Imechanginwa na kaka Dan Nkurlu wa Dallas, Texas.
Kibwagizo Kipya...Mtikisiko na kuanguka kwa uchumi wa Dunia
Wimbo wetu ulio bora, ule ule wenye viitikio vingi visivyoleta maana wala mwelekeo umepata kibwagizo kipya “mtikisiko wa Uchumi wa Dunia na kuanguka kwa uchumi wa nchi Tajiri’! Naam, wanasiasa na watendaji wa Tanzania wamepata kibwagizo kipya kuwaimbisha Watanzania wimbo wa uvumilivu wa umasikini wao kwa kudai kuwa hali yetu inaendelea kuwa ngumu kutokana na kutikisika kwa uchumi wa dunia na kuanguka kwa mfumo wa fedha na mabenki katika nchi tajiri.Hebu tafakari, tangu tulipopata Uhuru wetu, tumekuwa tukipata kibwagizo kipya kila siku kuhalalishiwa umasikini na uduni wetu kila siku kutoka kwa watu tuliowapa dhamana ya kutuongoza.Tulianza na ukabaila, tukaja na ukoloni, tukaupandisha madaraja kadhaa, kama vile ukoloni mamboleo, ubwanyenye, ubepari, ikaja hekaya ya uchanga wetu, ukosefu wa wataalamu wa kutosha, ikaja unyonyaji tulioufuta kwa kutumia Azimio la Arusha, kukawa na maasi ya jeshi, uasi wa kina Kambona, kifo cha Karume, vijiji vya ujamaa, maduka ya ushirika, bei za mafuta 1974, ukame, vita vya Kagera, Makaburu, Walowezi, Manyang’au wa Kenya na kuanguka kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ulanguzi, uhujumu uchumi, uhaini, mpasuko wa chama, ruksa, kutokwajibika, Benki ya Dunia, Vyama vingi, uwekezaji, kodi, mikataba ya madini, utalii, umeme wa shida, bei za mafuta, ufisadi, VAT, mvua, ukame, ubinafsishaji na sasa tunalaumu kuanguka kwa uchumi wa dunia!Hivi, katika sababu zote hizi, ni lini tuliweza kuamka, kujipangusa vumbi na kuanza kupiga hatua kwa kujifunza kujikinga na dhoruba kwa yaliyotukumba na kujijenga kwa uimara na kinga kama ule wimbo maarufu wa mipira ya kiume wa “Salama, chaguo la Kisasa, Salama kinga njema”? Ni lini tulijipima nguvu zetu kwa dhati na kutumia bidii zetu zote, zikiandamana na maarifa na ufanisi na fikra bora kujiimarisha kutoka umasikini na unyonge?Yaani ina maana katika miaka karibu 50 tangu tujitawale, bado hatujaweza kuvumbua njia bora ya kujiimarisha kiuchumi bila kulaumu wengine kwa udhaifu na umasikini wetu?Majuzi, mamlaka ya ukusanyaji kodi na mapato ya Taifa maarufu kama TRA, imetamka kuwa ilitarajia kukusanya mapato ya Takriban Shilingi Trilioni 2.62 katika kipindi cha miezi 6 iliyopita, lakini imeweza kukusanya Shilingi Trilioni 2.45 na kupungukiwa mapato ya Shilingi Bilioni 200.00. TRA imesema kuwa kupungukiwa kwao kukusanya mapato haya, kumetokana na mtikisiko na kuanguka kwa Uchumi wa Dunia! Nimepiga mahesabu ya haraka haraka na kubaini kuwa TRA wamekusanya takriban asilimia 94 (94%) ya makisio au makadirio ya mahesabu yao, nikajiuliza, je kupungukiwa kwa asilimia 6 (6%) ni kweli kumetokana na kusuasua kwa uchumi wa dunia? na jee mtikisiko huu utatuumiza kiasi gani kwa kupungukiwa asilimia 6 ya mapato mpaka tuanze kusema hatuna pesa za kununulia madawa?Nikakumbuka Serikali ilisitisha kununua magari mapya, na hili limeokoa fedha nyingi tuu, hivyo basi pengo la 6% litajiziba! Zaidi, ni kuwa Mwezi Januari ya mwaka huu 2009, mapato yaliyokusanywa na TRA yalikuwa ni asilimia 23 (23%) zaidi ya mapato yaliyokusanywa