Imeandikwa na Anastazia Alfred, Magdalena Balisidya, Amina Mrope (DSJ), Beatrice Shayo, Restuta James, Joseph Mwendapole, Richard Makore, Moshi Lusonzo, Romana Mallya na Eliwinjuka Shani.
CHANZO: NIPASHE la tarehe 06/07/2010.
Ukiwa Dar ogopa maeneo haya
Na Waandishi wetu
5th July 2010
Uhalifu, mauaji nje nje!
Eneo la Mbezi wilayani Kinondoni hivi sasa ndilo linaloongoza kwa matukio ya uhalifu katika Jiji la Dar es Salaam.
Kuna mlolongo wa matukio ya ujambazi katika maeneo ya Mbezi ambapo watu kadhaa wameuawa miezi ya karibuni kwa kupigwa risasi kwa kuvamiwa nyumbani na wengine kuvamiwa wakiwa kwenye magari yao wakati wakijiandaa kuingia nyumbani na kupigwa risasi.
Miongoni mwa matukio yaliyotokea Mbezi ni la takribani wiki moja iliyopita na kulihusisha kundi la watu saba waliokuwa na silaha za moto ambao walivamia kwenye nyumba inayomilikwa na mfanyakazi wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Elinawinga Massawe mkazi wa Mbezi Msakuzi, Makondeko kata ya Kibamba, na kumuua kinyama kwa kumpiga risasi ya kichwa Nkingwa Mboja (25), mfanyakazi wa kiume wa nyumba hiyo.
Aidha, katika tukio hilo watu wawili walijeruhiwa ambao ni mwalimu wa Shule ya Chekechea iliyopo eneo hilo, aliyetambuliwa kwa jina moja la Ndimpo ambaye alipigwa risasi kifuani wakati mama wa baba wa nyumba hiyo, Mamboloo Massawe (85) alijeruhiwa na kitu chenye ncha kali kwenye mkono wake wa kushoto.
Jeshi la polisi lilifanikiwa kuwatia mbaroni watuhumiwa wanne.
Juni 13, mwaka huu, Padri wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mavurunza, Athanas Zengo, akitoa mahubiri ya Jumapili, alilaani matukio ya ujambazi pamoja na mauaji ya raia wasio na hatia katika maeneo ya Kimara na Mbezi na kuwatupia lawama viongozi wa serikali wenye dhamana ya usalama wa raia kutokuwajibika.
Alisema kila baada ya siku chache anashiriki kuwazika raia wasio na hatia wanaouawa na majambazi.
Padri huyo alisema viongozi hao walioshindwa kutimiza wajibu wao ni afadhali wakajiuzulu na wasipofanya hivyo, wananchi wasiwachague katika uchaguzi mkuu ujao.
Uporaji pikipiki Goba
Matukio ya kuwapora pikipiki vijana wanaofanya biashara ya usafirishaji wa abiria na kuwaua yameshamiri katika maeneo ya Mbweni, Goba na Tangi Bovu kwa kutaja machache.
Katika eneo la Mbweni kuna matukio zaidi ya manne yameripotiwa hivi karibuni baada ya watu wasiofahamika kuwakodi vijana wenye pikipiki na kisha kuwaua na kuwapora pikipiki.
Tukio la karibuni lilitokea Jumatano usiku Mbezi Tangi Bovu na kuwalazimisha vijana wanaofanya biashara hiyo katika eneo hilo wiki iliyopita kuandamana kupinga vitendo vya polisi wa Kawe kuwatishia pale wanapotaka watuhumiwa wachukuliwe hatua.
Watoa huduma wa pikipiki huko mbweni, Bunju na maeneo mengine wilayani Kionondoni wanalalamika kuwa polisi hawafuatilii matukio ya kuuawa licha ya kupelekewa taarifa.
Kwa upande wa Makongo Juu, wakazi wake wanasema kuwa vitendo vya uhalifu eneo hilo bado ni tatizo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wakazi hao walisema kuwa matukio ya uhalifu hasa utumiaji wa silaha kama rungu, panga, shoka na silaha za moto yamekuwa yakiendelea.
