Sunday, July 25, 2010

NAPE NNAUYE ACHEZEWA RAFU UBUNGO DSM

Imeandikwa na Angela Semaya; Tarehe: 24th July 2010 "Habari Leo", Tanzania.

MWANACHAMA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye, anayeomba ridhaa ya kugombea Jimbo la Ubungo amelia kuchezewa rafu katika kampeni za kura za maoni zinazoendelea Dar es Salaam.

Nnauye akiwa kati ya wagombea 13 wa CCM waliopanda jukwaani kunadi sera zao kwa ajili ya kuomba kura kwa wanachama jana, alilalamika kuchezewa rafu baada ya kunyimwa nafasi ya kujibu maswali aliyoulizwa na wanachama waliotoka eneo la Tupendane na Kilimani kata ya Manzese waliokuwa wamekusanyika katika uwanja wa Kilimani.

Mara baada ya Nnauye kujinadi mbele ya wanachama, Mwenyekiti wa Kampeni, Thadeus Kiwenge, alihoji iwapo kuna mwenye swali wakajitokeza watu wawili ambao waliuliza maswali ambayo hata hivyo, Mwenyekiti huyo alidai hayakuwa ya msingi na kusababisha mtafaruku.

Muuliza swali wa kwanza alisema amesikia kuwa mgombea huyo ni mkorofi na ‘alikivua nguo’ chama hadharani, wakati muuliza swali wa pili alisema wamesikia mtaani kwamba hata wanachama wakilipigia kura jina lake haliwezi kurudi.

Kiwenge alisema hayo hayakuwa maswali ya msingi hivyo yasijibiwe na mgombea licha ya yeye Nnauye kutaka apewe nafasi ya kujibu huku wananchi nao wakishinikiza apewe nafasi hiyo, lakini akakataliwa.

Nnauye aliyeonekana kukerwa na kuzuiwa kujibu maswali hayo, ghafla alishuka jukwaani huku akirusha mikono na kulalamika na baadaye kuonekana akitulizwa na mgombea mwenzake, Hawa Ng’humbi.

“Hapana haiwezekani, hali hii tangu jana kuna watu wanapangwa kuniuliza maswali, halafu hawataki kunipa nafasi ya kujibu … nitapigania haki yangu hadi mwisho,” alisikika akisema.

Katika hali ya kuonekana kuchanganyikiwa, Nnauye aliondoka na gari lake kwenye mkutano na kisha kurudi baada ya muda, wakati wagombea wote wakiwa wamemaliza kujinadi.

Akizungumza na waandishi nje ya uwanja kutokana na tukio hilo, Nnauye alisema hali ilivyo ni dhahiri kuna mgombea amepangwa kwa alichodai ni kupewa muda mfupi wa kujieleza tofauti na wagombea wengine na kunyimwa haki ya kujibu maswali aliyoulizwa.

“Nina hakika nitashinda, mimi ni mwanachama halali. Nitadai haki yangu hadi mwisho … nitakachofanya ni kupeleka malalamiko yangu sehemu husika,” alisema.

Awali akijinadi, Nnauye alisema inahitajika damu mpya na kamanda atakayekuwa na nguvu ya kupambana na wapinzani, hasa katika jimbo hilo lenye upinzani mkali na kwamba yeye anaweza kupambana.

Ng’humbi alijikuta naye akiulizwa swali linaloshabihiana na la Nnauye na muuliza swali yule yule, hata hivyo yeye alipewa nafasi ya kulijibu na Mwenyekiti wa Kampeni.

Muuliza swali alimwambia Ng’humbi kwamba alikuwa meneja wa kampeni za Mbunge wa sasa, Charles Keenja ambaye inadaiwa hakurudi kwa wananchi kwa miaka yote akiwa mbunge na kuhoji ni namna gani mgombea huyo atawashawishi waweze kumwamini kumpa nafasi hiyo.

Ng’humbi ambaye alionekana kujibu kwa ujasiri, alisema alipewa jukumu na chama la kuwa meneja, lakini wenye mamlaka ya kuchagua mbunge walikuwa wao wananchi.

“Jamani mimi nilipewa jukumu la chama nikafanya, nikamleta kwenu. Lakini waliopiga kura kumchagua si ninyi au? Kama

hakurudi miye si kazi yangu, maana baada ya hapo niliondoka zangu baada ya kupewa kazi ya ukuu wa wilaya katika

maeneo niliyowatajia,” alisema.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Shamsa Mwangunga ambaye pia anaomba ridhaa ya CCM kugombea Ubungo, alitoa mpya baada ya kumaliza kujinadi na kisha kukiamkia Chama Cha Mapinduzi, shikamoo.

Mwangunga akijinadi alisema amekuwa na mchango mkubwa wa kuhamasisha na kuwezesha wanawake kuingia bungeni kwa kile alichoeleza kuwa ni mzoefu wa masuala ya wanawake, serikalini na bungeni. “Mimi si mshamba bungeni. Nina uchungu na kwetu Ubungo.

Niko jikoni, mkinipa nafasi naweza kuwatetea. Mimi ni mchapakazi hodari.

Rais Kikwete alisema wanawake hawajamwangusha na mimi ni sehemu ya wanawake hao,” alisema. Wagombea wengine waliojinadi ni Zangina Shanang Zaninga, Assumpta Nalitolela, Alfred Nchimbi, Kanali Gaspar Hiza, Peter Msuya, Dk. Apollo Kissai, Eliona Nkya, Slastaus Mwisomba, Perpetua Haule na Michael Lupiana.

Wakati huo huo, wagombea katika jimbo la Kinondoni nao walipita kuomba kura katika kata mbalimbali zilizopo katika wilaya ya Kinondoni.

Akijinadi katika Kata ya Makumbusho, mgombea mwenye umri wa miaka 23 na mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Tumaini, McDonald Runilinyilija alijifananisha na Mtume Muhammad na Bwana Yesu kwa kile alichosema walitumikia wananchi katika umri mdogo.

Runilinyilija alisema bungeni hakuna umri na kwamba akipewa nafasi anaweza kuwatumikia wananchi wa Kinondoni. Alisema, “chako ni chako tu hata kikiwa kizani utakiona, nipeni kura zenu.”

Iddi Azzan ambaye anatetea kiti chake, aliomba wanachama wampe tena kura za ndiyo ili arudi bungeni miaka mitano mingine kufanya kazi kwa kile alichoeleza miaka mitano iliyopita ilikuwa ya kujifunza.

Mgombea pekee mwanamke katika jimbo la Kinondoni, Shy-rose Bhanji, alisema sifa yake kubwa ni ya kutokata tamaa na kuwaomba wanachama wamwamini, wampe kura ili aweze kuwatumikia.

Wagombea wengine waliojinadi kuomba ridhaa Kinondoni ni Bakari Maige, Kakolwa Mbano, Mkuruma Muniwori, Mustafa Nuru, Mpoki Mwambulukutu na Issa Mohammed Issa.

No comments:

Post a Comment