Monday, July 26, 2010

UCHAGUZI CCM (TANZANIA) SI SHWARI

Imeandikwa na Martha Mtangoo, Dodoma; Tarehe: 25th July 2010 Habari Leo





WAKATI kukiwa na taarifa za kusimamishwa kwa Makatibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika baadhi ya wilaya nchini kutokana na kile kinachodaiwa kuegemea upande fulani wa wagombea na hata kujihusisha katika utoaji wa rushwa, Katibu Mkuu wa chama hicho, Yusuf Makamba amekuja juu na kusema hatambui jambo hilo.

Taarifa za kusimamishwa kwa makatibu hao zimekuja kutoka katika majimbo matatu ya Dodoma Mjini ambako Katibu wa CCM wilayani, David Mzuri ametajwa kusimamishwa kama ilivyo kwa Katibu wa Wilaya ya Bukombe, Mberito Magova na msaidizi wake, Novatus Kibati.

Hata hivyo, akizungumzia suala hilo jana Makamba alielezea kushangazwa kwake na taarifa za kusimamishwa kwa makatibu hao, akisema yeye kama mtendaji mkuu wa chama, atakuwa kichaa kama ataamua kuwafukuza Makatibu wa CCM wakati huu wa uchaguzi.

Alisema kuwa kinachofanywa sasa na chama chake ni kuimarisha usimamizi wakati wa uchaguzi wa kura za maoni.

“Ninyi mnazipata wapi habari za kuwa tunafukuza Makatibu wa CCM, mimi ndiye Katibu Mkuu wa chama hatuna sababu za kuanza kufukuzana, tunachofanya ni kuimarisha usimamizi wa zoezi hili, mfano Mikumi imekuwa wilaya mpya ambayo haina Katibu, sasa nikaona badala ya kumpeleka Msaidizi wa Mkuu wa Mkoa, nikaamua kumpeleka Nduta, na hata mzee Mzuri tumempeleka kusimamia Gairo,” alisema.

Lakini taarifa za awali ambazo gazeti hili ilizipata kupitia Mwandishi Martha Mtangoo aliyeko mjini Dodoma zinasema kwamba, tuhuma nzito za rushwa na upendeleo kwa baadhi ya wanachama wa CCM wanaowania kuteuliwa kugombea ubunge katika jimbo la Dodoma Mjini, zimemtia matatani Katibu wa Wilaya wa Chama hicho, David Mzuri na kwamba amesimamishwa kazi kuanzia jana.

Mzuri aliyekuwa pia Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Wilaya hiyo kwa CCM, ametajwa kufikwa na balaa hilo akituhumiwa ‘kumbeba’ waziwazi mmoja wa wagombea 18 wa jimbo hilo, Alhaji Adam Kimbisa.

Kimbisa, Meya wa Jiji la Dar es Salaam, ambaye pia ni Katibu wa Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania, ameibukia Dodoma Mjini kuusaka ubunge, dhamira ambayo haikuwa inafahamika na wengi mpaka alipochukua fomu.

Kusimamishwa kwa Mzuri kulithibitishwa jana na Katibu wa CCM wa Mkoa wa Dodoma, John Barongo, aliyesema baada ya kupokea malalamiko mengi juu ya Katibu wake wa Wilaya akihusishwa `kumbeba’ Kimbisa, uongozi wa Mkoa umeamua kumsimamisha kazi.

Alisisitiza, kusimamishwa kwake kutasaidia kufanyika kwa uchunguzi juu ya tuhuma hizo na kama itathibitika alitenda makosa ya kumsaidia Kimbisa, atafukuzwa.

Mzuri mwenyewe alipotakiwa kuzungumzia suala hilo, hakuwa tayari kwani aliwakimbia waandishi kwa kutumia gari binafsi.

Kabla ya uamuzi wa jana, mgombea huyo alikuwa anatuhumiwa yeye na familia yake kuwa walikuwa wakimpigia debe mmoja wa wagombea wenzake na hata kutoa rushwa.

