Imeandkwa na Martha Mtangoo, Dodoma; Tarehe: 25th July 2010 Habari Leo
MAOFISA watatu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), mkoani hapa juzi walinusurika kupigwa na wananchi katika Kata ya Makulu,Kijiji cha Njedengwa baada ya kudhaniwa ni wezi.
Mkuu wa Takukuru mkoani hapa, Eunice Mmari aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa tukio hilo lilitokea juzi saa mbili usiku baada ya kupatiwa taarifa na raia mwema kuwa kuna baadhi ya viongozi wa eneo hilo wapatao 30 wamekusanyika nyumbani kwa Mwenyekiti wa Tawi la CCM Njedengwa kwa ajili ya kupewa pesa ili wamchague diwani.
Mmari alisema mara baada ya kupatiwa taarifa hiyo wakiwa njiani kuelekea eneo la tukio, waliona mtu akiwa katika pikipiki akiwa mbele ya gari lao waliamua kumpita na baada ya kumpita mtu huyo alipiga kelele za kuwataarifu Takukuru waliokuwa wanaelekea eneo hilo.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Takukuru wananchi hao waliokuwa wamekusanyika katika nyumba hiyo walipiga filimbi na kuwataarifu wanakijiji wenzao kuwa wameingiliwa na majambazi hali ambayo iliwafanya wanakijiji hao kuwazingira maofisa wa Takukuru na kutaka kuwapiga wakidai kuwa ni wezi.
Akielezea zaidi juu ya tukio hilo, alisema kuwa zaidi ya wanakijiji 200 waliwazingira na kutaka kuwapiga ambapo wengine waliwamwagia pombe na kudai kuwa ni wezi huku wengine wakisema kuwa kama wamekuja kwa ajili ya kumharibia diwani wao hawamuwezi ni bora wakamuacha.
Alisema kuwa waliwekwa chini ya ulinzi huku wakiwa wamezungukwa na wananchi kwa zaidi ya saa mbili.
Alifafanua kuwa sakata hilo liliisha saa nne na nusu usiku baada ya Mwenyekiti wa kitongoji hicho kuwasihi na kuwaachia huru wananchi hao ambao walitaka pia kuvunja vioo vya gari ya maofisa hao.
Aidha alisema kuwa, mbali na tuhuma hiyo pia Diwani huyo wa Kata ya Makulu, Ali Biringi anachunguzwa na Takukuru baada ya kukutwa na kadi 98 zisizo halali za CCM.
Alisema kuwa awali Takukuru ilipata taarifa juu ya diwani huyo kuwa na kadi hizo ambapo alikutwa na jumla ya kadi 177 za CCM ambapo baada ya kukaguliwa alikutwa na jumla ya kadi 98 zisizo halali na kuwa uchunguzi bado unaendelea
No comments:
Post a Comment