Wandugu kutoka Afrika na nchi zinazoendelea, haya ni masahibu/maelezo machache tu yanayotulazimu kuyajua katika kupata huduma ya tiba yoyote ile nchini Marekani.
1. Kama sio dharura (yaani kama sio ajali yoyote, n.k.), ni lazima ufanye miadi (appointment) kiasi kama cha muda wa miezi miwili kabla ya tarehe ya kumwona dakitari.
2. Katika kufanya miadi hiyo, unakwenda kwenye ofisi ya dakitari na unapewa fomu za aina mbili au tatu tofauti za kujaza. Ndani ya fomu hizo; fomu mojawawapo, mbali na taarifa za kawaida kama jina kamili anuani unapoishi, namba za simu na wadhamini wako, unatakiwa kuelezea magonjwa yanayokusibu, magonjwa yanayowasibu familia yako na magonjwa yanayosibu ukoo wako, dawa au vyakula ambavyo vinakusibu (allegies), na magonjwa ambayo uliwahi kuugua huko nyuma, na upasuaji uliowahi kufanyiwa huko nyuma.
3. Fomu nyingine unaelekezwa tarehe ya kwenda kumwona dakitari na unachagua dakitari unayetaka akuhudumie kwa aidha jina lake au jinsia yake. Kisha katika hiyo fomu ndio kuna mkataba pia wa ahadi yako (sio tiba) ambao unasema kwamba unatakiwa ufike nusu saa au dakika 20 kabla siku uliyopangiwa kumuona dakitari. Pia mkataba huo unasema kwamba endapo utashindwa kufika siku na saa ya miadi, angalau uwapigie simu saa 24 kabla ili wampange mtu mwingine katika sehemu yako. Na endapo hukufanya hivyo ukamezea tu kwa kukaa kimya na usionekane muda wako ukifika, basi utalipia $25.0 (sawa kama na Tshs.25,000/=). Hivyo ukiweka miadi ya kumuona Dakitari huku, ni heri uhakikishe unafika au adhabu ndio hiyo.
4. Ukishafika siku na saa husika, unatakiwa uandike jina lako kwamba umefika. Majina yanaandikwa kwa namba. Kwa mfano jina langu lilikuwa Na. 15 katika orodha. Karani aliyenipokea kaniuliza endapo nimekuja na nambari ya Bima itakayogharimia matibabu yale. Mimi sikuwa na hiyo nambari, hivyo nikalazimishwa kusaini mkataba mwingine wanauita "Waiver". Hii maana yake ni kwamba, endapo Kampuni niliyosema itanilipia itapelekewa bili ya tiba hii na kuniruka (kukataa kulipa), maana yake deni hilo linageuka kuwa deni binafsi na kwamba mimi mwenyewe ndio nitalazimika kulilipa.
5. Baada ya hapo unaitwa kwa dakitari. Hapo unakuta nesi anayechukua uzito wako na urefu wako. Pia anakuuliza endapo unaumwa kitu gani kwa wakati ule. Pia anakuuliza endapo umewahi kufanyiwa upasuaji wowote katika maisha yako huko nyuma. Pia anakuuliza endapo kuna dawa hutumii (allergic).
6. Kisha anakuja Dakitari na yeye anarudia maswali ya nesi. Kisha anakufahamisha nini atakachokufanyia katika utaratibu wa vipimo. Kisha anakuacha na karatasi mbili; moja ni kama joho linalovaliwa na wagonjwa wakati wa uchunguzi na la pili kama kanga au gagulo; ya kuvaa chini yake. Daktari atauliza katika magonjwa ulioyoorodhesha katika Mkataba siku uliyofanya miadi uliugua wakati gani na katika mazingira gani. Kwa mfano mimi aliniuliza nilifanyiwa upasuaji wa kidole mwaka gani na kwa sababu gani? Nilikiuguzaje kidonda, nk.
7. Mimi kama mzazi aliniuliza nina watoto wangapi na wana umri gani na nilimaliza kuwa mzazi mtarajiwa mwaka gani (yaani nilipokata siku za kike - menopause). Pia endapo watoto wangu niliwazaa katika mazingira gani. Kama walizaliwa kwa Siza(upasuaji) au walizaliwa kwa njia ya kawaida. Baada ya hapo Dakitari anakuacha uvue nguo ili uvae hizo karatasi nilizotaja hapo juu.
8. Ukishakuwa tayari ndio sasa dakitari anakuja kukupima kutegemea na kipimo utakacho. Kwa upande wangu, dakitari akaanzia kunipima mapigo ya moyo. Baada ya hapo akanipima maziwa na tumbo na kuendelea na kuchunguza hadi miguuni. Baada ya hapo dakitari akanishauri kuwa mwepesi wa kupima matiti mara moja tu mwanzoni mwa mwezi. Dakitari kisha akanipa vipeperushi vya namna ya kujipima binafsi matiti hayo, na aina ya vyakula vya kutumia katika umri wangu wa miaka 55. Akasema kwamba kwa kuwa mifupa inalegea tokana na umri mkubwa, amenihimiza nikatumie vyakula vyenye madini mengi ya Kalshiam (calcium) ili inijengee mifupa imara isiyotetereka. Katika mojawapo ya vyakula hivyo ni kula bamia la kuchemsha kwa wingi na matunda aina ya machungwa (citrus).
9. Hivi vipimo nilivyochukuliwa hapa ni mwanzo tu. Natakiwa nikafanyikwe kipimo kingine baadaye cha kuthibitisha endapo nina saratani au la; kipimo ambacho hufanywa kwa kutumia mionzi (radiation). Nimepewa namba ya simu ili nipige simu huko niweke miadi mingine juu ya kufanyiwa kipimo hicho cha mwisho.
10. Jamani kweli huku matibabu au huduma ya tiba inafanywa kwa uangalifu mkubwa sana. Maana huku dakitari au nesi akifanya kosa lolote la kizembe kwa mgonjwa ni Mahakamani hakuna msalie.
Jambo hili linanikumbusha jinsi kichanga binamu yangu alivyokufa hospitali ya Mkoa wa Morogoro mwaka 2005 tokana na uzembe wa manesi. Baada ya mama mtu, ambaye kwake ulikuwa uzazi wa kwanza kujifungua; manesi walimfunga mtoto wa kiume aliyempata katika kanga na wakasahau; ETI WALISAHAU kumfunga mtoto kitovu. Mtoto yule alikufa kwa sababu ya kutokwa damu nyingi kupitia kutovuni. Hakuishi hadi saa 24. Kesi hii ingekuwa huku naona manesi wale wote waliomhudumia mzazi yule wangefutiwa leseni zao za kufanyia kazi. Lakini huko nchini kwetu Tanzania, wanapeta tu kwa unyonge wa mzazi mwenyewe na kwa kutokujua kwamba angechukua hatua gani baada ya kosa lile. Ni katika kutumia usemi ule wa kwamba hata "nikishitaki mtoto nimeshamkosa". Lakini watu kama hawa wangeshitakiwa, wasingerudia kabisa uzembe au kufanya makosa ya kupoteza maisha ya binadamu kama vile ilivyotokea.
Umetoa mwanga mzuri sana kwa watu ambao huwa wanajiuliza kuhusu matibabu yanavyofanyika nchini Marekani!
ReplyDeleteMaelekezo mazuri kabisa na yaliyo sawia!