Friday, April 10, 2009

KIPIMO CHA SARATANI YA MATITI (MAMMOGRAM) MAREKANI

Leo nawafahamisha kuhusu kipimo tajwa kinavyofanywa huku kulikoendelea.

Nilifika kwenye kitua cha kutolea huduma hii kiitwacho Washington Radiology Associates, P.C. kilichpo Chase Tower, 4445 Willard Avenue, suite 200, Chevy Chase, Maryland 20815. Msishangae kwamba nimesema ni Washington DC. Kwa sababu DC imepatikana kutoka jimbo la Maryland katika historia yao. Kwa hiyo pamoja na kwamba kituo hiki kiko Maryland, kiko jirani (mpakani) kabisa na jimbo hilo ndio maana nasema hivyo.

Muda wangu wa kumuona mtaalam (Radiologist) mhusika ulipofika akaniita jina. Huyu ni Dr. Lee wa Washington Radiology Associates, P.C., Chase Tower, 4445 Willard Avenue, Suite 200, Chevy Chase, Maryland 20815. Nikamfuata alikokuwa akielekea. Akanifikisha katika chumba kidogo (cubicle) na kunifahamisha niondoe nguo zote za juu ya tumbo; yaani kifua kiwe wazi. Nikafanya hivyo na kuelekezwa nijivalie joho nililolikuta katika plastiki, kwa maelezo kwamba, baada ya kulitumia, nilitie katika kikapu ndani ya chumba hicho.

Akanichukua hadi chumba cha kipimo. Katika Upimaji matiti, mashine ya mammogram imesimamishwa hivyo hata kipima chake ni kupima ukiwa umesimama. Kuna vipimo vya aina tatu. Kwanza unapimwa sehemu nzima ya mbele ya kifua ikichanganya matiti yote mawili. Kisha unapimwa titi moja moja kwa ubavuni kwake. Kwa kuwa upimaji huu unagandamiza sehemu hizi nyeti za wanawake, kuna hisia za uchungu kiasi fulani. Kwa kuwa maumivu haya huchukua muda mfupi na kwa kuwa kile ni kipimo kwa ajili ya afya zetu, hayo yote yanakuwa si kitu. Ili mradi mtu upate tiba.

Baada ya kunipima akaniarifu kuwa nitarajie majibu toka kwa dakitari wangu aliyenipima Pap Smear Dr. Andrew Engel wa Foxhall OB/GYN Associates, P.C., 4910 Massachusetts Ave. NW. , Suite 112, Washington DC 20016-4368, Washington DC, USA. Kwamba yeye akishapata majibu ya kipimo changu, atakipeleka kwa Dakitari aliyenipeleka kwake. Kipimo hiki kinagharimu $300.

Huu haukuwa mwisho wa kipimo hiki. Wiki mbili baadaye nikaitwa tena kuhakikisha kipimo hicho hicho. Safari hii ya pili baada ya kupimwa, Dr. Ingrid Ott wa taasisi hii akajihakikishia zaidi kwa kuchukua maji yaliyomo ndani ya "cyst" kwa kuyafyonza na sindano. Maji hayo yalionyesha rangi ya njano kavu. Baada ya kuyachunguza akaniambia niko salama. Hata hivyo kwa watu wa umri wangu wa miaka 55 akasema inabidi niache kutumia vyakula vitokanavyo na wanyama (dairy products) kama vile maziwa, jibini, mtindi, na nyama yenyewe; vyakula ambavyo kwa asili yetu Walugulu wa Morogoro huwa ni nadra sana kuvihudhurisha katika milo ya kila siku.

Kisha nikapewa picha zote nilizopigwa siku ile (x-ray, ultra-sound) na kushauriwa kuwa niwe natembea nazo ili nikienda kwenye kipimo kama hicho mwakani, dakitari aweze kuzisoma na kuangalia kama kuna tofauti yeyote itakayojitokeza. Yaani nimrahisishie kazi endapo kutajitokeza tofauti ya hali iliyopo sasa.

No comments:

Post a Comment