Tuesday, January 6, 2009

HAKI ZA BINADAMU - ULEVI WA MADARAKA

NA DIXON BUSAGAGA, MOSHI

KAMANDA wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani Kilimanjaro, Benetson Gobelabo, amemkamata na kumfungia pingu kwenye kasha la takataka kwa muda wa saa tano mpiga debe, Kennedy Shayo, kwa madai kuwa amekuwa akiwasumbua kwa muda mrefu.

Shayo, mkazi wa Manispaa ya Moshi alijikuta kwenye wakati huo mgumu wa kuvuta hewa chafu katika eneo hilo la takataka kwa muda wote aliofungiwa hapo.

Tukio hilo la aina yake, lilitokea majira ya saa 12:30 asubuhi jana katika kituo kikuu cha mabasi cha mjini Moshi, ambapo mtuhumiwa huyo alidai alikuwapo kituoni hapo kwa lengo la kuwasafirisha watoto wake kwenda shule nchini Kenya.

Akisimulia tukio hilo, Shayo alisema alikwenda kituoni hapo kwa lengo la kuwasafirisha watoto wake watano kwenda katika Shule ya Loktoktok nchini Kenya, ndipo Kamanda Gobelabo alipomkamata na kumfungia pingu kwenye kasha linalotumika kuhifadhia takataka kituoni hapo.

“RTO ameamua kunidhalilisha, kama mimi ni mtuhumiwa aliponikamata angenipeleka kituo cha polisi ambacho hakipo hata mita tano kutoka hapa, kwa nini ameamua kunifanyia hivi?” alihoji Shayo.

“Huu ni ukiukwaji wa haki za binadamu, ni sheria gani inayomuelekeza kunifunga pingu kwenye hili ‘dust bin? Ananifananisha na takataka, kwa hili sitakubali, tutapelekana mahakamani, hivi ni kama amenivua nguo mbele ya watoto wangu,” aliongeza Shayo.

Akielezea sababu ya kufanya kitendo hicho, Kamanda Gobelabo alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa kwa kosa la kupiga debe na ni kiongozi wa kundi la wapiga debe na wezi katika kituo hicho cha mabasi.

Alisema Novemba mwaka jana, kikosi chake kilianza operesheni maalumu ya kuwaondoa wapiga debe katika kituo hicho, lakini baadhi yao wamekuwa wakikaidi amri ya kuondoka, akiwemo mtuhumiwa huyo.

“Katika operesheni yetu tumefanikiwa kuwaondoa wafanyabiashara wadogo wadogo, lakini kwa wapiga debe, wale wenye akili timamu waliondoka, wale wakaidi ndio tunaopambana nao, akiwemo huyu Kennedy,” alisema.

“Huyu bwana amekuwa akitusumbua kwa muda mrefu, maana haondoki hapa stendi, huyu anasema mimi nakula sahani moja na R.T.O, tayari tumemkamata mara kadhaa na kumpiga faini, mara nyingine tumemfikisha mahakamani, kule nako ana haki zake, anarudi na sasa anaongoza kile kiwingu cha wapiga debe na kundi la wezi pale stendi,” aliongeza Gobelabo.

Akielezea zaidi juu ya Shayo, kamanda huyo alisema jina la mtuhumiwa huyo hivi karibuni liliingia kwenye kikao cha manispaa baada ya kamanda huyo kuulizwa endapo askari wake wamezidiwa nguvu na mtuhumiwa huyo katika zoezi la kuwaondoa wapiga debe kituoni hapo.

Alipoulizwa kuhusu kumfunga pingu kwenye kasha la takataka kwa muda wa saa tano pasipo kumpeleka kituoni, Gobelabo alisema mtuhumiwa amekuwa akiwakimbia mara kwa mara na kwamba amelidhalilisha Jeshi la Polisi, ndiyo maana aliamua kumfunga katika kasha hilo.

“Ametusumbua sana huyu bwana, kwanza ana kesi nyingi na yuko nje kwa dhamana, sasa nilipomkamata nikamfunga nikamwambia utakaa hapa mpaka tutakapomaliza kazi,” alisema Gobelabo.

“Yeye si anataka kukaa stendi, kwani nilimfungia wapi? Ingekuwa nimemfungia msikitini, shuleni ama kanisani hapo sawa, lakini yeye si anataka akae stendi, sasa si alikuwa stendi, alikuwa humo humo ndani ya stendi, ila kwa kumdhibiti,” aliongeza Gobelabo.

Aidha Kamanda Gobelabo alisema wataendelea na zoezi hilo la kuwaondoa wapiga debe katika kituo cha mabasi mjini hapa hadi jeshi hilo litakapohakikisha wapiga debe wanaondoka katika kituo hicho na kuongeza kuwa Shayo atashitakiwa kwa kosa la kupiga debe katika kituo cha mabasi.