mwezi januari ya mwaka 2008! Sasa kama uchumi wa dunia ambao tunajua ulianza kuyumba mwezi wa Septemba 2008, ulikuwa ni mbaya iweje mapato ya mwezi Januari 2009 yawe makubwa marudufu kuliko mapato ya Januari 2008?Je Serikali yetu imewahi hata mara moja kubana na kupunguza matumizi yake ambayo mara nyingi si kwa manufaa ya Taifa? Ikiwa ripoti za Utoh, mdhibiti mkuu wa mahesabu wa Serikali zinaonyesha matumizi mabaya na kukosekana kwa uhakiki na uadilifu katika kuthibitisha matumizi au kuweka kumbukumbu za matumizi kwa mujibu wa kanuni za mahesabu na kihasibu, ni vipi leo tulaumu kuyumba kwa uchumi wa Dunia kama mapato yetu yamepungua lakini hatjali jinsi tunavyoyatumia kwa kuwa tumejijengea umaarufu wa kufuja, tunakodai "Pondamali, kufa kwaja"?Nikakumbuka kauli za Rais Kikwete mwaka huu 2009, katika kipindi cha miezi miwili iliyopita ambapo aliashiria kuwa kushindwa kwa Tanzania kujinasua kiuchumi, kunatokana na hali mbaya ya uchumi duniani. Kwanza alitangaza kuomba stimuli kutoka kwa nchi tajiri, akisema ni lazima na sisi tupewe mgawo wa fedha kusisimua na kufufua uchumi wetu, baadaye akalaumu bei ya mafuta kuwa ghali sana na hivyo kutuangamiza kiuchumi.Bei ya mafuta Duniani, imeshuka tangu Julai 31 2008 ambapo pipa moja lilikuwa likiuzwa kwa Dola za Kimarekani 145, mpaka bei ya leo hii April 6 2009 ambapo pipa ni Dola za Kimarekani 52, hii ikiwa ni punguzo la asilimia 65 (65%) katika kipindi cha miezi 10! Sasa najiuliza, kama kwa miezi 10 bei ilishuka mpaka ikafika dola 33 Disemba 30 2008, iweje tuendelee kulaumu bei za mafuta kuwa ghali? Je kama bei ya mguu wa ng’ombe imeshuka, kiasi kuweza kununua miguu mitatu badala ya mmoja kwa gharama hiyo hiyo, hivi tutaendelea kulia kuwa hatuna uwezo wa kujipatia Protini za kutosha?Kila kiongozi na mtendaji wa Tanzania anakimbilia kuimba kibwagizo kipya, “uchumi wa dunia”, najiuliza ni lini tutajiangalia ndani na kubaini kuwa hatujaathirika sana na tunaweza kupona? Nitaelewa kuwa tunaumia kama mfumo wetu huu mpya wa uchumi wa soko huria na uwekezaji ungekuwa umeshafikia hatua kuwa wawekezaji wote wameulaza na kutuachia majengo na mashimo matupo huku wao wakiwa wamekimbia na hela. Lakini hilo si kweli kwa kuwa tumeambiwa majuzi kuwa yale makampuni ya uchimbaji dhahabu, yalijikusanyia mapato ya Dola Bilioni 3 na Seikali yetu ikaambulia mapato ya Dola milioni 1 ikiwa ni asilimia 3 (3%) tuu! Baya zaidi kwa hawa waimbishaji wa kibwagizo kipya wanaendela kutafuta mbinu za kuwapa wawekezaji ahueni na kutupunguzia mapato. Ole Naiko katangaza wiki mbili zilizopita kuwa TRA na TIC wanaunda kamati ya kuwapa Wawekezaji mfumo bora na wa unafuu wa kodi! Astaghafulahi, leo tunalia tuna mapato duni, bado tunafikiria kupunguza mapato kwa kutoa misamaha ya kodi?Ni lini tutajifunza kutokana na makosa tuliyoyafanya hapo kale? Ni lini Watanzania na hasa Viongozi wetu na Watendaji watabadilisha mitazamo yao na ufikiri wao na kuanza kukubali kuwa jawabu pekee la Tanzania kuendelea si visingizio bali ni kuongeza uzalishaji mali wa ndani ambao utatokana na jasho letu na juhudi zetu na si kutegemea misaada au kulalama kuwa kuungua kwa mwingine, kumeangamiza