Mmoja wa wananchi wa eneo hilo akizungumza na gazeti hili kwa masharti ya kutotajwa jina, alisema vitendo hivyo vimekuwa vikitokea nyakati za usiku.
Alitolea mfano tukio lililotokea zaidi ya wiki moja iliyopita majira ya saa 2:00 usiku ambapo majambazi walivamia maduka mawili, grosari na genge na kupora mali na fedha.
Makongo nako moto
Katika tukio hilo lililotokea Makongo eneo la Saiberia, watu watatu walijeruhiwa sehemu mbalimbali za miili.
Katika kipindi cha mwaka huu zaidi ya matukio matatu makubwa yalitokea ambapo kati ya hayo moja lilisababisha kifo cha mkazi mmoja baada ya majambazi kuvamia kwenye duka moja.
“Maeneo ya huku kama unavyoyaona ni mapori, yametuzunguka na nyumba zipo moja moja, hivyo wahalifu wamekuwa wakitumia mwanya huo kupora wananchi au kuvamia na kupora mali kwenye maduka au majumbani,” alisema.
Alisema Jeshi la Polisi linatakiwa kujipanga ipasavyo ili kuhakikisha maeneo kama hayo yanapata vituo vidogo vya polisi.
“Tunahitaji tuwe na kituo cha polisi huku kwanza wakazi ni wengi na kituo tunachokitegemea ni cha Chuo Kikuu ambacho kinahudumia watu wengi,” alisema.
Ubungo Darajani himaya ya vibaka
Nalo eneo la Ubungo Darajani linatajwa kushamiri vitendo vya uhalifu hasa wa kupora watu.
Inadaiwa kuwa genge la vijana zaidi ya 20 linalofanya uhalifu limepiga kambi katika eneo hilo kiasi ya kuhatarisha maisha ya wakazi wa eneo hilo na wasafiri wanaotumia barabara ya Mandela.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kibangu, Kata ya Makuburi, Desdery Ishengoma, alithibitisha kukithiri kwa vitendo hivyo na kueleza kuwa vinachangiwa na biashara ndogondogo zinazofanywa kando kando mwa barabara ya Mandela, eneo la Darajani.
Alisema tayari ofisi yake imeandika barua kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni na kupendekeza kuwa eneo hilo lifanywe bustani za miti na maua badala ya biashara ndogondogo.
Alisema mbali ya pendekezo hilo, ofisi yake imetengeneza mpango wa kuweka sungusungu katika eneo hilo na kwamba kwa sasa vijana watakaoshiriki kazi hiyo wameanza mazoezi.
“Kwa kweli hapa darajani hali ni mbaya sana, watu wanaumizwa na kuporwa kila saa na kila siku...sisi tumeshaliona tatizo hilo na kama nilivyokueleza, tumeanza kuchukua hatua,” alisema Ishengoma.
Alisema kwa siku wamekuwa wakipokea malalamiko zaidi ya matano kutoka kwa watu mbalimbali wanaojeruhiwa na kundi hilo la uhalifu.
“Lakini naamini hao ni wale wachache wanaoamua kuja kwetu, matukio ni mengi sana kutokana na hatari iliyopo,” alisema.
Wananchi waliozungumza na gazeti hili walisema kikundi cha vijana hao kimekuwa kikifanya uhalifu na kukimbilia chini ya daraja.
Alfred Mushi, mkazi wa eneo hilo alisema vibaka kwenye eneo hilo wamekithiri huku polisi wakifumbia macho matukio ya uporaji na kuwaacha vibaka wakitamba.
“Si unaona kituo cha polisi kipo jirani tu, lakini hapa vibaka wanatamba utafikiri hamna vyombo vya dola...ukienda polisi unaulizwa una gari? au wanakuambia hawawezi kutoka kwa sababu hakuna askari wa kubaki kituoni,” alisema Mushi.
Alisema wakati mwingine askari wamekuwa wakiandika maelezo na kuahidi kufuatilia tukio, lakini hawafanyi hivyo na ndio maana vibaka wanatamba katika eneo hilo.
Alisema: “Hali hiyo imekuwa ikichochea hasira za wananchi, ndio maana wakifanikiwa kukamata mhalifu wanamchoma moto kwa kuwa polisi wakimkamata kibaka asubuhi, mchana unamkuta mtaani.”
