Wandugu,
Hapa nawasimulia kama nilivyoyashuhudia maadhimisho haya ya kuapishwa Rais wa 44 wa Taifa la Wamarekani (USA) na Rais wa Kwanza Mweusi wa Taifa hili katika televisheni Bwana Barack Hussein Obama leo hii Januari 20, 2009 kuanzia mwendo wa saa tano na nusu hadi saa saba na nusu mchana.
1. Kilichonishangaza kuliko vyote ni kutokuona hata kwa mbali, kinyanya (bibi mzaa baba wa Barack Obama) kilichotoka kijijini Kogelo, Kisumu, Kenya katika Maadhimisho haya. Najiuliza picha nilizoziona zikimuonyesha anakwenda Nairobi kupanda ndege ili awasili USA Januari 17, 2009 kwa ajili ya maadhimisho haya labda hazikusema kweli. Huenda hakuhudhuria maadhimisho haya? Jibu hadi hapo kwa sasa sina. Nikifahamu ukweli wa jambo hili nitawaarifu.
2. Wimbo wa Taifa la Marekani umeimbwa mwishoni tu mwa maadhimisho sio mwanzoni (na mwishoni), kama vile tulivyozoea nchi za Afrika zinavyofanya.
3. Rais George W. Bush, alimkaribisha Rais Mteule Obama na mkewe White House kabla ya Maadhimisho. Ratiba yenyewe ya kina Obama ilikuwa hivi: Walianzia kwenda Kanisani na kutoka hapo Kanisani wakapelekwa Ikulu kupata kifungua kinywa na familia ya Bush. Kutoka Ikulu wote wakaelekea Bungeni (Capitol Hill) kulikondaliwa maadhimisho. Wamarekani wanasema sio kawaida ya Rais Mteule kualikwa na aliyekuwapo White House kabla ya kuapishwa. Kwa hiyo kwa hili, Bw. Bush kama vile ametaka kuonyesha dunia kuwa hana kinyongo na kiongozi ajaye.
4. Kwa kawaida ya utamaduni wao Marekani, Mara baada ya Watu wote waliopo White House kuelekea Jengo la Bunge, huku nyuma yanakuja malori kupakia mizigo ya rais aliyeachia madaraka kupakia kila kilicho chake na kukipeleka kwao; na wakati huo huo, kuingiza Ikulu kila kitu cha kiongozi aapishwaye atakayeingia Ikulu kunanzia baada ya kuapishwa.
5. Hivyo Bwana Bush na mkewe baada ya kuapishwa Rais Obama walipelekwa Uwanja wa Ndege kurejea kwao jimboni Texas na Bwana Obama walitangaza kuwa mara tu baada ya kuapishwa anaelekea kwenye ofisi yake Ikulu kuendelea na kazi kama kawaida. Kwake yeye ni vita mbele. Kazi yake ya Urais, hakuichelewesha hata dakika moja!
6. Umati mkubwa sana ulijaa katika viwanja vinavyosambaa umbali wa maili tatu kuanzia kwenye Lincoln Memorial hadi Capitol Hill; huku maarufu kwa jina na The Mall. Umati uliokadiriwa na waandishi wa Habari dakika za majeruhi kuwa ni watu waliokadiriwa kuwa laki tano.
7. Vazi alilovaa Bibi Michele Obama la rangi ya Dhahabu na vito vyake vyote; waandishi wa habari wamesema; aliyefanya kazi ya kuchora vazi hilo na kulitengeneza ni mzalendo wa hapa hapa USA.
8. Katika maadhimisho haya kulikuwa na Marais waliopita wote wanne walio hai kuanzia kwa Jimmy Carter na mkewe, George Bush baba mtu na mkewe, Bill Clinton na mkewe (ambaye ameteuliwa na Obama kuwa Waziri wa mambo ya Nchi za Nje; anachukua nafasi hiyo kutoka kwa Condoleeza Rice); George Walker Bush na mkewe. Baada ya kuapishwa, ukimjumlisha na Obama na Mkewe, kulikuwa na pea tano za Marais wa Marekani.
9. Mabinti wa Rais wa Marekani Sasha na Malia Obama waliingia sehemu ya Maadhimisho wakifuatana na bibi yao mzaa mama ambaye waandishi wa habari wameendelea pia kuelezea kuwa ataishi Ikulu na familia ya mwanawe Michele Obama. Katika maadhimisho hayo pia alionyeshwa kaka yake Michele Obama aliyekaa jirani na dada yake wakati wa kuapishwa.
10. Wenzetu huku, jambo la Kuapishwa linatekelezwa kama vile jambo la jukwaani na kweli lilifanyikia Jukwaani. Kwamba Mgeni mheshimiwa kabisa anakuwa wa mwisho kutoka. Hivyo "Mwali" Obama alikuwa akisubiriwa kwa hamu sana kuonekana na umati uliokusanyika kumshangilia. Na alipoonekana anatoka to mlangoni kuelekea Jukwaani alipopangiwa kuketi, vilisikika vishindo vya kelele za shangilizi ambazo waandishi wa habari hapa Marekani wamekiri kuwa hawajawahi kuvisikia. Hii ni kutokana na tekinolojia ya kileo. Katika huo uwanjwa walikojaa kadamnasi ya watu waliokuja kushuhudia tukio hili kuliwekwa televisheni kubwa uwanja mzima (The Mall) ili watu waone kinachoendelea japokuwa walikuwa mbali na Viwanja vyenyewe vya Bunge. Hivyo nao waliona mambo yakiendelea kama vile walikuwapo pale panapo maadhimisho. Ili mradi hata waliokwenda japo hawakushuhudia kwa macho yao, televisheni zilikuwapo kuwashuhudishaa tukio lile. Kama ambavyo wengi wetu tulioepuka adha ya makundi makubwa ya watu tulivyoamua kubaki nyumbani na kushuhudia tukio hili la kihistoria katika televisheni.
11. Kulikuwa na kwata ya Askari ambayo mimi kwa kweli sikuishuhudia, ambayo ilifanyika baada ya kuapishwa kwa Rais lakini nimeikosa sana kwa sababu napenda sana kuangalia jinsi askari wanavyotembea kwa mpangilio maalum. Kwa hiyo huku hakuna utaratibu wa Vikosi mbalimbali vya Majeshi ya Ulinzi na Usalama kutoa heshima au kitu kama hicho kabla ya maadhimisho. Hayo yanakuja baadaye kama sehemu ya kustarehesha wananchi.
Zainab,
ReplyDeleteUmeripoti sawa sawa mtiririko wa mambo katika tukio hili litakaloingia katika historia.
Siku njema!