TAASISI
ya Kiislamu ya Imam Bukhary iliyo chini ya Mwenyekiti, Sheikh Khamis
Khalifa, imesema kuwa utaratibu uliotumiwa na Mufti wa Tanzania, Shaaban
Simba, katika kumteua Kadhi Mkuu ni sahihi na hauna shaka yoyote kwa
kuwa umezingatia na kutimiza matakwa ya sharia za Kiislamu.
Tamko hilo limekuja ikiwa ni siku moja tangu jopo la masheikh 25
kutoka taasisi na jumuiya mbalimbali za Kiislamu Tanzania, kusambaza
tamko la kupinga uteuzi wa Mufti hivi karibuni.
Sheikh Khalifa
alisema ni jambo la kushangaza na kuhuzunisha kwa jopo la masheikh 25
kupinga utaratibu uliotumika katika uteuzi wa kadhi wakati ndiyo huo
ambao wao wenyewe waliuelezea kuwa unaokubalika kwa mujibu wa madhehebu
ya Imam Abu Hanifa na Imam Shafii, ambapo Waislamu wa Tanzania asilimia
99.9 ni wa madhehebu ya Shafii.
Alisema jopo hilo liliwahi kutoa tamko katika vyombo vya habari
Agosti 13 na 16 mwaka huu kuwa mwenye mamlaka ya kumteua kadhi katika
dola ya Kiislamu ni Khalifa, sultan au rais kwa vile ndiye mwenye haki
kimsingi ya kufanya kazi anazostahili kufanya kadhi.
“Tamko la masheikh hao lilisema kwa mujibu wa Fik’hi (sheria) ya
Kiislamu kwa kufuata madhehebu ya Imam Abu Hanifa na madhehebu ya Imam
Shafii, iwapo Waislamu watahitaji kuwa na kadhi katika nchi ambayo
haitawaliwi kwa misingi ya Kiislamu, basi kabla ya kumteua kadhi
atachaguliwa Amiri, yaani kiongozi wa Waislamu wa nchi nzima na huyo
ndiye atakayekuwa na uwezo wa kumteua kadhi akishauriana na wanazuoni
(masheikh) na watu wenye busara, kwa nini sasa wampinge?” alihoji.
Sheikh Khalifa aliongeza kuwa kwa mujibu wa utararibu huo, kiongozi
aliyechaguliwa kuwaongoza Waislamu wa Tanzania nzima kwa uwakilishi wao
ni Mufti Sheikh Simba, ambaye alichaguliwa kwa uwakilishi wa masheikh
kutoka mikoa na wilaya zote za Tanzania Bara na ndiye mwenye jukumu la
kumteua kadhi pia.
Alisema ni jambo la fedheha na aibu kwa jopo hilo kujaribu kuwahadaa
Waislamu kuwa utaratibu haukufuatwa huku wakiuficha ukweli kuwa sababu
ya kupinga ni kutokana na aliyeteuliwa hatokani na kikundi chao cha
Answar Sunna.
Alisema katika taarifa yao wamedanganya kwa kudai kuwa kadhi
alistahili kuchaguliwa na taasisi, wakati tamko lao wenyewe linasema
wazi kuwa anayestahili kumteua kadhi ni kiongozi mkuu aliyechaguliwa
kuwaongoza Waislamu katika nchi husika.
”Hakuna mahala popote katika Sharia ya Kiislamu panapohusisha wingi
wa taasisi katika uteuzi wa kadhi bali Sharia inaonesha mwenye uwezo huo
ni mtawala wa dola au kiongozi mkuu wa Waislamu aliyechaguliwa katika
nchi husika.
“Hata hivyo, ingawa sheria inampa uwezo wa kumteua kadhi japo na
washauri wake wachache, Mufti Simba alimteua Kadhi Mkuu, Sheikh Abdallah
Mnyasi, kwa ushauri wa tume ya dini nchini, ambayo inajumuisha wajumbe
wa Baraza la Ulamaa taifa pamoja na masheikh wa mikoa na wilaya zote
hapa nchini,” alisema Sheikh Khalifa.
Aidha, aliwataka Waislamu kote nchini kumtambua Kadhi Mkuu ambaye ni
mwazuoni aliyebobea katika elimu ya Sharia ya Kiislamu, na kupeleka
mashauri ya Kiislamu kwenye mahakama hiyo ili kupata uamuzi wa kisharia.
Sheikh Khalifa alisema ni vema kwa Waislamu kupuuza propaganda za
kikundi hicho cha masheikh wa Kiwahhabiyya ‘Answar Sunna’ ambacho
kinapinga uteuzi wake baada ya kuwatupa nje masheikh wao.
Alisema kuwa hapa nchini maanswar Sunna ni kikundi cha watu wachache
kilichozuka siku za karibuni, ambacho kila wakati kinajihusisha na
vurugu miongoni mwa Waislamu watulivu kila mahala walipo.
“Hivyo
haiwezi kuwa busara kwa Kadhi Mkuu atokane na kikundi hiki ambacho hata
utaratibu wao wa kidini unatofautiana na Waislamu asilimia 99 katika
nchi hii,” alisema Sheikh Khalifa.
Aliongeza kuwa masheikh hao
wanatakiwa wajitambulishe kwanza wao ni wafuasi wa madhehebu gani na
wanataka kadhi ateuliwe kwa kufuata utaratibu upi kisha wakae kikao chao
na wafuasi wao wamteue kadhi wao atakayehusika na mashauri yao kuliko
kupoteza muda.
No comments:
Post a Comment