Thursday, April 16, 2009

KODI WALIPAZO OBAMA NA BIDEN MAREKANI

Mambo ya ukweli na uwazi kama haya yaliyoanikwa na gazeti tajwa hapa chini ndio yanayowafanya wenzetu, angalau kuwa na imani na viongozi wao kwamba hawaliibii taifa. Tofauti na nchi zetu, hata sheria ikiwepo ya kutangaza mali kiongozi aingiapo madarakani, ETI kuna kipengele kinachosema hawezi kuwajibishwa kutangaza mali alizonazo atokapo madarakani. Ni ulaghai mtupu. Kwa mtindo huo, ni kiongozi gani katika nchi zetu za Afrika ambaye atachukuliwa kuwa ameingia na kutoka madarakani akiwa na uchungu na wananchi wake na nchi yake na kwamba hakukomba mali za taifa? Hakuna kigezo cha kupima uadilifu wa namna hii.

Habari hii nimeitoa katika gazeti la "The Examiner" la Washington DC la leo Alhamisi, Aprili 16, 2009. Jana kulikuwa na maandamano katika majimbo mengi tu katika nchi ya Marekani pamoja na Mji Mkuu wa Serikali haya Washington DC. Kwa hiyo leo kuna habari nyingi za maandamano yaliyofanywa jana ya kupinga ukatwaji wa kodi katika Bajeti ijayo, ukatwaji ulioidhinishwa na Serikali ya Rais Barack Obama. Katika kufafanua jambo hili, gazeti hili limechapisha pia mapato ya Obama kwa mwaka uliopita na kodi zake alizolipa yeye na zile za Makamu wake wa Rais Bw. Joe Biden.

Nchini Marekani, Aprili 15 ya kila mwaka ndio siku ya mwisho ya kujaza fomu za makato ya kodi za mwaka uliopita (2008/2009) wa kila rais mwenye kipato ambacho sio cha Chini kama inavyochukuliwa katika nchi hii. Kipato cha chini kama wastani ni $30,000 kwa mwaka. Kwa hiyo wapatao zaidi ya kiasi hicho wanawajibika kisheria kujaza fomu hizo ili wakatwe kodi.

Marekani kwa sasa ina deni la Dola trilioni 11 ($11.00 trillion). Kulingana na idadi yake ya watu katika nchi hii, kila mtu anadaiwa $184,000 gazeti hilo linasema.

Gazeti limesema kwamba Familia ya Obama ina kipato cha mwaka jana cha $2.7 milioni (Dola milioni mbili na laki saba) iliyopata zaidi kutokana na mauzo ya vitabu vya Obama ambavyo vinauzika sana tangu ameukwaa urais. Katika mapato hayo, Obama amelipa kodi zinazofikia $885,323.

Katika idadi hiyo, kodi ya kulipia deni la riba ya nyumba ni $50,000, na $172,050 wametoa sadaka (charity). Sadaka hizo ni pamoja na $25,000 walizotoa kwa NGO iitwayo CARE International na $25,000 walizotoa kwa The United Negro College Fund.

Kwa Upande wa Bw. Biden, yeye na mkewe mapato yao mwaka uliopita yalifikia $269,256 zilizotokana na mishahara kutoka Bunge la Senate, Widener University Delaware Tecnical & Community College pamoja na Mirahaba (royalties) toka katika Hakimiliki ya Kumbukumbu za Makamu wa Rais (audio).

Wao wamelipa kodi kiasi cha $46,952 kutokana na mapato yao ya Serikali Kuu, $11,164 ni kodi iliyolipwa katika jimbo la Delaware na $1,885 wametoa sadaka mbalimbali.

No comments:

Post a Comment