Monday, January 12, 2009

"SANDWICH FAMILIES"

Wandugu mlioko nyumbani Afrika,
Huku Washington DC, na maeneo mengi tu ya nchi za Magharibi kwa ujumla wao, wanaita familia zenye kulea wazazi wao kuwa ni "SANDWICH FAMILIES". Wametumia msamiati huu kutokana na mfano wa "sandwich". Sandwich ni chakula kama vipande viwili vya mkate kisha katikati yake kuna kitu kingine kama vile mayai, mboga, nyama, jibini, n.k.

Kwa hiyo kwa huku Marekani, baba na mama, wanajihesabu kama wako katikati. Watoto wako chini na wazazi wao wako juu. Hivyo hawa baba na mama wanakuwa na kazi ya ulezi wa kizazi kilichopita na kizazi kinachowafuata wao. Ndio wababu wakaitumia hili neno "sandwich" kwa maana hii.

Takwimu zao zinasema kuwa kuna familia kama hizi milioni 15 U.S.A pekee. kwa hiyo kwa wenzetu hawa jambo hili linaonekana kama kitanzi kwao. Kwamba, wanashindwa kugawa mapenzi ipasavyo kwa watoto wao wakiwa na wazazi wao. Nilipoulizauliza, nikaambiwa kuwa hapo zamani, kama vile kabla ya vita kuu ya Pili, mambo yalikuwa tofauti, na wazazi kama wa kwetu Afrika, walikuwa wakilelewa na watoto wao na ilikuwa ni jambo la kawaida. Lakini sasa maendeleo yamepiga hatua, hivyo wameona bora wazazi wao wawatenge kwa kuwatengenezea makazi ya wazee.

Huko, wanakuita wenye "Assisted Living Residence", yaani nyumba za kuishi watu wanaohudumiwa. Mzee awe mgonjwa au mzima, ili mradi tu akifikia hatua ya kuhitaji msaada wa kuishi mathalani kusaidiwa kula na haja zingine, basi huyo anastahili kufikishwa akalelewe huko.

Kwa wale wazee ambao ni wagonjwa wasiotarajia kupona, au ugonjwa wowote ambao umeshatibiwa na dakitari, lakini unahitaji uangalizi wa karibu bila ya kulazwa hospitali, wao nao wana makazi yao wanaita "Nursing Homes" ambako kuna Wahudumu maalum waliosomea jinsi ya kuishi na kuwalea vikongwe hawa.

Kwa Vikongwe wengine wenye uwezo wa kifedha, huweza kukodi huduma za Walezi, basi hawa hubakia majumbani mwao (hasa wale wasiokuwa na watoto wala ndugu wa karibu) na kulipia gharama za kutunzwa na Wahudumu zinazopishana kulingana na uzito wa ulezi unaohitajiwa. Kikongwe kama hana usumbufu anaweza akatozwa kati ya dola 150 hadi dola 200 ($150 - 200) kwa siku. Na kwa kikongwe anayehitaji huduma saa 24 kutegemea na mahitaji yake, inaweza kufika hata zaidi ya hapo.

Kwa hiyo kwa wenzetu huku, Maendeleo yamewafanya waone kuwa kulea wazee wao ni mzigo ambao wako tayari kulipia gharama akalelewe na wahudumu nje ya mazingira ya nyumba zao. Kwa wale wanaoamua kubanana hapo hapo na wazee wao na kuwalea hadi mwisho wao; kama vile jinsi mke wa Rais mtarajiwa wa Marekani Bibi Michelle Obama (anayeishi na mama yake mzazi), ndio hizo "sandwich families". Jamani tutahadharini na haya maendeleo. Sijui mitikasi hii ikitufika sisi Wa-Afrika itakuwaje?

Huku Washington DC ni jambo kubwa linalozungumzwa na kuandikwa sana tu kuwa he! Jamani, Ikulu anaingia mama Mkwe wake Barack Obama! Kana kwamba hiki ni kioja. Kumbe ni kitendo cha kuwasifia watoto hawa ambao wameamua kuishi na wazee wao kwa shida na raha. Mimi naona bibi yao kina Sasha na Malia Obama atakuwa Nguzo kamili ya kuweza kusaidia ulezi wa wajukuu hawa hasa katika kipindi hiki cha miaka minne ya Mheshimiwa na Mkewe kuwa katika mihangaiko ya kuongoza nchi kubwa kama hii ya USA.

No comments:

Post a Comment