Monday, July 26, 2010

MGOMBEA AKUTWA NA MGUU WA MTU MAKONGOROSI, CHUNYA, TANZANIA

Mgombea akutwa na mguu wa mtu Mbeya
*Ni wa Chadema aliuficha uani, akamatwa

Na Maregesi Paul

MGOMBEA ubunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), katika Jimbo Jipya la Makongorosi lililoko Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya, George Mtasha (50), amekamatwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya baada ya kukutwa na mguu wa mtu.

Katika tukio hilo, Mtasha ambaye pia ni mwenyekiti mstaafu wa chama hicho Mkoa wa Mbeya, amekamatwa na mwenzake aliyefahamika kwa jina la Paul Mnyambwa (43).

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Adcocate Nyombi, aliiambia MTANZANIA kwa njia ya simu jana kuwa, Mtasha na Mnyambwa walikamatwa jana saa 12.50 alfajiri baada ya polisi kupata taarifa kutoka kwa raia mwema, kwamba watu hao wanamiliki mguu wa mtu.
“Ni kweli kuna watu wawili wakazi Bwawani, Makongorosi Chunya ambao wote ni wafanyabiashara wa madini ya dhahabu, tunawashikilia hapa. Kabla ya kuwatia mbaroni, awali tulipata taarifa kutoka kwa raia wema ambao walitwambia kwamba, watu hao wanamiliki mguu wa mtu kitendo ambacho ni kinyume cha sheria.

“Tulipopata taarifa hizo, vijana wetu kutoka hapa mkoani, walikwenda huko na kufanya upekuzi katika nyumba ya Mtasha ambapo walikuta mguu wa kushoto ukiwa umefukiwa kwenye takataka ndani ya ua wa nyumba yake. Kwa hiyo, hivi tunavyozungumza watuhumiwa wote wameshafikishwa hapa mkoani, tunaendelea kuwahoji ili tujue ni kwa nini wanamiliki mguu huo na wameutoa wapi,” alisema Kamanda Nyombi.

Kwa mujibu wa Kamanda huyo wa polisi, mguu huo ni wa kushoto na ni kipande kilichoanzia gotini hadi kwenye nyayo.

Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Mbeya, Shambwee Shitambala, alisema kukamatwa kwa Mtasha ni pigo kwa chama hicho kwa kuwa alikuwa ameahidi kukisaidia chama wakati wa uchaguzi mkuu.

“Taarifa za kukamatwa kwa Mtasha ninazo ila inaonekana kuna mazingira ya kisiasa kwa sababu ni juzi tu amerudisha fomu za kugombea ubunge katika Jimbo la Makongorosi. Katika tukio hili nasikia mtoa taarifa alimpigia simu RPC badala ya OCD wa Chunya, kisha askari polisi wakatoka Mbeya Mjini kuja kuwakamata watuhumiwa Chunya wakati hata hapo Chunya kuna polisi,” alisema Shitambala ambaye kitaaluma ni mwanasheria.

Mtasha amekuwa Mwenyekiti wa Chadema tangu chama hicho kilipoanza kujulikana mkoani Mbeya miaka mingi iliyopita. Aliondolewa katika wadhifa huo Machi mwaka huu baada ya kushindwa katika uchaguzi uliomweka madarakani, Sambwee Shitambala.

No comments:

Post a Comment