Sunday, April 5, 2009

TEMBEA UONE - (TRAVEL IS THE GREATEST EDUCATOR)

Kwa kweli leo nimetembea na nimeona.

Tulivyozoea utamaduni wetu wa ukarimu wa Mwafrika, huku Marekani haupo; tena mwenye udhuru unashukiwa kuwa ni mhalifu.

Mimi nilikuwa natembelea maeneo yaliyotangaza biashara za mitumba majumbani. Huku Washington DC, USA, biashara ya mitumba haifanywi sokoni kama nchi nyingi za kwetu Afrika. Huku biashara ya mitumba, mtu akiamua siku yoyote (mara nyingi ni siku za mwisho wa wiki majira ya joto) kuuza vifaa vyake anatangaza kwa kutumia mabango kama siku mbili kabla. Katika mabango hayo yanayobandikwa barabara maarufu zipitazo madaladala anaonyesha kuwa anauza mitumba (yard sale) katika nyumba fulani na kuonyesha kwa mshale kwamba nyumba husika iko upande gani. Wengine wanaandika na namba ya simu kwamba kwa bahati mbaya ukipotea namba ya nyumba au mtaa, yupo mtu anajibu simu na kukuelekeza sehemu tarajiwa. Mitumba ya huku ni kila kitu, sio nguo na viatu tu kama tulivyozoea kuona.

Sasa leo Jumapili Aprili 5, 2009 nikaona matangazo ya aina hiyo sehemu tatu. Sehemu ya kwanza nilipoona ni Na. 2037 K Str. NW. Kwa kawaida minada hii huanzia saa tatu asubuhi na kuishia saa tisa mchana. Hivyo nikatoka mapema tu kuelekea huko nilikoona tangazo nikiwa ndani ya Basi la Metro(daladala). Nilipofika kwenye tangazo nikaona kumbe wameonyesha biashara inaanza saa tano asubuhi wakati mimi niliwahi saa nne na nusu asubuhi.

Nilipofika kwenye nyumba husika nikakuta mlango umefungwa. Nilielewa kwamba muda bado itanibidi nisubiri hadi hiyo saa tano asubuhi. Wakati huo huo udhaifu wa binadamu nikapatwa na dharura ya kutaka kwenda haja. Ndipo kisanga kiliponianza. Kwa kuwa hali ya hewa ilikuwa nzuri sana na jua lilikuwa likiwaka na baridi limepungua sana, watu wengi walikuwa wakifanya mazoezi ya mbio au kutembea, binafsi au na mbwa wao, na wengine wameketi tu barazani mwao wakifurahia hali hiyo. Nilipokuwa nikisubiri, ng'ambo ya barabara kukawa na mwenye nyumba mmoja ametoka nje anaota jua. Katika nyumba hiyo Na. 2030 Mtaa wa 37 NW (Kaskazini Magharibi) kulikuwa na bendera ya Marekani ya kiasi cha ukubwa wa mita moja ya mraba ikipepea.

Huku Marekani mtu yoyote kwa utashi wake anaweza kupeperusha bendera ya nchi yake yoyote nyumbani kwake. Sio kama sisi kwetu Tanzania bendera zinapepea ofisi za Serikali tu.

Kwa shida niliyokuwa nayo nikaikaribia nyumba ile na kumuomba radhi mwenye nyumba na kumueleza kwa nini nilikuwa pale na sababu ya kumuomba anisaidie niende msalani kwake nikajisaidie. Bwana yule aliyekuwa pandikizi la baba kiasi cha umri kama miaka 50 akanielekeza kwamba nipande ngazi zilizokuwa jirani kisha nitembee kushoto kiasi cha maili moja nitakutana na mgahawa wa "Starbucks" na huko ndio nikajisaidie. Kibinadamu nimemshukuru kwa kunielimisha njia pa kwenda japokuwa kibinadamu pia vilevile nilisononeka sana nafsi kuona wenzetu wa Marekani wameendelea kiasi cha kwamba mtu hayuko tayari kumkaribisha binadamu mwenzie asiyemfahamu kwa dharura kama ile.

Nikawa sina jinsi, nikafuata maelekezo aliyonipa mwenyeji yule. Nikapanda ngazi kuelekea huko chooni. Bahati nzuri kiasi cha mita 10 mbele yangu nikamuona mtu aliyekuwa na ngozi nyeusi kama yangu. Bwana huyu naye alikuwa kiasi na umri wa zaidi ya miaka 40. Nikamwomba radhi na kumkimbilia kana kwamba nilikuwa napelea baharini bila ya matumaini ya kuokolewa. Nikamtolea shida yangu bwana huyo na nikagundua moja kwa moja kwamba si mzaliwa wa Bara hili la Marekani. Baada ya kumfahamisha shida yangu bwana yule alifanya hima sana kurudi nyumbani kwake na kufungua mlango chapchap na hapo ndipo nilipoweza kumaliza shida yangu. Baada ya kumaliza shida yangu nikamshukuru kama mtu aliyeokoa maisha yangu kwa jinsi nilivyokuwa nimehamanika na dharura niliyokuwa nayo. Anaitwa Dr. KALAMOGO COULIBALY kutoka Ivory Coast. Bwana wa kwanza aliyenielekeza Starbucks alikuwa Mmarekani mweupe; hata hivyo nimeshawishika kuamini kwamba hata angekuwa Mmarekani mweusi kama mimi angenifanya hivyo hivyo kama alivyonifanya bwana huyu wa kwanza.

Katika kubadilishana kadi za kikazi (business cards), alinifahamisha kwamba aliwahi kufanya kazi na Dr. Ibrahim Lipumba katika Benki ya Dunia hapa Washington DC, na kwamba anakumbuka walivyoishi naye vizuri na akanipa salam nimpelekee mheshimiwa Mchumi huyu nitakaporudi Tanzania. Bwana huyu ambaye pia ni Mchumi, ameniambia kuwa Mkataba wake na Benki ya Dunia ulishamalizika na kwamba sasa anafanya kazi katika Ofisi ya Posta ya Marekani. Nikamwomba radhi sana kwamba nimemchalewesha kwenda kazini, akasema Jumapili huwa hafanyi kazi ila alikuwa anaelekea Benki kuchukua fedha ili ampelekee mama yake mzazi huko Ivory Coast. Nikamuombea sana baraka za Mwenyezi Mungu kwa yote; yaani kunihudumia mimi na kuniondolea tatizo langu pamoja na moyo wake wa huruma kwa kumkumbuka mama yake mzazi na kumpelekea fedha.

Sehemu za huku mijini hakuna vyoo rasmi vinavyojengwa na serikali za mitaa kwa ajili ya kuwasaidia wapita njia, isipokuwa vyoo vinavyotumika kama vya matumizi ya umma ni vile vilivyopo migahawani kama huko nilikoelekezwa "Starbucks" na migahawa mingineyo. Hivyo ndugu zangu mfikapo huku Marekani, msitegemee kupata huduma mkipatwa na dharura kama iliyonipata mimi. Kweli tembea uone. Kama kwetu Afrika, mgeni kama huyu anaelekezwa msalani na akitoka huko urafiki na udugu utapatikana kwa jinsi tulivyo wakarimu kwa wageni, na hasa mgeni atakayekuwa na fadhila baada ya kuwa amesaidiwa katika dharura kama hii lakini sio wenzetu wa huku. Ubinadamu huo hawana.

No comments:

Post a Comment