Monday, July 26, 2010

Na Muhingo Rweyemamu, RAI - 26/7/2010

KWA vyovyote itakavyokuwa, Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu utatawaliwa na vijana, Rai inaweza kuthibitisha.

Tofauti na miaka ya nyuma ambayo siasa za uchaguzi ziliongozwa na kutawaliwa na wazee huku vijana wakiwa wasaidizi wa ushindi wa wazee hao, mambo yanaonekana kubadilika sana katika uchaguzi wa mwaka huu na vijana wanaonekana kujizatiti na mbinu mpya kuliko watu wa makamo.

Gia aliyoingia nayo Januari Makamba, ya kutembelea Jimbo zima la Bumbuli na kufanya kile wataalam wanaita ‘participatory research’ huku akibuka na kitabu kinachoeleza hali halisi ya wakazi wa Jimbo hilo, ni moja ya mambo yaliyowashitua siyo wagombeaji wenzake tu, bali pia hata vijana waliomo bungeni.

Wakielezea hali hiyo, Ismael Jussa, Mbunge wa kuteuliwa pamoja na Zitto Kabwe, walisema jambo alilolifanya Makamba, limewapa changamoto kama vijana ili waweze kufanya mambo makubwa zaidi ya hayo siku z ijazo.

Takwimu za idadi ya watu, zinatuonyesha kwamba Tanzania ni taifa changa. Kwa maana kwamba ina idadi kubwa ya watoto na vijana kuliko watu wazima. Kwa mujibu wa Shirika la Ujasusi la Marekani, CIA, wastani wa umri wa Watanzania ni miaka 18.7 Hii maana yake ni kwamba ukichukua umri wa wazee , ukajumlisha na umri wa watoto , kisha ukagawa mara mbili, umri wa wastani ni miaka 18

Katika Tanzania watoto wenye umri wa chini ya miaka kumi na tano ni milioni 17 wakiwamo wavulana 8,853,529 na wasichana 8,805,810. Wastani wao ni asilimia 43.


Watu wenye umri kati ya miaka 15-64 ni milioni 22 wakiwamo wanaume 10,956,133 na wanawake 11,255,868 na wastani wao ni asilimia 54 ya Watanzania wote wakati wenye umri juu ya miaka 65 wanafanya asilimia 2.9 ya Watanzania kuwa au kama watu milioni moja na nusu.

Hata hivyo, ukichukua watu wenye umri tangu miaka 0 hadi miaka 29 wanatengeneza asilimia 70 ya Watanzania ambao wengi wao ndiyo kundi kubwa la wapiga kura na hasa wanaopiga kura kwa mara ya kwanza ambao wanaingia katika uchaguzi na vionjo vyao, maono yao na matamanio yao.

Idadi kubwa ya vijana wapiga kura wamo katika Shule za Sekondari za kidato cha tano na sita (1.5) na kutoka Vyuo Vikuu wamo 82,428 ambao wanatarajiwa kuleta hamasa kubwa katika kampeni hizi.

Kihistoria, vijana wamekuwa nguzo muhimu katika ukombozi wa nchi yetu kupitia TANU, na pia katika kuhakikisha ushindi wa chama hicho na Chama Cha Mapinduzi ambacho ndiyo mrithi wa TANU.

Kwa bahati mbaya, katika miongo ya karibuni, vijana wengi wamekuwa daraja la wazee katika kufikia uongozi. Umoja wa Vijana wa CCM umekuwa ukitumika kuhamasisha watu kupiga kura, kujibu mashambulizi na kwa ujumla kutia hamasa chaguzi za chama.

Miaka ya karibuni, chama hicho kikongwe kilianzisha kikundi cha ‘Tanzania One Theatre Group’ ambacho kwa kiasi kikubwa, kimefanikiwa kuwakusanya Watanzania katika sehemu za kampeni na hivyo kusikiliza hotuba.

Vyama vingine vinejitahidi kuanzisha vikundi ingawa hakuna chama chenye kundi lenye nguvu kama TOT. Hata ndani ya CCM, vikundi vingi vya vijana vimejaribu mara kadhaa kuibuka lakini havikufika mbali.

Safari hii, mambo yamebadilika kabisa, badala ya vijana kuwa wasindikizaji wa wazee, sasa vijana wameamua wenyewe kushika bendera ya chama hicho. Katika sehemu kadha wa kadha, mwitikio wa vijana umewakosesha raha wazee hata kabla ya kipindi cha kampeni kuanza.

Idadi ya vijana waliochukua fomu kugombea Ubunge na Udiwani kwa tiketi ya CCM ni kubwa mno na kutakuwa na shughuli pevu wakati wa uteuzi.

Sambamba na hilo, ujio wa waziwazi wa wanafunzi wa Vyuo Vikuu katika harakati za uchaguzi mkuu wa mwaka huu, unaonyesha mabadiliko makubwa yatakayotokea wakati wa kampeni.