Mwananchi mwingine, Abdalah Jumaa, aliwalaumu askari wa vituo vidogo kuwa na kasumba ya kupuuza malalamiko ya wananchi.
“Ukiongea na Kova (Suleiman Kova, Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam) anakujibu vizuri kuliko hawa askari wadogo, yaani ukiwa na tatizo huwezi kuhudumiwa bila kuwasiliana na Kamanda Kova ili awaagize watu wake katika vituo husika...sijui kwa nini hawa askari wako hivyo,” alisema.
Polisi wa Kituo kidogo cha Ubungo Kibangu ambao hawakupenda kutaja majina yao, walisema wakati mwingine wananchi wamekuwa wakikuza matukio ikilinganishwa na hali halisi.
“Kama wananchi wanasema hapo Darajani kunatisha, mbona hawaleti malalamiko yao hapa? Ni kweli pale kuna vibaka, lakini sio tatizo kubwa kama ulivyoelezwa na hao unaosema ni wananchi,” alisema askari mmoja.
Baada ya kueleza hayo, askari wa kituo hicho walimtaka mwandishi wa habari hizi kuwasiliana na Kamanda wa Kanda Maalum kwa ufafanuzi zaidi kwa maelezo kwamba wao sio wasemaji wa jeshi la polisi.
Mwananyamala na vibaka
Kwa upande wa Mwananyamala, wakazi wa eneo hilo wamelalamikia ongezeko la vibaya na kulitupia lawama Jeshi la Polisi kwa kushindwa kukabiliana na vitendo vya uhalifu vinavyoendelea kutokea eneo hilo.
Siwema Juma, mkazi wa eneo hilo alisema, kila kukicha eneo hilo kumekuwa na ongezeko la vibaka ambao wamekuwa wakiwaibia wakazi na wapita njia.
Alisema baadhi yao hujifanya kuwa ni wapiga debe ambao wamekuwa wakiwaibia abiria.
Siwema alisema vibaka hao wanazidi kushamiri katika eneo hilo na hakuna hatua zozote zinazochukuliwa.
Mwanyekiti wa Serikali za Mtaa, Kitwana Katembo, alisema mara kwa mara wamekuwa wakiwakamata wahalifu na kuwachukulia hatua.
Hata hivyo, alisema hivi sasa kuna unafuu kulinganisha na kabla ya Januari.
Alisema ndani ya mwaka huu matukio yanayojitokeza zaidi ni ya uporaji wa simu.
Eneo lingine ambalo linatisha kwa uhalifu ni Jangwani ambapo wakazi wake wamesema kuwa eneo hilo kuanzia Magomeni hadi Faya sio salama.
Licha ya kutoa taarifa kwenye jeshi la polisi eneo hilo bado ni hatari.
Baadhi ya wakazi wa jiji wakizungumza na gazeti hili, walisema bado tatizo hilo linaendelea eneo hilo na kwamba wanaoibiwa mara nyingi ni wanawake.
Mkazi wa eneo hilo aliyejitambulisha kwa jina moja la Mwajuma, alisema kuwa kuna uhalifu wa kutisha katika maeneo ya Magomeni hadi Jangwani.
Wakazi wengine wanasema inapofika saa moja usiku ni hatari kuvuka eneo hilo kwa miguu na kwamba hali ni kama hiyo majira ya afajiri.
Aidha, wanasema vibaka wanapora watu simu, mikufu, mikoba ya na mali nyingine za wanaokuwa kwenye magari na kukimbia.
Wakati wakazi wakilalamikia hali hiyo, Mwenyekiti wa Serikali za Mitaa Magomeni, Shawedi Abdallah, alisema uhalifu katika eneo hilo umepungua kulinganisha na miaka ya karibuni.
Tabata Relini moto
Eneo la Tabata Relini nalo linatajwa kushamiri kwa uhalifu ambapo wakazi wameliomba Jeshi la Polisi kuweka ulinzi katika kituo cha Tabata Relini kufuatia eneo hilo kushamiri vibaka na kufanya uporaji.
