Friday, 16 July 2010 08:31
0diggsdigg
Fidelis Butahe na Aziza Masoud
MTOTO wa Profesa jwan Mwaikusa ambaye aliuawa kwa kupigwa risasi akiwa nje ya nyumba yake, amesema hahusishi mauaji hayo na ujambazi kwa kuwa waliotoa maisha ya baba yake hawakupora chochote.
Profesa Mwaikusa, ambaye atazikwa kesho nyumbani kwake Tegeta Salasala, aliuawa usiku mara baada ya kurejea nyumbani kwake wakati watu wasiojulikana walipomvamia kwenye gari na kumtaka ashuke na baadaye kumfyatulia risasi mbili.
Kabla ya kumuua mwanazuoni huyo, watu hao walimuua mpwa wake, Gwamaka mMwakilasa kwa kumpiga risasi mbili mgongoni na baada ya kumuua Prof Mwaikusa walikwenda nyumba jirani na kumuua mfanyabiashara, John Mtuikifuani na kutoweka.
Baada ya kumfyatulia risasi, watu hao wameripotiwa kuwa walimburuzia profesa huyo nje ya gari na kumkanyaga kwa miguu wakati wakimsogeza ili wapekue vitu ambavyo walikuwa wakivitaka.
Akizungumzia mauaji hayo ya baba yake, Baraka alisema ni vigumu kuhusisha mauaji hayo na wizi wa kawaida au ujambazi kwa kuwa majambazi wangeweza kuchukua gari na vitu vingine vilivyokuwa ndani ya gari la marehemu.
"Sioni kama tukio hili ni wizi au ujambazi kwa sababu hawajaiba kitu chochote ingawa walikuwa na uwezo wa kuiba kila kitu walichokitaka. Gari halikuwa na tatizo lolote.
"Kama wangekuwa majambazi, wasingekuja kwa miguu, lazima wangekuwa na usafiri wa kueleweka na lazima kungekuwa na wenzao nje, lakini wao walikuwa wawili tu tena ni vijana ambao wanaweza kuwa na umri kama wangu," alieleza Baraka.
Kwa mujibu wa Baraka baadhi ya watu waliofika kwenye msiba huo walieleza kuwa eneo hilo limekithiri vitendo vya kupora na watu kadhaa wamekuwa wakivamiwa na kuporwa vitu mbalimbali.
Kwa masikitiko, Baraka alisema Profesa Mwaikusa hakustahili kukatishwa maisha yake kikatili kiasi hicho na kusisitiza kuwa huo hauwezi kuwa ujambazi tu.
"Nilimuona mmoja wa majambazi na kwa sura nitamfahamu. Alikuwa mwembamba na kichwani alikuwa na nywele nyingi. Baba ameuawa kama jambazi, kifo hiki kimenisikitisha sana kwa kweli siwezi kusahau maishani," alisema kwa uchungu.
Baraka pia alisema kuwa mwanazuoni huyo, ambaye pia alikuwa wakili, atazikwa kesho nyumbani kwake Tegeta Salasala jijini Dar es Salaam na kwamba ratiba ya mazishi itatolewa leo baada ya vikao vya wanandugu.
Alisema kuwa familia ya marehemu imeamua kumzika Profesa Mwaikusa nyumbani kwake kwa kuwa kabla ya kufikwa na mauti, alitaka azikwe katika nyumba yake hiyo.
"Kabla ya kifo chake baba aliwahi kutuambia kuwa akifa azikwe hapa nyumbani. Uzuri ni kwamba maneno hayo hakutuambia sisi tu, alikuwa akiwaeleza na ndugu zetu wengine," alisema Baraka.
"Baba alikuwa na nyumba nyingi, lakini aliwahi kusisitiza kuwa akistaafu atakuwa anaishi hapa na akifa azikwe hapahapa nyumbani kwake."
Awali kabla ya kupangwa siku ya mazishi, taarifa zilieleza kuwa baadhi ya ndugu wa marehemu walitaka marehemu akazikwe Mbeya, lakini mke wake na watoto, walishinikiza azikwe Dar es Salaam.
"Hili jambo tumeshalimaliza; hayo ni mambo ya kawaida ambayo hutokea msibani, lakini tulivyowaeleza ndugu zetu juu ya kauli alizozitoa baba, mambo yote yakaenda sawa. Kwa hiyo baba yetu mpendwa tutamzika hapa nyumbani," alisema Baraka.
This comment has been removed by a blog administrator.
ReplyDeleteThis comment has been removed by a blog administrator.
ReplyDelete