Sunday, July 4, 2010

LULU NA BUSARA ADHIMU ZA WANAMTANDAO WA TANZANET

3 Julai, 2010, Saada Al-Ghafry

Katibu,
Ahsante sana kwa ripoti hii. Nawaomba wanaukumbi nichukue nafasi hii kufanya jambo la kidikteta, nilishaahidi kuwa anapotakiwa dikteta, niko tayari wakati wowote, na ninawaomba wanaukumbi wengi, kama si wote, mniunge mkono kwa haya nitakayosema ili ukumbi usonge mbele badala ya kukwama kwenye matope na magurudumu yanabaki yakizunguka hapo kwa hapo.

Kwanza, sahani ukiziweka mahali pamoja, zinagongana, na binadamu ni hivyo hivyo.

Pili, uongozi ni jukumu, na uongozi wa Tanzanet hauna hata faida ya kulipwa wala marupurupu. Ingekuwa vizuri iwapo mawasialiano baina ya viongozi kwa viongozi, na viongozi na wanachama yangekuwa ya kiungwana na kuvumiliana.

Tatu, naomba tutambue kuwa kwa sababu uongozi ni jukumu, uongozi una wajibu wa kuwa mfano kwa wanachama na taifa, kama vile wazazi wanavyotakiwa kuwa mfano kwa watoto.

Nne, panatokea migongano, ni uungwana tukiwa wepesi wa kuombana msamaha tunapokoseana, na mwenye kuombwa msamaha, ni uungwana kuridhika na kumsamehe aliyekukosea. Hata kama huko nyuma tulikuwa wagumu wa kufanya hivyo, tufungue ukurasa mpya na tuanze kufanya hivyo sasa. Hakuna aliyekamailika: Sote tuna mema yetu, na sote tuna mapungufu.

Tano, wanaukumbi wote ni watu wenye majukumu mengi sana. Majukumu mengine yasitufanye tukazembea majukumu yetu humu ukumbini. Tuko hapa kwa ridhaa zetu wenyewe, hatukulazimishwa.

Sita, ni wajibu wa kila mwanaukumbi kuhakikisha kuwa uanachama wake ni hai, hata kama una uhakika kuwa umetuma pesa, kunaweza kukatokea matatizo kwenye mawasiliano baina ya chombo kinachotumiwa kutuma (km paypal, western union nk) na chombo kinachopokea (bank, mtu binafsi nk). Wakati wa mchakato wa kupokea ada, Stella alikuwa muwazi, alikuwa akitoa orodha ya wote ambao ameshapokea ada zao, na kushauri kila mmoja ahakiki kuwa orodha iliyotolewa imekamilika. Wajibu wa kuhakikisha kuwa jina lako liko kwenye orodha wakati wewe umeshalipa, ni lako mwenyewe, maana mwakilishi wa kanda na Mhazini, wote ni binadamu na inawezekana wamekosea. Kati ya mhazini, mwakilishi wa kanda na wewe binafsi, ni jambo rahisi kutafuta tatizo liko wapi iwapo una hakika umelipa na jina lako halipo kwenye orodha.

Saba, kuhusu ripoti ya Katibu, na kwa kukosa wadhamini, ndipo ninapoigiza udikteta:
Namba 1 na 2 ni wazi. Kwenye namba 3, nakubaliana na Stella, hasa ukizingatia hayo niliyokwishaandika hapo juu. Nitaacha namba 4 kwa sasa, na ningeomba majibizano baina ya Katibu na Mwasa2 yasitishwe mpaka hapo watakapopatikana wadhamini na/au mnadhimu wa ukumbi. Namba 6, inaelekea mwenyekiti amepitwa kidogo na wakati. Toka enzi za uenyekiti wa LGF ilibadilika kuwa walioko Tanzania pia walipe ada. Hata hapo ilipokuwa Watanzania wamepewa msamaha, aliyetaka kuwa na haki ya kura au kupigiwa kura, ilibidi alipe ada, kwa hiyo msamaha huo usingemuhusu PDN kama mwenyekiti hivyo halikuwa suala la kujadili kabisa wakati wa tatizo hili. Namba 6, 7 na 8 ningependekeza zisijadiliwe kwa sasa bali Katibu aziingize kwenye agenda ya mkutano mkuu kwa sababu maamuzi yake yawe ndiyo muongozo kwenye uendeshaji wa Tanzanet baadaye.