Wakazi hao walisema vitendo vya uhalifu vimezidi kushamiri katika kituo cha daladala na kwamba kila siku watu wanaporwa vitu ikiwemo simu, mikoba na kuachiwa majeraha mwilini kwa kuchanwa na vitu vyenye ncha kali.
Amina Omary, mkazi wa eneo hilo alisema wanawake wanaongoza kwa kufanyiwa uporaji na vibaka ambao amedai wanaofanya vitendo hivyo ni vijana wanaotumia dawa za kulevya.
Alisema ingawa polisi wanafahamu eneo hilo ni hatari, hawaweki ulinzi wakati wa usiku.
“Polisi wanafahamu eneo hili lina vibaka lakini hawaweki ulinzi na kila leo watu wanaporwa ikifika saa mbili usiku tunaogopa kusimama kituoni kusubiri usafiri,” alisema.
Balozi wa Nyumba 10, Juma Selemani, alisema vitendo vya ukabaji katika eneo hilo ni tatizo sugu na watu ambao sio wenyeji wa eneo hilo wanaporwa kwa kutokana na kutofahamu kuwa muda wa usiku eneo hilo ni hatari.
Alisema ili kukomesha vitendo hivyo eneo hilo ameliomba Jeshi la Polisi kufanya ulinzi na kuwakamata wapiga debe na kuongeza kuwa ndio wahusika.
Tabata Kimanga nako kunatajwa kushamiri kwa vibaka ambao ni tishio.
Wakazi hao walisema kuwa wakati mwingine vitendo vya wizi na uporaji hufanyika mchana, lakini hakuna hatua zinazochukuliwa.
Mkazi wa Tabata Bima, Boniface Shangwe, alisema vibaka wengi ni wale wanaopiga debe mchana na inapofika usiku wanageuka wezi.
“Hapa Tabata Bima usithubutu kupita peke yako zaidi ya saa tano, huwa wanajibanza hapa kona kuna ka-uchochoro haipiti siku tatu utasikia mtu kaporwa,” alisema.
Alisema wapiga debe hao pia wamekuwa wakiwakwapulia mabegi wanawake kwenye daladala na kuchukua simu za wanaume kwa kujifanya wanawania kupata usafiri.
Mkazi wa Tabata Savannah, Justa Mbiro, naye aliwaelekezea lawama wapiga debe kuwa mara nyingi huwa ni vijana ambao wameshindikana nyumbani kwao hivyo kuamua kuhamia katika kazi hiyo.
“Kuna mtu juzi alikuwa anatoka muziki hapa Tabata Mawenzi akapigwa panga kichwani, hawa ni vijana wa hapa hapa wanavizia watu wanaotoka muziki na kuwafuatilia hadi sehemu wanazoona giza wanaanza kazi yao,” alisema Mbiro.
Kutokana na shida ya usafiri kutoka Ubungo Extenal kuelekea Kisukuru kupitia shule ya Yusuf Makamba, watu wengine huamua kutembea kwa miguu kukatisha jeshini kuelekea Kisukuru sehemu yenye umbali kama kilomita tatu.
“Eeneo hili lina msitu mkubwa kwa kuwa ni eneo la jeshi sasa ukipita usiku ni giza kweli kweli na unapaswa kuwa na roho ngumu kama uko peke yako maana vibaka wamekuwa wakijificha vichakani na wakiona kama kuna mtu anapita peke yake wanamvamia,” alisema mkazi wa Kisukuru, Amina Mwamba.
Roba mbao ya misumari
Maeneo mengine yaliyokithiri kwa wizi ni maeneo ya Tabata Dampo barabara ya Mandela ambapo wizi wa maeneo hayo umebatizwa roba ya mbao.
Vibaka hao wamekuwa wakitumia njia ya kuwakaba koo watu wanaopita maeneo hayo kwa kutumia mbao iliyojazwa misumari.
“Roba ya mbao isikie tu maana hiyo hata ungekuwa na nguvu gani wakikuwekea hiyo unapaswa kutulia tu na kutoa kila ulichonacho, ile mbao inakuwa na misumari iliyochomekwa sasa wakikuwekea wanakwambia toa ulichonacho ukibisha wanazidisha kukaba na inaweza kukutoboa koo,” alisema mkazi wa maneo hayo, Joseph Minde.
