Sunday, August 5, 2012
RUSHWA YAVURUGA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA !
RAIA MWEMA
On Aug 2, 2012
Rushwa yavuruga Bunge
Mwandishi Wetu
Toleo la 252
1 Aug 2012
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe
BAADA ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Katibu wake Mkuu, Eliakim Maswi, kunusurika kung’olewa na mtandao wa mafisadi kupitia kwa wabunge wanaodaiwa kupewa rushwa kutimiza azma hiyo, taarifa zinaeleza zamu inayokuja ni dhidi ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.
Membe anatarajiwa kuwasilisha hotuba yake bungeni wiki ijayo, na inaelezwa kwamba msimamo wake dhidi ya watuhumiwa wa kashfa ya ununuzi wa rada umemfanya kusubiriwa kwa hamu na baadhi ya wabunge ambao nao wanaelekezewa tuhuma kupewa fedha na mafisadi ili kushinikiza kumng’oa waziri huyo au hata kumchafua wakati wa mjadala wa bajeti ya wizara yake.
Maandalizi hayo dhidi ya Waziri Membe yanakuja katika wakati ambao, vyanzo kadhaa vya habari vya gazeti hili vinamnukuu Rais Jakaya Kikwete akipata kumweleza Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kwamba; “nimechoka kuapisha mawaziri wapya,” akiwa na maana hataki kumpoteza waziri yeyote kwa sasa.
Kikwete anakaririwa kutoa kauli hiyo baada ya joto la mafisadi kupitia wabunge kutaka kumng’oa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter na Katibu wake, Maswi ambao wanaaminika kudhibiti mirija ya unyonyaji ya mafisadi iliyopachikwa katika Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
Mpambano uzalendo vs ufisadi
Katika harakati za kuokoa jahazi na kudhibiti nguvu ya mafisadi katika kuwang’oa viongozi wa Wizara ya Nishati na Madini, baadhi ya mawaziri, wabunge na timu nyingine maalumu zilizoshirikisha viongozi kutoka makao makuu ya CCM, zilishiriki huku baadhi ya wabunge wa kambi ya upinzani wakiunga mkono juhudi hizo katika imani ya kupigania maslahi ya Taifa.
Taarifa zilizotufikia zinaeleza kuwa stahili iliyokuwa ikitumiwa ni kupita kila walipokuwa wakipita ‘mawakala’ wa ufisadi ambao nao walikuwa wakiwaona wabunge mmoja mmoja kwa kuzingatia orodha waliyojiandalia.
Katika juhudi hizo, Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka, anadaiwa kulazimika kutumia usafiri wa bajaji nyakati za usiku kupita kwa baadhi ya wabunge ili kuwaeleza hali halisi ni kwa nini viongozi wapya wa Wizara ya Nishati na Madini wanapigwa vita.
Mbali na Waziri Kabaka, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Stephen Masele, ambaye ni Mbunge wa Shinyanga Mjini, naye alikuwa na kazi maalumu ya kupita kila alipokuwa akipita mbunge mmoja kutoka moja ya majimbo mkoani Arusha (CCM).
Inadaiwa kuwa mbunge huyo alikuwa na kazi ya kusambaza fedha ili ‘kuwanunua’ wabunge wafanye mashambulizi dhidi ya uongozi wa wizara, fedha ambazo alizipata kutoka kwa baadhi ya kampuni zilizowahi kufanya biashara na TANESCO kwa njia za kifisadi.
“Kazi ilikuwa moja tu, wao wanapoondoka katika ‘kijiwe’ fulani baada ya kugawa fedha sisi tulikuwa tunakwenda kueleza ukweli na kwa kulinda maslahi ya nchi badala ya maslahi ya genge la wafanyabiashara wanaotafuna nchi,” alieleza mtoa habari wetu.
Mbunge wa Mwibara, Alphaxard Kangi Lugola naye anadaiwa kutembea kilomita kadhaa bila usafiri wa chombo chochote, akitoka hoteli moja kwenda nyingine ili kuweka mambo sawa kwa kufichua ukweli kwa wale waliopewa rushwa.
“Kazi ilikuwa moja tu ambayo ni rahisi. Ilikuwa ni kazi ya kusema ukweli, kwa maslahi ya nchi. Tulikuwa tunasema fedha za rushwa zimetoka kwa nani, kwa sababu gani na kwa maslahi ya nani na kwa malengo gani hasa dhidi ya nchi,” alieleza mtoa habari wetu.
