Tarehe 9 Aprili, 2009 niliwahi kupata fursa ya kutembelea makumbusho Kadhaa hapa Washington DC, ambayo kwa bahati nzuri yote ni bure. Gharama yako ni usafiri kwenda na kurudi.
Nikaamua kutembelea makumbusho ya National Museum of African Art, yaliyopo 950 Independence Ave. SW, Washington DC. Nilipofika tu mlangoni baada ya kusachiwa, kitu cha kwanza nilichokiona kulia kwangu ukutani ni KANGA NZITO YA NIDA DSM!
Hapo nikasema ama kweli na sisi tunakumbukwa huku Marekani. Nilipouliza Mapokezi nikaambiwa kuwa kanga hiyo ilitengenezwa mahsusi kwa ajili ya Siku ya Kuapishwa kwa Rais Barack Hussein Obama, na kwamba hakuna doti za biashara dukani kwao. Na kweli ilikuwa na picha ya Obama katikati na maandishi yake yalisema hivi: 'UPENDO NA AMANI AMETUJALIA MUNGU'. Kisha katika kibao cha maelezo wakatafsiri usemi huo katika kiingereza "God has blessed us with Love and Peace". Kwa kweli nilifurahi sana kuona alama ya utamaduni wa Mtanzania katika Makumbusho haya. Kwa bahati mbaya sehemu muhimu sana ya Makumbusho haya inafanyiwa Ukarabati Mkubwa kwa sasa kiasi kwamba sikuweza kuzunguuka zaidi ili nione vilivyomo humo kwa sababu kwenye ukarabati ni sehemu iliyokatazwa kuingia.
Hata hivyo pia niliwahi kutembelea THE SMITHSONIAN CASTLE ambayo ndio makao makuu ya Makumbusho yote nchini Marekani yaitwayo "Smithsonian". Makumbusho yote yenye jina hili ni bure kwa sababu ni Urithi wa Marekeni kutoka kwa Bwana wa Kiingereza mwenye jina hili "Smithson". Bwana huyu aliishi katika karne ya 19 nchini Uingereza. Bwana huyu hajawahi kufika Marekani. Yeye alikuwa ni Muingereza. Bara la Amerika alilisikia tu kutoka kwa wenzie na habari mbalimbali vitabuni. Aliamua kurithisha mali zake zote baada ya kufa kwake kwa Wamarekani baada ya kukataliwa kuwamo katika kundi la Wateule (Royalty) wa Uingereza kwa sababu yeye alikuwa kilokote (mtoto wa nje ya ndoa). Kwa sababu hii, hakuwa na haki ya kurithi utajiri mkubwa wa baba yake. Alifanya jitihada sana katika maisha katika taaluma ya tafiti mambo mbalimbali baada ya kufanikiwa kulimbikiza mali nyingi tu.
Hivyo alipofariki 1829, Waosia wake uliposomwa juu ya kurithishwa huku, ndio sababu Bunge la Marekani likatunga sheria kufanya mali yake ni kwa ajili ya Makumbusho ya Watu Wote kwa kutotoza gharama yoyote katika Makumbusho hayo. Hadi sasa, yapo majumba ya Makumbusho 17 yaliyo chini ya Asasi hii ya Smithsonian jijini Wasington DC, USA. Sehemu kubwa ya Makumbusho haya yapo mtaa huu wa "Uhuru.", unaotazama uwanja maarufu wa kitaifa nchini Marekani "The Mall" . Hii "Mall" ni kiasi cha kilometa tatu za urefu, na upana unaofanana na upana wa Uwanja wa Mnazi Mmoja Dar es Salaam. Uwanja huu ndio ulijaa umati wa watu siku alipoapishwa Rais Barack Obama Jauari 20, 2009 na kuvunja rekodi ya kujaza uwanja (crowd-puller) kwa Marais wote walipita wa Marekani.
Makumbusho mengine yaliyojaa elimu kedekede ni yale ya National Museum of Natural History. Humu mna historia ya Sayari yetu dunia tangu viumbe hai vilipoanza hadi tulipo sisi binadamu na hadi tunavyojimaliza, pamoja na kupungua kwa nguvu ya jua na kuiacha dunia tupu miaka milioni nne na nusu ijayo. Kunaonyeshwa pia viumbe hai walivyoanzia baharini, waliopukutika/waliopotea (extinct) na waliopo sasa. Pia kuna bustani ya Darwin ya maua ya Orchids. Bustani hii ni hai na inatunzwa kila siku. Humo katika bustani kunanukia vizuri sana mauwa haya, ambayo yako katika aina mbalimbali na rangi mbalimbali.
Jumla ya Makumbusho ya Smithsonian, kama yalivyoorodheshwa katika kitabu cha Washington DC Official Guide Winter/Spring, 2009 kinachotolewa na Washington DC Convention and Tourism Corporation ni kama ifuatavyo:
1. Anacostia Community Museum. Hii Makumbusho imo ndani ya nyumba iliyokuwa ya Mheshimiwa Frederick Douglas, Mmarekani Mweusi wa karne ya 19 aliyeukataa Udhalilishwaji wa Watu weusi nchini Marekani. Yeye alimtumia rafiki yake Mmarekani mweupe kumnunulia nyumba hii kwa kuwa wakati huo Mtu Mweusi Marekani hakuruhusiwa kununua nyumba. Rafiki yake Mweupe akamnunulia nyumba hiyo kisha kumkabidhi na hati zake.
2. Freer Gallery of Art and Arthur M. Sackler Gallery
3. Hirshhorn Museum & sculpture Garden (humu mna masanamu yakiwa kichele)
4. National Air and Space Museum
5. National Air and Space Museum Steven F. Udvar-Hazy Center
6. National Museum of African Art (humu mna Kanga ya Tanzania)
7. National Museum of American History
8. National Museum of Natural History
9. National Museum of The American Indian (mna mkataba wa Geronnimo)
10. National Portrait Gallery (humu iko picha ya Angelina Jolie)
11. National Postal Museum
12. National Zoological Park (humu mna Panda wa China)
13. Fenwick Gallery of the Smithsonian American Art Museum
14. Smithsonian American Art Museum
15. Arts & Industries Building
16. Smithsonian Associates
17. Smithsonian Institution Information Center.
No comments:
Post a Comment