Buguruni kituo cha mabasi nako ni eneo hatari lisilofaa kupita kuanzia saa nne usiku. Wapiga debe wa maeneo hayo wanaodaiwa kufanya kuwakaba watu na kuwapora.
Maeneo ya Temeke nayo si salama kutokana na kutapakaa kwa vibaka. Kwa mfano, Jumapili iliyopita, mkazi mmoja wa Tabata aliporwa simu, Sh. 20,000 na heleni majira ya saa nne usiku eneo la Temeke Hospitali.
Mkazi huyo alisema aliporwa baada ya kukabwa na kundi la vibaka, lakini hakuripoti polisi kuepuka kupoteza muda wake.
Naye Mwenyekiti wa Serikali za Mitaa wa Bahari Beach, Gaspari Raphael, amesema uhalifu umezidi katika mtaa huo na kwamba unasababishwa na vijana wasio na ajira na wengi ni waliofukuzwa kwenye machimbo ya Ununio.
Gilbert Mrosso, mkazi wa eneo hilo, alisema hivi karibuni alinusurika kufa, baada ya kuvamiwa na majambazi na kumjeruhi vibaya na kuporwa mali na kuwa alipohitaji msaada wa polisi hawakufika.
Yombo usiamke alfajiri
Nao wakazi wa Yombo Kilakala wamelalamikia kuwepo na makundi ya ujambazi, hali ambayo inawazuia kuamka mapema kwenda katika biashara zao.
Catherine Mrema, alisema wanapokuwa wakipita kuelekea kituoni hukutana na makundi hayo kisha kutishiwa na mapanga na kuporwa.
Mkazi mwingine, Allen Ngugo, alisema mara nyingi majambazi huvamia maduka na kupora.
Aidha, alisema eneo hilo ni sehemu ya majambazi kujificha baada ya kufanya uhalifu maeneo mengine.
Mwenyekiti wa Serikali za Mitaa wa eneo hilo, Yahaya Mnari, alithibitisha kutokea kwa matukio hayo.
Alisema matukio ambayo yametokea karibuni ni uvunjaji wa maduka na kuvamia nyumba za wageni na kuwapora mali zao.
Mnari alisema hata katika tukio la wizi wa ujambazi uliofanyika katika ATM ya NMB iliyoko katika eneo la Hospitali ya Temeke gari ilifichwa darajani baada ya kufanya uhalifu huo.
Alisema kwa sasa wametafuta kikundi cha watu 30 ambao watapatiwa mafunzo ya ulinzi shirikishi ili kupunguza wimbi la ujambazi katika eneo hilo.
Vitendo vya uhalifu pia vimeshamiri Yombo Dovya, ambapo wananchi wanalalamikia hali hiyo.
Lina John, alisema kuwa eneo la shule linatumiwa na makundi ya vibaka na wahalifu wengine kuwapora mali zao.
Kwa upande wao, wakazi wa Mbagala wanasema kuwa matukio ya wizi wa kutumia nguvu yanaendelea kuwapa hofu, ambapo makundi ya vijana wanaofahamika kama ‘Mbwa Kachoka’ na ‘Mbwa Mwitu’ yanaendelea kuvamia nyumba na kuiba.
Wanaliomba Jeshi la Polisi kuendelea kukabiliana na makundi hayo ambayo ni hatari kwa maisha yao.
Hassan Ngayonga, mkazi wa Mbagala Kiburugwa, alisema licha ya polisi kukabiliana na makundi hayo, bado yanaendelea kuvamia na kupora.
Maeneo ambayo yanaonekana kuvamiwa mara kwa mara ni Charambe, Nzasa, Kiburugwa na Shimo la Mchanga.
Diwani wa kata ya Mbagala, Tito Osoro, akielezea matatizo hayo, alisema kwa ujumla tishio la makundi ya watu hao hakuna kwa kuwa Polisi wamewasambaratisha kwa kuvamia kambi zao na kuwakamata.
Eneo lingine linalotisha kwa uhalifu ni Daraja la Salender ambako licha ya kuweko na kituo cha polisi, vibaka wanawakaba wapitia njia na kuwapora.
No comments:
Post a Comment