CHANZO:- GAZETI LA TANZANIA DAIMA JUMATATU (JANUARI 05, 2009)

KUVUNJWA KWA HAKI ZA BINADAAMU ZA BW. KENNEDY SHAYO - MOSHI

Kwa kufungiwa pamoja na pipa la taka, Afande Benetson Gobelabo amemvunjia Bw. Kennedy Shayo haki zake za msingi kama ifuatavyo, kama zilivyoanishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977:

1. Ibara ya 12(2). Haki ya kustahili heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake. Kufungiwa na pipa la taka ni kumfananisha na mnyama.

2. Ibara ya 13 (4): Mafuruku ya kubaguliwa na mtu au mamlaka yeyote inayotekeleza madaraka yake chini ya sheria yoyote au katika utekelezaji wa kazi au shughuli yoyote ya mamlaka ya nchi. Benetson Gobelabo kwa kitendo hiki hakufuata, sheria hivyo amembagua Bw. Shayo kana kwamba sio mmoja wa wananchi wa nchi hii. Je amepata mamlaka haya toka sheria gani kumtweza binadamu mwenzie namna hii?

3. Ibara ya 13(1): Haki ya kuwa sawa na kila mtu mwingine mbele ya sheria, haki ya kulindwa na kupata haki yake sawa mbele ya sheria imekiukwa na Bw. Gobelabo.

4. Ibara ya 13 (3) (e): Haki ya bw. Shayo ya kutoteswa, kutoadhibiwa kinyama au kutopewa adhabu iliyomtweza na kumdhalilisha. (hasa katika hai hii ya kutofanya kosa lolote).

5.. Ibara ya 14. Haki ya kuishi; kwa sababu kwa kumfunga na kumlazimisha kuvuta hewa yenye sumu ya pipa la takataka amempunguzia umri wa kuishi Bw. Shayo na vile vile kumsababishia magonjwa mazito yanayoonekana na yanayoweza kumpata hivi sasa na yasiyonekana yanayoweza kumpata baadaye tokana na kuvuta hewa hiyo.

6. Ibara ya 15: Haki ya kuwa huru na kuishi kama mtu huru. Afande Gobelabo amevunja kabisa haki hii kwa kumfunga Shayo bila hatia wala kufuata taratibu zozote zile za kisheria.

7. Ibara ya 16(1): Bw. Shayo amevunjiwa haki yake ya kuheshimiwa na kupata hifadhi ya nafsi yake. Amekosa sana amani bwana huyu katika kufanyiwa kitendo hiki. Si hivyo tu; imekosa amani pia familia yake, amekosa heshima na hifadhi ya maskani yake na mawasiliano yake binafsi. Kwa kuwa amefungiwa pipani, familia yake imekosa amani, jamii iliyomzunguka inamwonaje, familia yake inajihisije kwa kitendo hiki, na mawasiliano yake na waliomzunguka yatakuwaje baada ya kitendo hiki cha kudhalilisha sana. Bw. Shayo amepatwa na msongo na mfadhaiko wa moyo hata kumfanya asiwe na uhuru wa kufikiria namna ya kujitafutia maendeleo yake. Kwa kulazimika kwenda mahakamani kudai haki yake, Afande Gobelabo atampunguzia muda wa Shayo wa kujitafutia riziki na maendeleo yake na ya familia yake.

8. Ibara ya 17(1): Uhuru wa kwenda kokote atakako. Kwa kufungiwa kwa saa hizo, hata ingekuwa kwa dakika moja tu, uhuru wa Shayo umekiukwa. Kama angetumia muda huo kupiga debe au vinginevyo kujitafutia riziki namna nyingine yoyote ile na kupata kipato halali kwa ajili ya maisha yake na ya familia yake.

9. Kanuni ya Asili ya Msingi wa Haki za Binadamu inayosema kuwa kesi ya nyani hawezi kupelekewa ngedere kwa kuwa wote ni wamoja na hivyo lazima kutakuwa na upendeleo tu. Kwa afande Gobelabo kuwa Mlalamikaji, polisi aliyemshika mtuhumiwa, kuwa mahakama na kumhukumu na mwishowe kutekeleza adhabu kama ndio Magereza, Bw. Shayo amekosewa haki yake ya msingi ya upatikanaji wa haki.

10. Kanuni ya Asili ya Msingi wa Haki za Binadamu inayosema ni wajibu kusikilizwa upande wa pili. Bw. Shayo hakupewa haki ya kusikilizwa upande wake ijulikane kama kweli amekosa au la.

Kwa ukiukwaji mkubwa sana wa haki za binadamu zilizoorodheshwa na zisizoorodheshwa (wachangiaji ongezeni nilizosahau), Bw. Shayo ana kila sababu na haki ya kufikisha lalamiko lake Mahakamani na kudai fidia ya Hela ya Madafu (Tshs.) atakayoamua kuidai kwa adha hii.

Mwatawala, Zainab M.
P O Box 453
Morogoro, Tanzania
East Africa
Tel. 255 023 260 3583
Cell: 202 427 4413
5167 Fulton Str. NW
Washington, DC., 20016
USA

No comments:

Post a Comment