Nane, kuhusu mapendekezo ya Katibu, namba 2-6 pia ni mambo ya kujadiliwa kwenye mkutano mkuu kwani maamuzi yake yataingizwa kwenye uendeshaji wa Tanzanet.

Tisa, kwa niaba ya ukumbi, namuomba radhi Stella kwa kutomtendea haki. Wakati wa uchaguzi, alijinadi kinagaubaga kuwa yeye ni perfectionist. Ametekeleza wajibu wake kwa ufanisi wa hali ya juu kama alivyojinadi, sidhani kama kuna mtu yeyote ambaye haridhiki na utekelezaji wake. Mimi binafsi, na kwa niaba ya ukumbi, namuomba aendelee kwa sasa. Kazi aliyokwishaianza ni nzuri, aiendeleze kwa muda mpaka uchaguzi utakapofanyika. Namshauri PDN, kwa nia njema ya kuijenga Tanzanet, amwombe radhi Stella binafsi au kwenye kurugenzi, tujikwamue tulipo, tusonge mbele.

Yaliyopita si ndwele, tugange yaliyopo na yajayo.

Kumi, naomba uongozi uitishe mkutano mkutano mkuu. Nadhani ni miaka mitatu sasa hatujawa na mkutano mkuu kwa hiyo kuna mengi yanayohitaji kurekebishwa, kutoa madukuduku ya wanachama na viongozi nk.

Nawasilisha na naomba wanaukumbi mniunge mkono, tufupishe majadiliano na tusonge mbele.

Rgds,
Saada



2010/7/4 Dan Nkurlu

Wana Tanzanet,



Kwa asilimia 95, nimemaliza uchunguzi wa suala zima lililofikia kwa Mhazini wetu Stella Semiti-Munuo kujiuzulu wadhifa wake. Kikubwa kilichotokea ni mgongano wa mawasiliano na bahati mbaya, jambo hili lilikuzwa kupita kiasi kwa makusudi ya kuleta vurugu ukumbini na si kuleta upatanishi na kuhakikisha kuna maelewano kati ya Mhazini na Mwenyekiti.



Uchunguzi huu umebainisha yafuatayo :



Mwenyekiti alichelewa kulipa ada yake katika muda uliopangwa na hivyo mgongano wa mawasiliano na expectations pamoja na kutumiwa jumbe za kukumbushwa na kupewa upendeleo maalum.
Mwakilishi wa Kanda Salim Khatri, hakuwasilisha jina la Mwenyekiti kwa Mhazini baada ya kupokea ada kutoka kwa Mwenyekiti. Tarehe kamili ya ada hii kupokelewa haijathibitishwa.
Kuvunjika na mgongano kimawasiliano (communication and professionalism/cultural breakdown) kati ya Mwenyekiti na Mhazini ambayo yanaonekana wazi kwenye email kati yao za siku hiyo June 23. Kuna mgongano wa expectations na define roles za kimajukumu. Mwenyekiti anaona wajibu wa kuhakikisha orodha ya walipa ada inakamilika ni kati ya Mhazini na wawakilishi, huku Mhazini anaona kuwa wajibu wa mwanachama yeyote bila kujali cheo au eneo ni kuhakikisha anawasiliana na mwakilishi au anawasilisha jina lake na uthibitisho wa kulipia ada.
Mwasambili kwa kudhamiria aliamua kuchafua hali ya hewa ukumbini kwa kuleta hadharani majadiliano kati ya Mwenyekiti, Mhazini, Khatri, Madete na yeye Mwasambili na kudai Mwenyekiti kachemsha na anapaswa kuomba samahani, huku akiuacha kwa makusudi ujumbe wa Khatri ambao ulithibitisha kuwa Mwenyekiti amelipia ada na ni Salim aliyechelewa kupeleka uthibitisho kwa Mhazini.
Tuna tatizo la makusanyo ya ada Tanzania na kuna suala la kudai walioko Tanzania wasiwe walipa ada (mazungumzo yangu na mwenyekiti yaliashiria kuwa kuna kipengele kinachodai WanaTanzanet Tanzania wawe exempted kulipa kodi, unless wanagombea).
Wasio mafundi mitambo au wanachama bado wameorodheshwa kama mafundi mitambo (Mwasambili, Henry Mgaya)
Mhazini kawateua George Kakoti na Seppy Nyang’oro kuwa wenye funguo za Benki bila Kurugenzi na Wanachama wote kuwa na tarifa.
Kuna tatizo la ukusanyaji ada kwa ujumla bila kujali kanda. Hii inatokana na baadhi wanachama kuchelewa kulipia ada ama kwa makusudi au mazoea ya kutokuwa makini kulipia ada pindi mchakato wa kukusanya ada unapoanza. Kuna wanachama ambao walijitahidi kuwasilisha ada zao lakini walikosa mwakilishi wa kanda na hivyo ada zao ama kuchelewa au kuwa na tatizo katika kuzifikisha zinapopaswa.