Waziri Mkuu na Rais Kikwete
Taarifa zilizotufikia zinaeleza kuwa siku chache kabla ya joto la mafisadi kupanda na kuelekea kutaka kufanikiwa, Rais Kikwete anatajwa kumwita Waziri Mkuu na kumweleza kuwa amechoka kuapisha mawaziri wapya.
Kauli hiyo ni kama ilikuwa agizo kwa Waziri Mkuu ambaye kichwani mwake alikuwa na kumbukumbu ya shinikizo la wabunge lililosababisha kusukwa upya kwa Baraza la Mawaziri.
Baada ya hapo, Pinda aliitisha kikao cha wabunge wa CCM walioko katika Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini. Wengine waliokuwamo katika kikao hicho ni pamoja na Spika wa Bunge, Anne Makinda, Waziri Profesa Muhongo na Katibu Mkuu, Maswi.
“Kikao kilidumu kwa saa sita hivi. Hali ilikuwa tete na Katibu Mkuu aliwaumbua baadhi ya wabunge. Aliwataja kwa majina wanaonufaika na TANESCO ambao ndio hao waliokuwa wakitetea viongozi waliosimamishwa kazi TANESCO warejeshwe.
“Wabunge wawili wa Viti Maalumu walirushiana matusi pale. Mmoja alimwambia mwenzake anatetea ufisadi wa TANESCO kwa kuwa anafanya biashara na shirika hilo, naye alisimama kumjibu bora yeye anafanya biashara na TANESCO kuliko mwenzake huyo anayefanya biashara kwa kuuza mwili wake.
“Maswi pia alimkumbusha mbunge mmoja namna alivyowahi kwenda kumwomba rushwa ya shilingi milioni 50 ili aende akawagawie wenzake. Alipomwambia hana kiasi hicho cha fedha alipunguza dau hilo hadi shilingi milioni 20. Ushahidi wa hilo umehifadhiwa na utawasilishwa sehemu husika,” kinaeleza chanzo chetu cha habari.
Malecela aitwa kuokoa jahazi
Waziri Mkuu wa zamani, John Malecela, alilazimika kutumika pia. Waziri Mkuu Mizengo Pinda anatajwa kumwomba amweleze hali halisi mbunge mmoja kutoka mkoani Arusha ili aache kuendelea kuwa wakala wa mtandao wa mafisadi waliokuwa wakinufaika na TANESCO.
“Mzee Malecela alikaa na .... mbunge (jina linatajwa) akamweleza kila jambo lakini jamaa alikuwa kichwa ngumu. Mzee alimwambia unakwenda kujimaliza kisiasa siku si nyingi, yeye akaendelea na msimamo wake, kwa hiyo Mzee akamwacha na sasa hali yake kisiasa ni mbaya. Yeye ni sehemu ya wabunge wanaotuhumiwa kwa rushwa,” kinaeleza chanzo chetu cha habari.
Siri ya wabunge kuomba rushwa
Siri za baadhi ya wabunge wa Bunge na hasa katika kuomba na kupokea rushwa nazo zimezidi kuanikwa na baadhi yao, wakilielezaRaia Mwema kwamba, wengi waliochukua mikopo ya hadi shilingi milioni 200 na kuanzisha biashara, biashara hizo zimekufa na mshahara wao ‘unatumikia’ mikopo hiyo na kwa hiyo, hawana chanzo kingine cha mapato.
Kutokana na hali hiyo, wabunge wamekuwa wakililia nyongeza ya mishahara na posho na kwa kupitia kamati zao wengine wanadai hufanya shinikizo la kupewa semina na baadhi ya mashirika na taasisi za umma.
Baadhi ya wabunge waliozungumza na gazeti hili kwa sharti la kutotajwa gazetini wamesema mbali na wabunge kuwa katika hali hiyo ngumu, kuna udhaifu wa serikali kiasi cha kuacha wabunge kuingilia shughuli za kiutendaji za kiserikali.
