Monday, July 26, 2010

WAGOMBEA MCHINGA WATUHUMIANA UCHAWI

Imeandikwa na Rashidi Mtagaruka, Lindi; Tarehe: 25th July 2010 Habari Leo



KAMPENI za kuwania uteuzi wa kugombea ubunge ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) jimbo la Mchinga lililopo Lindi Vijijini, mkoani Lindi, zimeingia sura mpya baada ya mgombea mmoja kumtuhumu mwenzake kuwa mchawi.

Tukio hili lililoshuhudiwa na mwandishi wa habari hizi, lilitokea juzi saa tatu na nusu asubuhi katika ofisi za CCM mjini hapa, lilimhusisha Mbunge anayetetea nafasi yake, Mudhihir Mudhihir ambaye alimuomba Mwenyekiti wa CCM Wilaya, Muhamed Gwaja kuwaondoa watu watatu wanaofuatana na mgombea mwenzake, Saidi Mtanda.

“Mheshimiwa Mwenyekiti, sina imani na watu walio ndani ya gari ya Mtanda, kwa maana ni wachawi,” alisikika akisema Mudhihir.

Hata hivyo Mtanda ambaye katika kampeni hizo zilizoanza Julai 22 mwaka huu, katika kata za Kiwawa na Milola alikuwa akitumia gari lake binafsi, alipinga pendekezo hilo kwa madai linapingana na kanuni za uchaguzi.

“Mwenyekiti kabla ya kukubaliana naye, kwanza atoe ushahidi wa kauli yake, maana Kanuni za uchaguzi hazijasema mahala popote kwamba mgombea haruhusiwi kuongozana na ndugu zake wakati wa kampeni,” alisema mgombea huyo ambaye ni msaidizi wa Katiku Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba. Mtanda aliongeza kuwa:

”Lakini pia kama Mudhihir mwenyewe si mchawi aliwezaje kuwabaini ndugu zangu katika msafara huo kuwa ni wachawi?”

Baada ya mabishano ya muda mrefu, Mtanda alitumia busara ya kuepusha mzozo huo ambao ulionekana kutaka kuathiri msafara wao uliokuwa ukielekea kata za Rutamba na Nangaru.

Akizungumza na gazeti hili baada ya ndugu hao watatu wa Mtanda kushushwa, Mkurugenzi wa Uchaguzi wilayani humo, Mohammed Nyama alisema haoni sababu ya kushushwa kwa watu hao. “Mudhihir hakupaswa kuwa na wasiwasi kiasi hicho, maana nchi yetu haiamini masuala ya uchawi.

Ninachoshukuru ni kuwa busara zimetumika kuepusha shari katika kampeni,” alisema. Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi anayefuatilia kampeni hizo, baadhi ya wagombea wamekuwa wakipata wakati mgumu kuwashawishi wanachama wa CCM wa jimbo la Mchinga.

Jimbo la Mchinga kwa miaka 15 sasa limekuwa chini ya Mudhihir ambao katika uchaguzi wa mwaka huu wamejitokeza wanachama wengine watano wanaoomba kuteuliwa kuiwakilisha CCM katika jimbo hilo. Mbali ya Mudhihir na Mtanda, wengine ni Mayasa Mikidadi, Khalfan Ng’uto, Said Farahani na mgombea aliyetambuliwa kwa jina moja la Mpwatile.

No comments:

Post a Comment