Katika mkutano mkuu wa CCM, vijana waliwafunika wazee kwa kila hali. Ukumbi ulikuwa ni wa shamrashamra zilizoongozwa na vijana.

Nyimbo pamoja na hotuba za vijana zilikuwa za mikiki mikiki. Wakati fulani ilionekana kwamba vijana wanataka kuimaliza enzi ya kikundi cha TOT ingawa waswahili walisema uzee ni dawa.

Pale vijana kwa mfano wa Vyuo Vikuu waliposimama kuimba wimbo wao, ukumbi mzima ulilipuka kwa shangwe na kujumuika katika kucheza wimbo huo unaokwenda kwa jina la NI KIKWETE.

Vijana kama Bushoke, Marlow, Flora Mbasha na Doki waliwafanya wajumbe wa mkutano mkuu kushindwa kuketi kwenye viti vyao. Katika kipindi cha burudani hizo, muda pekee wajumbe walipopata nafasi ya kupumzika, ni pale nyimbo za TOT zilipokuwa zikipigwa.

Ujio wa vijana katika kampeni hizi, unatufundisha jambo moja kwamba hali ya sasa ya siasa, ni sawa na jini aliyefunguliwa kwenye chupa. Uwezekano wa kumrudisha ni mgumu na kwa msingi huo, ni lazima tujifunze namna ya kuishi naye.

Mazingira ya zamani ya siasa za nchi zetu, yalikuwa yanatoa nafasi pana kwa viongozi waliomo madarakani kuwa walezi wa vijana wanaochipukia katika uongozi. Kwa sasa, hali hiyo haipo sana. Hivi karibuni, Chama Cha Mapinduzi kilikuwa na semina kule Iringa ambayo ilikuwa ikiwaandaa vijana wake. Hata hivyo, hayo siyo maandalizi ya kisiasa, yalikuwa maandalizi kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka huu.

Vyama vya upinzani navyo vinao vijana machachari waliokuwamo bungeni na wale waliomaliza shule. Kwa bahati mbaya, habari zao hazisikiki sana kama zinavyosikika zile za CCM na labda sababu kubwa ni ukosefu wa chombo cha kitaifa cha kuwaunganisha na kuwapatia mafunzo vijana. Baada ya siasa kupigwa marufuku katika shule na katika vyuo, vijana wanasiasa wanaokotwa barabarani au wale ambao waliasi amri ya kuzuia siasa katika taasisi za elimu. Kinachoshangaza ni kwamba hata wale vijana wanaochukua kozi za Political Science, hawana muda rasmi ulioruhusiwa kisheria na kitaratibu wa kufanya mazoezi kwa yale wanaotarajia kufanyia kazi.

Kwa nini vijana wanahitaji kuandaliwa? Kwanza kilichojitokeza kule Dodoma ni sababu tosha ya kuwafikirisha wazee na kuwaandaa vijana ili watambue nini cha kuongea, wakiongee lini na wapi.

Kwa mfano katika mkutano huo wa Dodoma, vijana wa Vyuo Vikuu walikaribishwa kusoma risala yao ambayo baadaye tulikuja kupata taarifa kwamba haikuwa imesomwa na yeyote. Yaani ilikuwa risala ya mashtukizi.

CCM ilikuwa imewaalika viongozi wa vyama vya upinzani. Walikuwapo Mwenyekiti Mrema, Mwenyekiti Lipumba na Mwenyekiti Dovutwa pamoja na wengine. Vijana katika hotuba yao, waliwageukia wageni hao ambao kimsingi walikuwa ni wageni wa mwenyekiti wa chama chao, wakasema: “Hawa Mavuvuzela, hawatuwezi”.

Kwa ujumla, maneno hayo yaliwaudhi viongozi wengi wa vyama hivyo. Mmojawao, Profesa Ibrahim Lipumba aliamua kuondoka kabla ya muda wake. Ilipofika muda wa Mwenyekiti kuongea, tofauti kati ya watu waliopata malezi ya kisiasa na wale ambao hawajapata malezi ya kisiasa ilijionyesha. Kikwete aliwakaribisha wageni wake, kuwasifia, kuwapa nafasi ya kuongea na kuwaomba uchaguzi wa mwaka huu uwe wa kistaarabu kwa sababu “tunajenga nyumba moja, hatuna sababu ya kugombania fito”. Hayo ni maneno yaliyosemwa na mtu aliyewakaribisha wageni nyumbani mwake. Mwenyeji, hatarajii watoto wake ‘wawachape fimbo’ wageni wake.

Mwanzo wa ngoma ni lele. Tunatarajia kuyaona mengi wakati wa uchaguzi.

No comments:

Post a Comment