Friday, April 10, 2009

JAJI WA MAHAKAMA YA RUFAA HAONI TABU KUJIFULIA NGUO

Leo nina habari za Jaji Mweusi Pekee katika Mahakama ya Rufaa ya Shirikisho nchini Marekani (United States Supreme Court) Mheshimiwa Jaji Clarence Thomas ambaye gazeti la "The Examiner" la Washington DC, la tarehe 2 Aprili, 2009 lilimnukuu juu ya mambo mengi tu kama ifuatavyo; kama alivyonukuliwa katika Hafla ya Jioni (gala) ya Asasi ya Haki za Binadamu (Bill of Rights Institute): Kwa bati alilopiga kichwani (mvi), naweza kuthubutu kusema kuwa ana umri wa miongo kama 6 hivi au keshaimaliza (60s).

"This is a rare sighting for me to be out during the week, especially a sitting week," akiwa na maana kwamba ni nadra sana yeye kukubali mialiko kama hii wakati Mahakama ikiwa kazini. Yaani anakuwa bize sana na kazi za kusoma kesi, kusikiliza kesi na kuandaa hukumu za kesi wakati huo.

"I would like to thank my bride for being here. We have been a team for a while and enjoy each other a lot, ... I tend to be morose; she tends to be energetic." Hapa ana maana kwamba anamshukuru sana mkewe aliyenaye na ambaye wamekuwa kama timu, wakati yeye akiwa anatafakari mambo ya kisheria, mkewe anakuwa mchangamfu kwa maana ya kwamba hawi kikwazo katika utendaji wake wa kazi za kila siku na wala halalamiki kwa hilo.

Anasema anapojisikia kulemewa na majukumu yake, "when he feels down" huwa anamgeukia mkewe "what I tell my wife is the 'Inter-Net', and I look up great speeches, like General Douglas MacArthur's speech at West Point." Hapa huenda akawa ana maana kwamba mkewe humsaidia katika kuzisikiliza au kupekuwa kwenye tovuti, Hotuba za waliomtangulia kama ya Kamanda huyu maarufu wa majeshi aliyemtaja.

Na itokeapo kwamba mambo yanakuwa kama kawaida, huwa anakwenda "pangoni" (basement) kuangalia mchezo wa kuigiza wa Televisheni wa "Saving Private Ryan".

Kwa sisi Waafrika hatuna mfano wa hili pango ninalozungumzia hapa. Huku Marekani, nyumba nyingi huanzia ghorofa moja au zaidi chini ya ardhi. Zinazoitwa Basement. Kama kwa mfano sehemu niliyopanga mimi. Naishi chini ya nyumba na hii ni studio basement kwa sababu inajitegemea (haichangii mlango wala maliwato. Ndio kwa DC nalipia $1,200 kwa mwezi. Kwa fedha zetu kwa wastani tu ni sawa na Tshs.1,200,000/=) za Tanzania. Pango la nyumba katika jiji hili kuu la Serikali hii ni kiboko.

Mheshimiwa huyu anaendelea kusema "I have to admit that I am one of those people that thinks the dishwasher is a miracle, I like to load it." Yaani, anakiri kwamba yeye ni kati ya watu wanaofikiri kwamba mashine ya kuoshea vyombo ni muujiza, hivyo anapenda sana kupangilia vyombo humo ili vioshwe na mashine hiyo.

"I still take out the trash, and me and my wife go to football games. We go motor-homing."
Mheshimiwa anasema hadi leo hii bado anakusanya na kutupa taka za nyumbani mwake, na pia huenda kuangalia michezo na mkewe. Pia wanapenda kuishi katika gari.


Kuishi katika gari huku Marekani ni sehemu ya utamaduni wao. Yaani mtu anakodi au ananunua gari/nyumba, gari hizi ni kama nyumba kwa sababu zina kila aina ya huduma ya nyumba ndani yake. Kwa hiyo ukiwa na gari kama hii, unaweza kuamua kwenda utakako, bila ya kuwa na gharama ya malipo ya malazi wala kula hoteli. Wapo watu nchini Marekani wanaoishi maisha yao yote katika nyumba zitembeazo kama hizi. Na wengine nyumba hizi huzipigia kambi ( kambi zinalipiwa) kwa maana ya kwamba mtu anaweza akapiga kambi katika nyumba hiyo bila ya kulazimika kutembea nayo. Na hizi kambi zipo katika miji maalum na sehemu maalum zilizotengwa kwa ajili ya gari za aina hii kupiga kambi. Kwa watembeao kama Mheshimiwa huyu, anapofika katika kambi hizi, inabidi alipie kwa siku, au wiki, au mwezi, n.k.

Alipoulizwa maoni yake juu ya Mahakama Kuu kabisa ya Marekani na jinsi ilivyombadilisha akajibu "not a whole lot. It's changed my hair. It's given me some girth." Anajibu kwamba Mahakama imemzeesha kwa kumuongezea bati alilo nalo kichwani (mvi) na kwamba imemuongezea uzito (kwamba sasa amenenepa). Mheshimiwa huyu hapa ana maana ya kwamba uzito wa kazi za Mahakama hii haumpi nafasi ya kutosha ya kufanya mazoezi, na kwamba kule kufikiri sana masuala mazito ya kesi wanazoshughulikia ndio zimemuongezea mbuliza (mvi)

Juu ya kazi yake ya Ujaji anasema "This job - it's easy for people who have never done it. What I've found is they know more about it than I do. Espeically if they have the title of law professor." Anasema kazi yaonekana rahisi kwa watu wasioifanya. Nimegundua kwamba walimu wa sheria wanaifahamu zaidi kazi hii kuliko mimi. (hapa bila shaka alikuwa anatania kwa sababu mjuaji wa kazi yoyote ni mtendaji kazi ile, sio mjua nadharia yake).

Mahakama ya Juu kabisa ya Rufani nchini Marekani ina majaji tisa tu. Katika Chumba cha Mahakama Majaji hawa hukaa kwa uzoefu wao (seniority). Jaji Mkuu anakaa kiti cha katikati. Anayemfuata anakaa kulia kwake, na kushoto kwake atakaa anayemfuata huyu. Na kulia kwake ni hivyo hadi wote waketi. Mheshimiwa jaji Clarence Thomas hukaa upande wa kulia (kwa Jaji Mkuu) wa meza ya majaji kabla ya Jaji wa mwisho kulia kwake.

Mheshimiwa Jaji huyu katika Kesi za Mahakama hii huwa ni Msikilizaji tu. Huwa haulizi maswali japo hii ni fursa kwa Majaji kuuliza swali lolote kwa mtoa hoja awe mtetezi au mshitaki.

No comments:

Post a Comment