Monday, July 26, 2010

M A Z I N G A O M B W E YA C C M TANZANIA

http://newhabari.co.tz

*Yajipanga kusimamia njia kuu za uchumi
*Yasisitiza elimu ya kujitegemea kwanza


*Yasema bila sayansi Taifa halifiki popte
*Yaagiza Serikali kufumua mitaala ya elimu
*Yakiri wingi wa wasomi umeanza kuwa tatizo

CHAMA cha Mapinduzi (CCM), kimeufanyia mapinduzi makubwa Mwelekeo wake wa sasa kwa kuamua uwalenge zaidi wananchi wa kipato cha chini ili waweze kushiriki katika mfumo halisi wa uchumi wa dunia ya sayansi na teknolojia.

Sambamba na hayo, Chama hicho kimeangalia kwa kina mwenendo wa uchumi wa dunia, na siasa za hapa nchini na kubaini kwamba kuna kila sababu ya kupunguza pengo kati ya walio nacho na wasio nacho.

Na ili kufanikisha mambo hayo, CCM imeamua kwamba kuanzia sasa itarejesha mfumo wa Upangaji wa Mipango na Usimamizi wa Uchumi ili kuipa dola nafasi ya kuwa mhimili wa uchumi katika mazingira ya ujenzi wa msingi wa uchumi wa kisasa wa Ujamaa na Kujitegemea katika mazingira ya uchumi wa soko na utandawazi.

Maamuzi hayo yamo katika madokezo yake kadhaa, ambayo yalipitishwa na Halmashauri Kuu ya CCM kabla ya kuwasilishwa katika Mkutano Mkuu wa chama hicho uliomalizika mwishoni mwa wiki mjini Dodoma.

Maamuzi hayo, yanaonekana kwamba Tanzania imeamua kufuata mfumo wa uchumi wa China; nchi ambayo Ujamaa pamoja na Ubepari vinafanya kazi sambamba, huku nguvu ya kiuchumi ya mabepari ikisaidia kupambana na umaskini wa walio wengi.

Tangu mageuzi hayo ya kukumbatia mifumo miwili ndani ya nchi moja yaasisiwe mwaka 1978, China imepiga hatua kubwa katika maendeleo ya uchumi. Mwaka jana, pato la nchi hiyo lilikuwa Yuan trilioni 30.07 ambazo ni sawa na dola za Marekani trilioni 4.287, ikiwa na ongezeko la uchumi la asilimia 9.3.

Mageuzi hayo, yaliletwa na Den Xiao Ping, ambaye alibadilisha mfumo wa Kikomunisti uliokuwa umeitenga China ya Mao Tse Dong na ulimwengu wa nje.

Baada ya mabadiliko hayo, uchumi wa China umekuwa ukikua kwa kasi ya ajabu, kiasi cha kuwa tishio kwa mataifa makubwa kiuchumi kama vile Marekani na Japan.

Katika kijitabu cha CCM cha Mwelekeo wa Sera za CCM katika Miaka ya 2010 hadi 2020, CCM inataja malengo makuu ya mwelekeo huo ambayo yana mambo kama sita hivi.

Baadhi ya mambo hayo ni pamoja na kupambana kikamilifu na suala la uchumi duni na tegemezi, kwa kujenga msingi wa uchumi wa kisasa wa Taifa linalojitegemea, na unaozingatia matumizi ya kiwango cha juu cha maarifa yatokanayo na sayansi na teknolojia.

Ili kuweza kufanikisha jambo hilo, chama kinaziagiza Serikali zake kujipanga kuwawezesha wananchi kiuchumi, kwa kuwapa elimu ya kisasa itakayowawezesha kufanikisha Mapinduzi katika Kilimo na Ujasiriamali.

Chama hicho kinasema ili mkakati wa kujenga msingi wa uchumi wa kisasa wa Taifa linalojitegema, ni lazima itolewe elimu ya kisasa. Na kwa msingi huo, Chama kinaziagiza Serikali zake mbili; Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kuchungulia upya katika mitaala yake na kuifumua ili kuweza kukumbatia sayansi na teknolojia tangu ngazi ya awali ya mfumo wa elimu.

“Kwa vile uchumi wa kisasa unahitaji watenda kazi wenye ujuzi na maarifa ya sayansi na teknolojia, ni lazima (watenda kazi hao) waandaliwe kwa kupewa elimu bora na ya kisasa,” inasema sehemu ya kijitabu hicho cha Mwelekeo wa CCM.

Aidha, chama hicho kinasema bila matumizi ya elimu ya sayansi na teknolojia, nchi haiwezi kuondokana na uchumi ulio nyuma na tegemezi.

“Kwa hiyo, lazima yafanyike marekebisho katika mitaala ili mafunzo yanayotolewa yapate mwelekeo wa sayansi na teknolojia. Serikali itatilia mkazo uwekezaji wa raslimali katika utafiti na kuufanya utafiti kuwa agenda ya kitaifa kwa kutenga asilimia moja (1%) ya pato ghafi la Taifa, kwa ajili ya utafiti na maendeleo,” inasema sehemu ya kijitabu hicho na kuongeza kuwa lazima Serikali isimamie taratibu za uhawilishaji wa teknolojia na utoaji hakimiliki kwa watafiti na wagunduzi.”