Na baadaye haikuwa siri tena, kwani karibu wagombea wote walimtaja Kimbisa kuwa ndiye ‘anayebebwa’ na Katibu aliyesimamishwa.

Kimbisa alidai, anapikiwa majungu ya kisiasa kwa kuwa yeye ni tishio zaidi miongoni mwa wana-CCM waliojitokeza kuwania ubunge Dodoma Mjini.

Alikwenda mbali zaidi na kumtaja Haidary Gulamali ambaye pia ni mgombea kuwa ndiye anayeongoza timu ya kumchafua kisiasa na kwamba hakuna rushwa yoyote anayoitoa kwa wananchi kwenye mchakato huo.

“Hizi ni hisia za kisiasa tu ambazo zinasababishwa na baadhi ya watu ambao wananiogopa na kuna watu ambao wameitwa na Gulamali, ili kunichafua kisiasa, lakini haya si ya kweli,” alisema Kimbisa.

Kwa upande wake, Gulamali alisema akiwa Katibu wa Mkoa wa Uchumi na Fedha, alitumia cheo chake kufikisha ujumbe wa wagombea wengine waliotaka haki na usawa iwepo katika mchakato unaoendelea wa kuwania kuteuliwa na CCM.

“Kilichotokea, ni kwamba nilielezea tukio ambalo lilitokea ili kuhakikisha kuwa haki inatendeka, simwogopi mgombea yeyote na nipo tayari kuyakubali matokeo ambayo yatatolewa na wananchi,” alisema Gulamali.

Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani hapa, Eunice Mmari, alisema taasisi yake ina taarifa juu ya malalamiko hayo na kuwa bado iko katika uchunguzi.

Kutoka Bukombe mkoani Shinyanga, Raymond Mihayo anaripoti kuwa, wanachama 16 kati ya 18 wanaowania kuteuliwa kugombea ubunge kwa tiketi ya CCM katika majimbo ya Bukombe na Mbogwe mkoani Shinyanga, juzi na jana walisusia kufanya kampeni zao kwa madai kuwa, uongozi wa chama hicho wilayani Bukombe ulikuwa unawakumbatia baadhi ya wagombea.

Kutokana na hali hiyo, uongozi wa CCM mkoani humo umechukua hatua ya kuwasimamisha kazi Katibu wa CCM Wilaya ya Bukombe, Mberito Magova na msaidizi wake, Novatus Kibati.

Habari zilizopatikana jana kutoka wilayani humo na kuthibitishwa na Katibu wa CCM mkoani Shinyanga, Mohammed Mbonde.
Alisema kwamba, wagombea hao waliandika barua za kujiuzulu kutokana na kuwapo kwa dalili za upendeleo kwa baadhi ya wagombea.

Tayari nafasi ya Magova ya kusimamia jimbo la Bukombe imechukuliwa na Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) wilayani humo, Mathias Mbogo wakati katika jimbo la Mbogwe, nafasi ya Kibati imezibwa na Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilaya, Mgohoma Mgohoma.

Mchakato wa kampeni za ndani ya chama kupata wagombea wa udiwani na ubunge katika majimbo na kata mbalimbali nchini leo unaingia katika siku ya nne kati ya kumi zilizopongwa na chama hicho tawala.

Katika hatua nyingine, wagombea wawili wa udiwani kupitia Viti Maalumu ndani ya CCM, jana waliripotiwa kupoteza fahamu kutokana na kile kinachodaiwa kupata mshituko baada ya kuambulia kura sifuri licha ya wao wenyewe kujipigia kura katika mchakato wa udiwani katika Kata ya Hombolo.

Wagombea hao waliotajwa kuwa ni Alice Kitendya na Rosemary Kaka waliokuwa wanachuana na wengine saba, wameripotiwa kulazwa katika wadi namba 9 katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma. Kufikia jana jioni, walikuwa hawajarejewa na fahamu.

No comments:

Post a Comment