Wednesday, April 8, 2009

ZIARA YA WODI YA WAZAZI SIBLEY MEMORIAL HOSPITAL

Mchapo wa leo ndugu zangu ni kutoka Hospitali ya Sibley Memorial Hospital iliyopo Washington DC. Nilikwenda huko kumwona rafiki yangu Michelle Maharajh Brown aliyejifungua mtoto wa kiume juzi tarehe 6 Aprili, 2009. Yeye alijifungua kwa upasuaji.

Leo ndio nilipata nafasi ya kwenda kumtembelea huko hospitali na niliyoyaona nimeona sina budi kuwafahamisha ndugu zangu Afrika jinsi mambo yalivyo tofauti na kwetu.

Nilipofika ofisi ya mapokezi nikauliza jina la mgonjwa wangu nikafahamishwa nipande gorofa ya tatu kushoto chumba Na. 315 ndiko aliko. Nilipomaliza lifti na kufika ghorofa husika nikaelekea nilikoelekezwa nikakuta geti. Hapo geti lake halifunguliwi hadi ugonge kengele ili ufunguliwe na walioko ndani. Kuna tangazo mlangoni linasema kwamba hawaruhusiwi watoto wodi ya wazazi isipokuwa kama watoto hao ni ndugu wazaliwa na mgonjwa/au mtoto aliyezaliwa.

Nikagonga kengele nikafunguliwa. Nikaelekea Chumba Na. 315. Kufika hapo nikasikia kwa ndani mtoto analia kwa sana (anabalaluka). Nikaingia na kuambiwa kuwa tangu azaliwe mtoto huyo saa 48 zilizopita, hajapata rizki yoyote kwa sababu maziwa ya mama yake hayajaanza kutoka. Akaitwa na akaja Dakitari wa watoto akamchukua mtoto na kwenda kumpima kabla ya kumpa maziwa ya ng'ombe. Dakitari akasema mtoto aliyezaliwa Paundi 7.15 amepungua ratili 0.15. Hiyo imetokana na njaa aliyokuwa nayo kwa saa 48 zilizopita. Hivyo akapewa hayo maziwa akayanywa kwa bidii zote na baada ya kunywa akalala usingizi fofofo.

Kisha Dakitari kamgeukia mama. Akamletea mashine ya kusukuma maziwa (pump) ili yatoke. Mimi kilichonishangaza ni kwamba ETI dakitari kasema kwa sababu chuchu ya mama ni tambarare (flat), mtoto anashindwa kuinyonya. Nikamjibu kwamba Chuchu nyingi za wanawake ziko hivyo. Zinabunuka tu baada ya kuanza kunyonywa na watoto. Kwa hiyo kadri mtoto anavyofanya jitihada ya kunyonya na kuvuta chuchu ndio chuchu itakavyojitokeza na ndivyo kadri ya maziwa ya mama yatakavyotoka.

Wakaniona mimi sijui. wakamwekea mzazi kimpira mfano wa chuchu juu ya chuchu yake asilia. Hivyo mtoto akawa ananyonya ile chuchu bandia aliyowekewa mama yake. Kwa elimu ya kuzaliwa niliyonayo, sikudhani kwamba ile chuchu bandia inaweza kumsaidia mzazi kutoa maziwa kwa mtoto wake mchanga.

Kabla sijaondoka, ikaletwa pampu ya umeme na vikorombwezo vyake kibaaaao. Mzazi akaelekezwa jinsi ya kuiwasha na kuitumia ile mashine ambayo kazi yake ikawa ni kama ile ambayo ingefanywa na mtoto. Yaani ya kuyafanya maziwa ya mama yatoke haraka iwezekanavyo ili mtoto apate chakula. Mashine hiyo (pampu) inawekwa juu ya matiti yote mawili juu ya chuchu na inafanya kazi kama ya kuvuta maziwa ya mama kwa muda wa robo saa na kisha inapumzishwa. Shughuli hiyo inaendelea kwa mara zozote awezazo mzazi kumudu ili mradi haina mipaka maalum kama mara moja au mbili kwa siku. Dakitari akasema anataraji kwamba kwa kutumia mashine hiyo, maziwa ya mama yanatarajiwa kutoka ndani ya saa 24 zijazo.

KISANGA kinakuja pale atakaporuhusiwa kuondoka kurejea nyumbani na kitoto kichanga chake. Sheria za Marekani zinasema hakuna mzazi anayeruhusiwa kuondoka kwa kutumia taxi (public transport). Lazima gari atakayosafiri nayo toka Hospitali hadi nyumbani iwe ni gari binafsi. Pili gari hiyo lazima iwe na kiti cha mtoto mchanga kinachochomekwa katika kiti cha nyuma cha gari. Pamoja na hayo sheria ya matumizi ya kiti hicho ni kwamba lazima kiwekwe kiti cha nyuma na mtoto anaangalia nyuma ya gari sio mbele. Mzazi atajijua atakapokaa hadi watakapofika nyumbani. Ili mradi mzazi wa mtoto ni marufuku kumpakata au kumbeba mtoto anapotoka hospitali. Kuhakikisha sheria hiyo inatekelezwa ni kwamba kuna nesi maalum anayekagua gari hiyo kabla mtoto na mama yake hawajaruhusiwa kuondoka. Huyo nesi akishakagua na kuridhika kuwa sheria imetekelezwa ndio mama na mtoto wtaruhusiwa kuondoka. Hayo ndio maendeleo ya Nchi zilizoendelea.

No comments:

Post a Comment