nyanya zetu zilizo kilometa 100 mbali na kwetu na tunachokiona ni moshi angani?Sina maana ya kukataa kuwa Uchumi haujayumba Duniani, lakini si kweli kuwa Tanzania inashindwa kupiga hatua mbele kwa kuwa Mabenki ya Marekani yanafilisika. Serikali yetu badala ya kuweka kipaumbele kujenga mfumo mzuri na bora wa uzalishaji mali , kama vile Rwanda walivyoamka, imeendelea kupitisha bakuli kuombaomba kila kona. Mizengo Pinda akiwa Ireland akitembelea wafugaji na wakulima, aliomba misaada na kukaribisha wawekezaji. Je ni lini ametoa ruzuku ya maana kwa yule mkulima kule Simanjiro ili ajinunulie pembejeo au alipwe bei bora ya mazao yake? Viongozi wetu wamebakia kuwa mapambo, watalii na omba omba, kutwa kucha kupiga domo bila kufanya kazi wala kutoka jasho kuona kuwa kuna ulazima wa kubadilika vitendo na tabia kama tunataka Taifa letu lipate maendeleo ya kweli.Benki Kuu majuzi imetoa takwimu kuwa kilimo kinaingizia Taifa letu asilimia 26 (26%) ya mapato yake kutokana na mauzo ya mazao yetu. Asilimia 80 (80%) ya Watanzania wanaishi vijijini, wakijilimia kijima na zile zama za kale za mawe! Kwa nini basi kama Watanzania Milioni 30 wanaishi vijijini na takriban nusu yao wana uwezo wa kuzalisha mali, kwa nini tunaendelea kuagiza vyakula kutoka nje ya nchi na si kuzalisha kwa ziada na kuuza nje ya nchi ili tusikumbwe na mtikisiko wa Dunia?Marekani, Uingereza, Uchina, Ujapan na nchi zote tajiri, bado zinahitaji chakula, migahawa yao bado inauza Kahawa na Chai, inahitaji maharage, nyanya, bamia, vitunguu, viwanda vyao vya nguo vinahitaji pamba, nyumba na maofisi na watu wao wanapenda maua na matunda. Hata Kenya , Congo na Zambia , wanahitaji Chakula! Oman wanakodisha ardhi Kenya walime chakula, sasa iweje tusema hatuwezi kujikwamua kiuchumi kisa Mabenki ya Marekani yamefilisika kutokana na uzembe na ukosefu wa maadili, gonjwa ambalo ni kubwa nchini mwetu?Nilichojifunza kutokana na kuanguka kwa Uchumi wa Dunia safari hii, ni kuwa kama nchi yangu ni mzalishaji imara na fanisi, haiwezi kutikiswa kutokana na njaa ya jirani! Nimejifunza kuwa Watendaji wengi wetu, ama ni Wasomi Wajinga au ni Mapunguani fuata Upepo wasio na uwezo wa kukaa chini na kufikiria kwa kina njia rahisi na madhubuti za kuongeza uzalishaji huku ukipunguza matumizi yasiyo na maana!Leo hii Singapore , Spain na Ireland ambazo zilijenga uchumi wao kutokana na uwekezaji wa Soko huria, wamekuwa ni wa kwanza kupiga yowe la kichaga lile la “yewomi, yeleuwi”, uchumi wao ukiteketea kutokana na wawekezaji kukimbia na kwenda kwenye soko la bei nafuu kuzalisha!Sisi tumeambiwa,tujifunge mkanda, tujikaze kiume, tuvumilie, tuhimili makali ya umasikini yanayoongezeka kutokana na kuyumba, kutikisika na kuanguka kwa uchumi wa dunia!Uuwi, Yewomi, yeleuwi, wimbo ni ule ule, tumepata Kibwagizo kipya, tuvumilie machungu na tunogewe na umasikini wetu kwa kuwa Uchumi wa Dunia Umeyumba na Kutikisika!
Thank you and have a wonderful day.Dan A. NkurluOperations Manager, Dallas Cash VaultWells Fargo Bank-CSSO1201 Main Street , Mac T5323-011Dallas , TX 75202Office: 214-761-0333Fax: 214-761-0326Cell: 612-708-1529Dan.Nkurlu@Wellsfargo.Com
No comments:
Post a Comment