Tuesday, April 21, 2009

WANASIASA WAKIBEZA VYETI BANDIA SAWA LAKINI SIO VITIVONI

Wanasiasa wakebehi vyeti vya elimu kuchunguzwa uchagauzi 2010


Na Fidelis Butahe na Salim Said

SIKU moja baada ya Kamisheni ya Vyuo Vikuu nchini (TCU) kutangaza nia yake ya kuhakiki vyeti vya wagombea 2010, baadhi ya wanasiasa wameponda mpango huo kwa madai kuwa umewekwa mahali pasipohusika.

Juzi Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Mayunga Nkunya alisema ukubwa wa tatizo la wagombea kutokuwa na elimu linazidi kudhihirika kutokana na taasisi mbalimbali kuzidi kufichua walioghushi vyeti ili kupata elimu ya juu.

Profesa Nkunya alisema hatua madhubuti zisipochukuliwa kiwango cha elimu kitazidi kuporomoka na hali ya usalama wa taifa itakuwa hatarini.

Pia alimtaka Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi nchini kuwasilisha vyeti vya wagombea mbalimbali wa nafasi za uongozi ili kuthibitisha sifa wanazojinadi kuwa ni kweli au la.

Wakizungumza na Mwananchi jana kwa nyakati tofauti baadhi ya wanasiasa walisema, sifa za mtu kuwa mgombea wa uchaguzi katika nafasi fulani hazihusiani na kiwango chake cha elimu.

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Ibrahim Lipumba alisema mpango huo, umewekwa mahali pasipohusika kwa sababu ili mtu agombee anatakiwa kujua kusoma na kuandika na kufafanua kuwa suala la elimu halina nafasi katika siasa.

“Tume ya uchaguzi inafanya kazi na sheria ya uchaguzi, ninachofahamu ni kwamba mgombea anatakiwa kujua kusoma na kuandika, sasa hao TCU wanapozungumza suala la elimu na vyeti tuwaulize lipo katika kipengele gani cha sheria.

“Nimepata taarifa nyingi juu ya wabunge wanaoghushi vyeti sina tatizo na hilo ila ninachosikitika ni kwamba suala hili limepelekwa mahali ambako si pake,” alisema Lipumba.

Alisema TCU inatakiwa kutambua sifa ya mgombea miaka yote haiendani na elimu aliyokuwa nayo kwa kuwa katika ulingo wa siasa, kinachopaswa ni utendaji kazi na hoja za msingi za mgombea na si elimu wala vyeti.

Naye Katibu Mkuu wa Chama cha NCCR-Mageuzi, Samwel Ruhuza alisema suala hilo, halina msingi wowote kwa sababu wapo wanasiasa wanaojenga hoja nzito bungeni na kusaidia wananchi katika majimbo yao, bila kuwa na elimu ya juu.

Alisema katika siasa suala la elimu halina nafasi kwa sababu hata vigezo vya Tume ya uchaguzi kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi, wagombea wanatambuliwa kwa kujua kusoma na kuandika na hakuna kipengele kinachuzungumzia suala la kiwango cha elimu kwa mgombea.


Maoni yangu:

Waheshimiwa viongozi wa vyama mbalimbali na Wabunge wanachosema ni sawa; kwamba; Ibara ya 67 (1)(a) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 inatamka wazi kwamba "...mtu yeyote atakuwa na sifa ya kuchaguliwa au kuteuliwa kuwa mbunge endapo ni raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliyetimiza umri wa miaka ishirini na moja (21); na ambaye anajua kusoma na kuandika katika Kiswahili au Kiingereza."

Kipengele hiki hata hivyo hakimuondoi hatiani Mbunge yoyote yule ambaye anafahamu kwamba cheti chake anachojisifia nacho ni cha kughushi. Hii ni kwa sababu kughushi ni kosa la jinai la Udanganyifu. Ni bora wangekiri kwanza kuwa wamefanya udanganyifu huo kisha umma wa Watanzania wawafikirie kuwasamehe au kuwafikisha Mahakamani kwa Udanganyifu wao.

Wahusika wakisubiri Tume ya Vyuo Vikuu nchini kuwaanika, maana yake wote wahusika wameshiriki katika kufanya Udanganyifu huo, hata kama walipopata vyeti hivyo, hawakufahamu kuwa vilikuwa vimeghushiwa (unaccredited). Hii ni kutokana na sababu kwamba serikali ilishawataka wote wanaohisi au kufahamu kwamba vyeti vyao havina sifa wavisalimishe ili vihakikiwe kisheria.

No comments:

Post a Comment