Kwa ujumla, mwelekeo huu unaonyesha dhamira ya CCM katika uwezeshaji wa wananchi mmoja mmoja na katika vikundi.

CCM inasema: “Mkakati mkuu wa uwezeshaji wa kiuchumi wa wananchi, ni ule unaohakikisha kwamba wananchi wenyewe wanamiliki na kuendesha uchumi wa nchi yetu ama mmoja mmoja kwa kupitia vyama vyao huru vya ushirika au kwa kupitia kampuni za wananchi ya ubia.

“Wakati huo huo, Watanzania wenye vipaji wataandaliwa katika fani za uongozi wa uchumi na kuwasaidia watu ambao wako tayari kuthubutu kuchukua hatua za kiuchumi. Kuthubutu kiuchumi, ndiyo chimbuko la msukumo katika uchumi wa kisasa.”

Moja ya mambo ambayo yamekuwa yakimhangaisha Rais Jakaya Kikwete tangu alipokuwa akinadi Ilani ya CCM ya mwaka 2005, ilikuwa ni tatizo la uwezeshaji wa watu wenye uwezo wa kuthubutu. Amerudia kusema mara kadhaa na amerudia tena kwenye mkutano mkuu uliomalizika Dodoma, kwamba benki za biashara si rafiki wa masikini.

Kwa maneno mengine, Mwelekeo huuu wa sasa wa CCM umekuja na majawabu juu ya dukuduku la muda mrefu la Rais Kikwete, la kutafuta uwezeshaji wa watu wenye nia ya kuthubutu kufanya mambo makubwa.

Kwa mujibu wa CCM, kwa mtazamo mpana wa Sera ya Uwezeshaji Kiuchumi, aina ya kwanza ya uwezeshaji ni ile ya mtu mwenyewe kujiwezesha. Yaani mtu anajiwezesha pale anapotambua vipaji alivyonavyo na anaamua kujituma kwa kuvitumia vipaji hivyo.

“Kwa ujumla, elimu yetu hadi hivi sasa imeegemea kwenye kuelimisha watu ili waajiriwe au watumwe. Lazima sasa elimu tunayoitoa kwa vijana wetu ijielekeze kwenye kuandaa watu wenye kujituma. Wanaojiajiri ni watu wanaojituma.

“Kuna vijana wengi wanaomaliza masomo ya sekondari, ya vyuo na hata vyuo vikuu, lakini hawapati kuajiriwa kwa sababu uchumi haupanuki kwa haraka kiasi. Hivyo jambo jema la nchi kuwa na watu wengi, vijana wengi waliosoma vizuri, sasa limeanza kuwa tatizo kwa nchi

“Kuwa na vijana wengi waliosoma, ni nguvu kubwa kwa Taifa. Ili Taifa liweze kuitumia nguvu hiyo kwa maslahi ya vijana wenyewe na kwa maendeleo ya kiuchumi na jamii ya nchi yetu, CCM itazitaka Serikali kuibua Mpango Kabambe wa kuwawezesha kiuchumi vijana wasomi walio tayari kujituma kwa kujiajiri ili watumie nguvu na maarifa waliyonayo,” CCM inaagiza.

Je; ni mpango gani umeandaliwa kwa vijana hawa? Chama hicho kinasema kwamba Serikali italazimika kuwapa mafunzo ya ujasiriamali na yanayohusu shughuli wanazokusudia kuzifanya, lakini pia Serikali iweke utaratibu mwepesi wa kupata mikopo nafuu.

Chama hicho kinasema wale wote watakaokuwa na nia ya kushiriki katika mpango huo, washauriwe kuunda chombo chao cha kushauriana.

“Utaratibu wa aina hii, wa kuwawezesha wasomi na wataalamu kujiajiri, una manufaa mawili kwa Taifa. Kwanza, unatoa ajira ya uhakika kwa wahusika na hivyo kuipunguzia nchi tatizo la watu kukosa ajira na madhara yake, na pili; unawezesha wasomi kutoa mchango chanya katika kujenga uchumi wa kisasa na kuongeza utajiri wa nchi,” inasomeka sehemu ya kijitabu hicho.

Chini ya utaratibu wa kuwawezesha wasomi, wajasiriamali, wafanyabiashara wa kati na wa juu, CCM inaziagiza Serikali zake kuandaa mkakati wa kibenki ambao utawezesha upatikanaji wa mikopo kwa makundi yote hayo.

“Benki nyingi tulizonazo sasa kwa aina ya shughuli zao, ni benki za kibiashara zaidi kuliko zile za kuendeleza sekta za uzalishaji mali, hususan kilimo. Aidha, hutoza riba kubwa. Hivyo ni muhimu Serikali ikahakikisha kuwa kwa makusudi, vinaanzishwa vyombo vya fedha ambavyo vitasaidia kuwawezesha wananchi kwa riba nafuu kuliko ilivyo sasa, ikilenga uanzishwaji wa Benki ya Kilimo, Benki ya Kuendeleza Viwanda na Benki ya kutoa mikopo ya muda mrefu ya ujenzi wa nyumba,” inaagizwa.

No comments:

Post a Comment