Saturday, January 31, 2009

To:
list@tanzanet.org

Mwandishi Wetu
Daily News; Saturday,January 31, 2009 @21:15

Serikali imeahirisha ununuzi wa magari yake mwaka huu na badala yake itanunua matrekta kwa nia ya kuimarisha kilimo nchini. Sambamba na hilo, imezuia rasmi semina, warsha, makongamano na mikutano isiyo ya lazima ili fedha za shughuli hizo zitumike kununua matrekta hayo.

Nia ni kutaka kuongeza idadi ya matrekta yaliyonunuliwa na halmashauri na yanayoletwa na sekta binafsi lakini pia kununulia pembejeo muhimu za kilimo na ufugaji. Hayo yalisemwa jana na Rais Jakaya Kikwete katika hotuba yake ya kila mwisho wa mwezi kwa taifa kwa mujibu wa utaratibu aliojiwekea ambapo alisema magari yatakayonunuliwa ni yale ya muhimu tu.

"Lengo letu ni kuona wakulima wetu wengi zaidi wanatumia matrekta, hivyo kutoa fursa ya kupanua ukubwa wa mashamba yao na kuongeza tija. Pia kuona mimea na mifugo yetu inahudumiwa vizuri zaidi," alisema Rais ambaye yuko Addis Ababa, Ethiopia, kuhudhuria mkutano wa Umoja wa Afrika (AU).

Alisema utaratibu mzima wa usambazaji na ugavi wa matreka hayo na pembejeo, utatolewa baadaye na serikali wakati wake ukifika. Hata hivyo muda ukifika alisema, matrekta hayo yatauzwa kwa vikundi vya wakulima kupitia vyama vyao vya kuweka na kukopa (SACCOS) au vyama vya ushirika. "Hii ni hatua ya mwanzo tu.

Kuanzia mwakani tutatenga fungu maalumu katika bajeti la kununua matrekta kwa ajili ya wakulima wetu," aliongeza. Katika kuongeza kasi ya utekelezaji wa mipango ya kuleta usasa katika kilimo, alisema tayari kuna mipango ya kurahisisha upatikanaji wa mbolea, mbegu bora na dawa za mimea na mifugo; huduma za ugani, kuimarisha miundombinu ya umwagiliaji maji na kuhakikisha masoko na bei nzuri kwa mazao ya mkulima na mfugaji.

"Tunapenda kuona kilimo chetu kinabadilika; tunajitosheleza kwa chakula na maisha ya wakulima wetu nayo yanabadilika na kuboreka. Naamini haya yanawezekana kabisa, iwapo tutafanikiwa kuyafanya haya na mengine tuliyoanza kuyafanya," alisema. Alisisitiza kuwa kwa taifa kama Tanzania linalotegemea kilimo, hapana budi kuongeza matumizi ya matrekta na matumizi ya wanyama-kazi kulimia badala ya kuendelea kutumia jembe la mkono.

Alisema serikali imekuwa inachukua hatua kadhaa za kuhimiza uingizaji wa matrekta nchini. Miongoni mwa hatua hizo ni kufuta ushuru wa forodha na kodi za ongezeko la thamani kwa matrekta, plau kutoka nje ya nchi. Pia, baadhi ya halmashauri za wilaya nchini zimetumia sehemu ya pesa za ASDP kununua matrekta na kuyauza kwa vikundi vya wakulima na hata mkulima mmojammoja.

"Lakini, ukweli ni kwamba kiasi cha matrekta yanayoingizwa nchini bado ni kidogo sana. Idadi hiyo haifanani na nchi ambayo kilimo ndio uti wa mgongo wa uchumi wake, na asilimia 80 ya watu wake wanaishi vijijini wakitegemea kilimo. Hali hii haikubaliki na lazima ibadilike," alisema.

Kuhusu Umoja wa Afrika (AU) Rais Kikwete aliwashukuru viongozi wenzake wa nchi wanachama kwa heshima kubwa waliyoipa Tanzania kupitia kwake na kwamba anapata faraja kubwa, kuona kuwa imeitumikia vyema AU na kuna mafanikio mbalimbali yaliyopatikana katika kipindi cha uongozi wa Tanzania.

"Lakini, pia yapo mambo kadhaa ambayo hatukuweza kuyamalizia ambayo tunamwachia kiongozi ajaye kuyashughulikia ... pengine jambo la faraja kubwa kwangu wakati huu ninapomaliza kipindi changu cha uongozi, ni ajenda ya msingi ya kikao chetu cha safari hii," alisema.

Alisema aliwaomba wenzake na wakamkubalia, kuwa katika kikao hiki wazungumzie suala zima la kuendeleza miundombinu barani Afrika. "Nilifanya hivyo kwa kutambua kuwa Umoja wa Mataifa ya Afrika tunaoutaka, utafanikiwa na kustawi tu pale nchi zetu zitakapokuwa zimeunganishwa kwa njia za uhakika za usafiri na usafirishaji, yaani barabara, reli na usafiri wa anga na majini. Nafurahi hiyo ndiyo ajenda yetu kuu," alisema.

Kuhusu mvua, Rais alisema hali ya upatikanaji wa mvua nchini inazidi kutia mashaka, kwani taarifa za mikoa yenye upungufu wa mvua zinaongezeka, hasa ukanda wa kati na kuashiria kwamba huenda kukawa na tatizo kubwa zaidi la upungufu wa chakula katika baadhi ya mikoa mwaka huu. "Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika wanaendelea na tathmini ya kina ya hali ya upatikanaji wa chakula nchini ilivyo sasa. Taarifa yao itatupa sura kamili ya hali ilivyo na hatua za kuchukua kukabiliana na tatizo. Naomba wananchi msiwe na hofu, tutalikabili tatizo hili kwa ukamilifu," aliasa.


No comments:

Post a Comment