FITINA, majungu na vitisho, sasa vinaonekana kuwachosha baadhi ya viongozi wastaafu wa serikali, ambao wamekuwa wakitajwa kuwa wanaweza kufikishwa mahakamani wakati wowote kwa makosa waliyoyafanya wakati wakiwa viongozi wa umma. Hali hiyo ilidhihirika jana, wakati Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Sinde Warioba, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Masaki, Dar es Salaam, na kueleza kuwa wanaotaka kumkamata wafanye hivyo haraka. Warioba ambaye aliwaita waandishi wa habari wa vyombo vitatu ofisini kwake kueleza kuchoshwa kwake na maneno ambayo yamekuwa yakisambazwa kuwa ni mmoja wa viongozi watakaofikishwa mahakamani kwa makosa ya kutumia ofisi za umma vibaya, aliwaeleza wana habari hao kuwa amechoshwa na maneno hayo ya uvumi na ameamua kueleza kile anachokijua kuhusu mambo anayotuhumiwa nayo. Alisema taarifa ambazo zimekuwa zikienezwa kwa kasi kwamba ataburuzwa mahakamani wakati wowote kwa tuhuma za kutafuna fedha za Mwananchi Gold Company si za kweli, na hata kama zina ukweli, yuko tayari kupandishwa kizimbani na kueleza ukweli wa kile anachokijua kuhusu kampuni hiyo. Akiongea taratibu, lakini kwa tahadhari, alisisitiza kuwa yuko tayari kukamatwa kwa sababu anaamini serikali ina nguvu ya kumkamata na yeye atajitetea mahakamani. “Nimewaita, lengo la kuwaita katika mkutano huu ni kueleza kwa mapana, Kampuni ya Mwananchi Gold Company Ltd, ilianzishwa na nani na kwa madhumumi gani. Hii ni kwa sababu kampuni hii imekuwa ikitizamwa vibaya na wananchi wakati ilianzishwa kwa ridhaa ya serikali. “Watanzania wengi wanaitizama kampuni hiyo kama ni ya kifisadi, wakati ukweli ni kwamba uamuzi wa kuanzishwa kwake ulikuwa wa serikali ambayo ilikuwa ikitekeleza sera yake ya kuwasaidia wachimbaji wadogo wadogo ili waweze kusafisha dhahabu zao hapa nchini na kuziuza kwa bei halali. “Ninasikitika kumekuwa na maneno mengi ya kupotosha kuhusu uanzishwaji wa kampuni hii na uamuzi wa serikali kulikalia kimya suala hili pasipo kueleza ukweli kuhusu kampuni hii, umenisikitisha zaidi,” alisema Jaji Warioba. Akizungumza kuhusu alivyoshiriki katika kuanzisha kampuni hiyo, alisema Kampuni ya uwakili ya Nyalali, Warioba & Mahalu, Law Associates, ambayo yeye ni mmoja wa mawakili wanaoimiliki, iliombwa na serikali kutoa huduma ya kisheria kusaidia kuundwa kwa kampuni hiyo. Alisema, kampuni yake ilifanya kazi hiyo kama ilivyoombwa na serikali na kuiwezesha kununua kiwanja cha ekari 30, kilichopo eneo la Vingunguti, jijini Dar es Salaam ambako kulifungwa mashine za kusafishia madini na ilizinduliwa rasmi na Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, Desemba mosi mwaka 2005. Jaji Warioba alisema, kampuni hiyo ilianza kufanya kazi kwa kununua dhahabu kutoka kwa wachimbaji wadogo wa wilayani Geita, lakini baadaye alishangazwa na uamuzi wa serikali wa kukataa kuendeleza mradi huo uliokuwa na tija kwa taifa. Alisema mradi uliokuwa ukiendeshwa na kampuni hiyo, ungeisaidia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuhifadhi dhahabu hapa nchini na ungeisaidia serikali kujua kiasi cha dhahabu kinachopatikana hapa nchini kuliko ilivyo hivi sasa ambapo dhahabu inachimbwa na kusafirishwa nje ya nchi kwa ajili ya kusafishwa, jambo linalosababisha taifa kushindwa kujua kiasi kinachochimbwa na mchimbaji. “Uamuzi wa kuanzishwa kwa Kampuni ya Mwananchi Gold ulitokana na nia njema ya serikali, serikali iliamuru BoT na Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) na Kampuni ya MA-CE ya Italia kuunda kampuni hiyo. Baada ya uamuzi huo, serikali ilikuja kwenye ofisi yetu ya uwakili ya Nyalali, Warioba & Mahalu Law Associates ili tuisaidie kuipatia huduma ya kisheria kabla na baada ya kuundwa kwa kampuni hiyo. “Mimi nashangaa tunakwenda kusafisha dhahabu nje ya nchi wakati kiwanda cha kisasa cha kusafishia madini yote kipo pale Vingunguti, tena kilianzishwa kwa uamuzi wa serikali. Lakini cha kustaajabisha, kwa sababu za kisiasa tu kiwanda hiki kinapigwa vita usiku na mchana, wanaharibu mradi huu kwa mambo ya kisiasa tu, kisha wanaanza kutafuta mchawi wakati mchawi ni wao. “Nasisitiza kwamba mradi huu ni wa serikali na serikali ndiyo ilikuja kwenye ofisi yetu kutuomba tuisaidie huduma ya kisheria ya kuanzisha Kampuni ya Mwananchi Gold Company Ltd na ikairuhusu BoT kuingia kwenye biashara hiyo kwa sababu taasisi hiyo ina fedha. Lakini sasa serikali imeishinikiza BoT ijitoe katika mradi huo na wiki tatu zilizopita BoT iliwasilisha rasmi kwenye bodi ya wakurugenzi wa Kampuni hiyo ya Mwananchi kwamba imejitoa na hivyo sasa imebaki NDC peke yake,” alisema Jaji Warioba kwa masikitiko. Aliwataja wanahisa wa Kampuni ya Mwananchi Trust, ambayo ipo ndani ya Mwananchi Gold Company Ltd kuwa ni Umoja Entertainment, VNB, WM Holding inayomilikiwa na Yusuph Mushi, na CCM Trust Company. Alisema katika Kampuni ya Mwananchi Trust, aliyekuwa na hisa nyingi ni Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilichokuwa na hisa 15. “Kwa hiyo, taarifa kwamba mimi nimetafuna fedha za mradi wa Mwananchi Gold Company Ltd si za kweli, sijatumia vibaya fedha za kampuni hiyo, kwani fedha zote tulizolipwa na BoT, ambayo ilitoa mkopo kwa mradi huo zipo kwenye maandishi na ushahidi upo wazi, ila nashangazwa sana, sijui kwa sababu za kisiasa mradi huu unapigwa vita,” alisema Jaji Warioba. |
No comments:
Post a Comment