“Kutokana na serikali kama mhimili wa dola kuonekana kuzidiwa na Bunge na hivyo kuwa too submissive to the parliament(kujisalimisha kwa Bunge), Bunge limejikuta likitumia vibaya nafasi yake ya kuisimamia na kuishauri serikali kwa kujiingiza kwenye masuala madogo madogo ya utawala na utendaji wa siku hadi siku.
“Wameacha kuisimamia serikali katika masuala ya kisera, sasa wanakuwa mawakala wa wafanyabiashara waliokosa zabuni au wafanyabiashara wanaofutiwa leseni,” anaeleza mmoja wa wabunge kutoka Kanda ya Ziwa.
Katika kuongeza nguvu hoja hiyo, mbunge mwingine anasema; “Wanaolalamika kuonewa au vyovyote wanapaswa kwenda mahakamani na si kwa wabunge, tena kwa kuwapa fedha.
“Wafanyabiashara wengi wanaoathirika na uamuzi wa watendaji wa serikali, siku hizi hawaendi tena kortini kupinga uonevu wanaodhani wamefanyiwa, wanakimbilia bungeni kwa wabunge.”
Mbunge mwingine kutoka Nyanda za Juu Kusini anataja sababu nyingine za wabunge kudai rushwa ni mfumo wa uchaguzi wa wabunge ambao ni wa gharama kubwa na baada ya uchaguzi, wananchi waliosaidia kampeni za mbunge wamekuwa wakiwageuza wabunge kama vyanzo vya mapato yao.
Anasema wabunge pia huchukua mkopo na kuanzisha biashara ili kujiongezea kipato lakini wengi kwa kukosa utaalamu wa biashara, biashara hizo zimekufa na wakati huo huo, mishahara yao ikikatwa kwa sehemu kubwa kufidia mkopo.
‘Kamati Maliasili ivunjwe’
Baada ya wito wa kutaka kamati za Hesabu ya Mashirika ya Umma inayoongozwa na Kabwe Zitto, Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa inayoogozwa na Augustine Mrema na Serikali Kuu ya John Cheyo zivunjwe, kama ile ya Nishati na Madini kutokana na tuhuma mbalimbali za ufisadi, wito umetolewa sasa kwa Spika Makinda kuvunja kamati nyingine za Bunge.
Kamati hizo ni pamoja na Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, Kamati ya Uchumi na Fedha na Kamati ya Ulinzi, Usalama na Mambo ya Nje.
Kamati za Ulinzi na ile ya Uchumi na Fedha zinashinikizwa na baadhi ya wabunge zivunjwe kwa kuwa wenyeviti wa kamati hizo tayari uadilifu wao unatiliwa shaka mbele ya wananchi. Kamati hizo zinaongozwa na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa na ile ya Uchumi inaongozwa na Andrew Chenge.
Lowassa alijiuzulu baada ya shinikizo kutoka katika Bunge la Tisa akihusishwa na kashfa ya kampuni tata ya ufuaji umeme ya Richmond. Chenge anatazamwa kama kiongozi aliyefanikisha ununuzi wenye utata wa rada ambayo mchakato wake ulitikisa mapaka kwenye bunge la Uingereza.
Lakini wakati hali ikiwa hivyo kwa Lowassa na Chenge, Kamati ya Ardhi inayoongozwa na Mbunge wa Kahama, James Lembeli, inadaiwa kutiwa mfukoni na genge la wafanyabiashara, ikidaiwa kwamba kwa nyakati tofauti genge hilo limewahi kuwalipa posho wajumbe wa kamati hiyo ili kujadili uamuzi wa serikali wa kuzuia vibali vya usafirishaji wanyama nje ya nchi.
Kamati hiyo ya Lembeli ‘ilitiwa mfukoni’ na wafanyabiashara hao katika kikao kilichofanyika Siku ya Jumapili (Novemba 6, 2011), siku ambayo si siku ya kazi za Bunge na inadaiwa wajumbe walilipwa na wafanyabiashara hao. Semina hiyo ilifanyika katika Ukumbi wa Pius Msekwa, bungeni mjini Dodoma.
Kamati hiyo pia inadaiwa kuwahi kulipiwa ukumbi wa semina na posho kwa wajumbe wake na wafanyabiashara wa uwindaji wa kitalii, semina iliyofanyika katika Ukumbi wa Mtakatifu Gaspar, mjini Dodoma, Aprili, mwaka huu.
Chazno: Gazeti la RaiaMwema
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment