Monday, April 27, 2009

VITA YA WENYEWE KWA WENYEWE ILIYOUNGANISHA SHIRIKISHO LA NCHI YA MAREKANI

Aprili 18, 2009 kikundi chetu cha Wanafunzi watokao Mataifa Yanayoendelea (Humphrey Fellows) tunaofadhiliwa na serikali ya Marekani (USA) tulitembelea uwanja wa mapambano ya Vita ya Wenyewe kwa Wenyewe wa Gettysburg, uliopo jimboni Pennsylvania. Katika uwanja huo ndipo ilipopiganwa vita kali kuliko zote katika miaka minne (4) ya Vita ya Wenyewe kwa Wenyewe ya Wamarekani kati ya mwaka 1861 hadi 1864.

Wamarekani wa Majimbo ya Kusini na wale wa Majimbo ya Kaskazini wakati huo walipigana Vita hivyo kwa sababu kuu ya kuachana na Utumwa. Wale wa Majimbo ya Kusini waliokuwa wakitegemea sana uchumi wao kwenye Kilimo kilichokuwa kikichangiwa nguvu kazi yake kuu na watumwa (Waafrika), na wale wa Kaskazini waliotaka kutokomeza Utumwa ili Watumwa hao watumike viwandani katika kuzalisha bidhaa mbalimbali. Hiyo ilikuwa ni sababu kuu mojawapo. Kama zilikuwapo nyingine msomaji wa habari hii utazikuta vitabuni kwani Wamarekani ni Mahiri sana katika kuandika Historia yao kinaga ubaga.

Tulipofika katika eneno la mapambano, kwanza tulipewa somo la kufahamu wakati huo vita ilipiganwa kwa kutumia silaha gani. Kila askari alitakiwa afungashe nini akienda vitani na medani ya vita yenyewe ilipiganwaje. Tukaambiwa hiyo bunduki ya uzani wa pauni 12 iliyotumika wakati huo ilikuwa ikitoa risasi moja moja tu. Kwa hiyo kila askari akilenga na kufyatua risasi moja, ilimbidi aingize risasi nyingine ili alenge adui mwingine. Kwa hiyo umahiri wa kutumia silaha hii ulitokana na mambo mawili. Kwanza ni uwezo wa kuingiza risasi haraka sana na uwezo wa kulenga shabaha kwa askari mwenyewe. Wakati huo magwiji wa kulenga shabaha "snipers" ndio waliokuwa wakiheshimiwa sana kwa sababu uwezo wao huo ndio uliokuwa tija kwa jeshi lolote. Pia katika upiganaji wao, Makamanda walikuwa wakipanda farasi katika uwanja wa vita, wakati askari wapiganaji walikuwa wakitembea kwa miguu.

Tulionyeshwa chakula waliokuwa wakisafiri nacho askari hao (aina ya mkate mgumu), risasi, bunduki, vifaa vya kulia chakula, kikombe cha maji, chombo cha kuchukulia maji/pombe, kinanda cha kuliza usiku, kifuko kilichokuwa na sindano na uzi wa kushonea jamanda la kijeshi likichanika vitani, na kadhalika.

Katika vita hivyo vya Gettysburg vilivyopiganwa kwa muda wa siku mbili, askari zaidi ya 51,000 waliathirika (casualties). Kuathirika huku ni pamoja na waliokufa, walioumia na waliopotea na kutojulikana walikokwenda, baada ya kuhesabiwa. Vita hivi vilipiganwa askari wakiangaliana kutoka mita kati ya mia tano na mia moja toka mstari wa adui hadi wa adui wa upande wa pili. Askari waliotoka majimbo ya Kusini waliitwa "Confederates" na wale waliotoka majimbo ya kaskazini waliitwa "Union". Kwa ujumla wake vita hii ilianza huo mwaka 1861 Confederates walikuwa na jeshi la askari zaidi ya 90,000 wakati wenzao wa kaskazini walikuwa na askari walizidi kidogo 60,000. Silaha za bunduki wakati huo zilikuwa zikitengenezwa katika viwanda jimboni Connecticut, ambalo ni jimbo la kaskazini. Hivyo wenzao wa Kusini walikuwa wakitegemea zaidi kuagiza silaha kutoka nchi za nje hasa Uingereza na Canada.

Kwa ujumla wake, wanahistoria wa Eneo hili la Gettysburg (Gettysburg National Military Park) wanasema Majeshi ya Kusini yalikuwa yanashinda vita hivyo na yalikuwa yanaelekea kwenye kupata ushindi wa jumla katika vita. Mapambano yaliyofanyika katika eneo hili ndio yalibadilisha matokeo ya vita hivyo kwa kuwa majeshi ya majimbo ya Kaskazini yalishinda chini ya Amiri Jeshi wao Mkuu, Rais Abraham Lincoln, rais wa 16 wa nchi hiyo aliyeingia madarakani mwaka 1860. Rais huyu anaheshimiwa sana katika historia ya nchi hii kwani ndiye aliyehakikisha kwamba Marekani haijitengi kuwa nchi mbili tofauti ya kusini na kaskazini bali inabaki kuwa nchi moja iliyotokomeza Utumwa chini ya utawala wake.

Katika mji huu mdogo wa Gettysburg, Wamarekani wameamua kuubakisha mji wao kama ulivyokuwa wakati wa Vita ya 1863. Sio katika maeneo yote, lakini sehemu kubwa ya majengo ya mji huu, mandhari yake, mavazi yake, vyakula vyake, na historia yake imehifadhiwa katika sehemu kubwa ya mji huu. Nilitembelea katika nyumba moja iliyoonyesha mashimo ya risasi iliyovurumishiwa wakati huo; mashimo yaliyozidi 100 na nyumba hiyo ilisimama imara (ya tofali la kuchoma).

Dada mmoja mchoraji mahiri aitwaye Bi. Amy V. Linenberger; ambaye ana ofisi yake hapo Gettysburg na anafanya maonyesho ya picha alizochora tulipomtembelea; alinionyesha baadhi ya michoro ya picha za askari wa wakati huo walivyokuwa wakionekana na majamanda yao ya kijeshi. Kuna hadithi inasimuliwa kwamba usiku kuna Msukule wa askari anakimbia mitaani akiwa ameshika mkono wake uliokatwa na unavuja damu( huku wanaita "ghosts" na kwetu tunaita Misukule). Dada huyu alinithibitishia kwamba hakutokei MSHINDI katika vita yoyote ile duniani, nami nilikubaliana naye.

Nikakumbuka vita yetu ya Kagera mwaka 1978 tuliyopigana tokana na uchokozi wa Nduli Iddi Amin Dada wa Uganda kuvamia Mkoa wa Kagera, nchini Tanzania, na nikaamini kweli hakuna MSHINDI vitani kwa sababu Tanzania ya leo hii mwaka 2009, bado inalipa madeni ya vita ile iliyochukua kama miezi miwili tu. Seuze hii ya miaka minne!. Hakuna Mshindi vitani.

Taarifa tunazopewa na vyombo vya habari kwamba eti Mmarekani au Tanzania imeshinda vita ni Siasa Tupu. Hakuna mshindi vitani kwa sababu gharama yake inakuwa ni kubwa sana na wala sizungumzii fedha. Gharama ya kupoteza binadamu vijana walio katika upeo wa maisha yao, wanaoumia na wanaopata Mifadhaiko, wanaoachwa wajane, vilema, mayatima, na mengine mengi ambayo hayahesabiki kifedha. Ni gharama kubwa mno kwa upande wowote ule wa pande mbili zinazopigana.

Katika matembezi yetu katika Hifadhi hiyo ya Majeshi ya Gettysburg, tulikutana na Mchungaji mmoja aliyetupatia picha ya watoto watatu iliyokutwa katika mmoja wa askari waliouwawa vitani hapo. Yaelekea askari huyo alikufa akiwa anaiangalia picha hiyo ya watoto wake waliokuwa kati ya miaka 3 na 6 hivi. Picha hiyo ilichukuliwa na kupelekwa katika vyombo vya habari wakati huo. Vyombo hivyo vikaitangaza picha hiyo magazetini na mama ya watoto alipatikana akiwa New York. Mama huyo alikuwa ameachana na mume yule askari. Baada ya kutangazwa aliwafuata watoto wake hao huko Gettysburg. Wasamaria wema na vyombo vya habari ndio vilisaidia kutangaza (hatima ya watoto hao) na michango yao ndio iliyosaidia kuanzisha Nyumba ya Kwanza ya Watoto Yatima mjini Gettysburg baada ya kumalizika vita hivyo.

Vita hii ilipiganwa kwa siku tatu mwezi Agosti, 1863. Kuanzia 1 - 3 Agosti, 1863. Siku tatu na kuacha Waathirika zaidi ya 51,000 ambao walikuwa wengi zaidi kuliko waathirika wa Vita vyote vya Vietnam waliopigana Wamarekani pia, vita iliyopiganwa miaka ya 1970; wakati ambao askari wa Marekani walikuwa na silaha kali zaidi, zilizouwa watu wengi zaidi kwa mara moja na silaha za kemikali za sumu. Silaha kama vile mabomu ya nyuklia, "Agent Orange", na "Machine Gun" zilizoweza kumwaga risasi kama upupu. Naomba tuelewane hapa. Hii idadi ya zaidi ya elfu hamsini ni ya askari wa Marekani TU waliouwawa. Sio idadi ya mamilioni ya Wananchi wa Vietnam walioangamia katika vita hii.

Endapo Majimbo ya kusini ya Marekani yangeshinda vita hivi, maana yake ni kwamba Marekani leo hii ingeendelea kuwa na Utumwa, na nchi hii ingekuwa ni nchi mbili tofauti sio nchi moja kama ilivyo sasa. Rais Lincoln ananukuliwa katika hotuba yake Maarufu sana ya kuunganisha nchi, aliyoitoa Novemba 19, 1863 wakati wa lala salama ya vita hivyo; kwani baada ya kushinda Gettysburg, majeshi ya Kusini yakaishiwa nguvu kwa sababu ya uchumi uliokuwa ukididimia, kukosa silaha (kwa sababu watengenezaji wa nchi za nje walikataa kuendelea kuwauzia Kusini kwa sababu ya kuendeleza siasa za kukataa kutokomeza Utumwa) na kuzidiwa na bunduki kali zaidi zilizotoka Connecticut.

Ifuatayo ndio hotuba aliyoitoa Rais huyu Maarufu sana siku hiyo katika uwanja huu wa kivita wa Gettysburg:

"Forescore and seven years ago our fathers brought forth on this continent a new nation, conceived in liberty and dedicated to the proposition that all men are created equal.

Now we are engaged in a great civil war, testing whether that nation or any ntion so conceived and so dedicated can long endure. We are met on a great battlefield of that war. We have come to dedicate a portion of it as a final resting place for those who died here that the nation might live. This we may, in all propriety do. But in a larger sense, we cannot dedicate, we cannot consecrate, we cannot hallow this ground. The brave men, living and dead who struggled here have hallowed if far above our poor power to add or detract. The world will little note nor long remember what we say here, bu it can never forget what they did here.

It is rather for us the living, we here be dedicated to the great task remaining before us -- that from thesed honored dead we take increased devotion to that cause for which they here gave the last full measure of devotion- that we here highly resolve that these dead shall not have died in vain, that this nation shall have a new birth of fredom, and that government of the people, by he people, for the people shall not perish from the earth. "

No comments:

Post a Comment