yake hiyo. Alianza kutumia tena simu yake, tarehe 1 Julai kwa kutuma ujumbe mfupi (sms). Namba alizokuwa anatumia sana kuwasiliana kuanzia 1 Julai 2012 ni: 0714 293425 0717 030405 0713 510585 na 0715 466995. Toleo lililopita la gazeti hili lilimnukuu mtoa taarifa akisema, “Wakati wakimtesa Ulimboka, ni Rama aliyekuwa akisisitiza kuelezwa kama Ulimboka ametumwa na CHADEMA na kwamba ni nani hasa katika CHADEMA anayemtumia.” Mmoja wa watoa taarifa wa ndani ya idara ya usalama anasema, “Wazo lililopo Usalama wa Taifa ni kuwa Ulimboka anatumiwa na Mnyika pamoja na Dk. Slaa.” Wengine ambao ni maswahiba wa Rama aliowasiliana nao mara nyingi katika kipindi hicho ni: Abdi Abdi Na. 0713 229919 Najma Damian Na. 0712 704908 Spa Wilson I. Sima Na. 0712 540502 na Zulfa Swalehe Na. 0719 496505. Katika daftari la wapigakura, Abdi Abdi anaonyesha amezaliwa 1977; Spa Wilson I. Sima amezaliwa mwaka 1960 na Zulfa Swalehe amezaliwa mwaka 1950. Rama ni mfanyakazi wa idara ya usalama wa taifa aliyepo chini ya naibu mkurugenzi wa idara ya usalama anayeshughulikia siasa, Jack Zoka. Anadaiwa kushiriki kikamilifu kumtesa Dk. Ulimboka katika moja ya majumba ya kificho na hatimaye kumtelekeza msituni Mabwepande, nje ya jiji la Dar es Salaam. Uchunguzi huu unakuja baada ya gazeti hili kuripoti kuwa Zoka, ndiye mtuhumiwa Na. 1 kwenye sakata la utekaji na utesaji wa Dk. Ulimboka. Zoka anatajwa pia katika kilichoitwa “…njama za kutaka kuangamiza” maisha ya katibu mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, mbunge wa Ubungo, John Mnyika na wengine waliopachikwa jina la “wakosoaji wakuu wa serikali.” Taarifa mpya za uchunguzi juu ya maandalizi na kutekwa kwa Dk. Ulimboka, zinakuja wiki moja tangu Kamanda wa Kanda Maalum ya Polisi mkoani Dar es Salaam, Suleiman Kova atangaze kufikisha mahakamani mtu mmoja aliyedai amekiri kuhusika na utekaji wa Dk. Ulimboka. Kova aliwaambia wandishi wa habari kuwa polisi wamekamata mtu aitwaye Joshua Malundi kutoka Kenya ambaye amekiri kuteka na kutesa Dk. Ulimboka. Amedai kuwa mtuhumiwa alikwenda kutubu katika Kanisa la Ufufuo na Uzima, Kawe, Dar es Salaam. Lakini tayari mchungaji wa kanisa hilo, Josephat Gwajima amekana kauli ya Kova juu mtuhumiwa wake na kusema, “Serikali lazima ieleze vizuri.” Mchungaji Gwajima amewaambia waamini wake, “Kwanza huyo mtu hajaja kwetu kutubu...kama kutubu, basi mtu huyo angetubu huko kwao Kenya na kuhoji, “…kwani kwao Kenya hakuna Mungu?” Taarifa za kuaminika zinasema, polisi hawajawahi kuwahoji Dk. Deogratias Michael aliyeshuhudia Dk. Ulimboka akitekwa; Mkurugenzi Mtendaji wa kituo cha Sheria na haki za Binadamu (LHRC) Hellen Kijo-Bisimba wala Onesmo ole Ngurumwa, mratibu wa mtandao wa watetezi wa haki za binadamu nchini waliokwenda kumchukua polisi Bunju. Gazeti toleo lenye makala hii

No comments:

Post a Comment