Mapendekezo yangu ni kama ifuatavyo:



Kumuomba radhi Stella Semiti kutokana na yaliyotokea na kumsihi aendelee na kazi yake kama Mhazini. Ama upatanishi ufanyike kuondoa mgongano uliotokea kati yake na Mwenyekiti.
Kurugenzi iwasilishe mchakato wa kuchagua wanachama watano ambao watakuwa ni baraza la wadhamini ambao watakuwa na uwezo wa kuusaidia na kuushauri Uongozi ulioko madarakani kwenye shughuli za utendaji wa kila siku na panapokuwa na mfarakano au mgongano ndani ya Kurugenzi au kati ya wanachama.
Kuwepo kwa muda maalum kila mwaka ambao Wanachama wa Tanzanet watawajibikia kulipia ada zao. Hili litakuwa ni suala la kuongezwa katika taratibu za Tanzanet na kuelimishwa kwa kila mwanachama mpya na hivyo kuondoa utata unaoendelea kutokea (rejea majibu ya email yangu kwa Richard Madete mwishoni mwa Mwezi May 2010 kuhusiana na Panga).
Wanachama wa Tanzania wapewe maelekezo kulipia ada zao moja kwa moja kwenye akaunti CRDB na kuwasilisha nakala ya deposit slip kwa Salim Khatri na LGF ambao ndio washika funguo wa akaunti Tanzania. Aidha, online access ya akaunti hii ifunguliwe na Mhazini apewe access yak u-monitor account activities.
Mitambo ya Tanzanet na walio mafundi mitambo wawekwe wazi na wenye access wawe na udhibiti. Hand over inapofanyika, waliondoka kazini wanapaswa kuwa deleted na access zao kusitishwa.
Akaunti zilizoko BoA na CRDB, ziwe chini ya Tanzanet na majina ya Signatories na wenye access kwenye akaunti hizi zifanyiwe mabadiliko kila mara panapotokea mabadiliko ya wasimamizi wa fedha hizi na majina ya washika fedha yawe yamepitishwa na Wanachama wa Tanzanet kwa umoja baada ya kupendekezwa na uongozi.
Ukumbi ujadili na kutolea uamuzi kitendo cha Mwasambili kutuma email za majadiliano kati ya Mhazini na Mwenyekiti kama uchochezi na kupuuzia email ya Khatri na kuendelea kwake kudai Mwenyekiti amechemsha
Ripoti hii imekamilika kwa kutumia mtiririko wa email zilizotumwa hapa ukumbini na majibu ya maswali niliyotuma binafsi kwa Mwenyekiti Nkwera, Mhazini Stella, Mwasambili na Salim Khatri.


Wenu Katibu Tanzanet

Dan Nkurlu



Revolutionary Right Reverend Kishoka

No comments:

Post a Comment