Na Eckland Mwaffisi, 26 Januari, 2009
*Waandaa kampeni ya kitaifa kutoa elimu nchi nzima *Milioni 300 zinahitajika kufanikisha mpango huo Na Eckland Mwaffisi KATIKA siku za hivi karibuni, kumezuka mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino), yanayotokana na shinikizo la imani za kishirikina kwa lengo la kutaka utajiri wa haraka kupitia viungo vya watu wasiokuwa na hatia. Kufuatia hali hiyo, Serikali na wadau wengine hususan taasisi za haki za binadamu, zimekuwa zikilaani mauaji hayo pamoja na kuendesha kampeni mbalimbali zenye lengo la kutoa elimu kwa jamii ili kuhamasisha vita dhidi ya ukatili wa mauaji ya albino nchini. Kwa kutambua uzito wa suala hilo, Kampuni ya Follywood kwa kushirikiana na Chama cha Maalbino Tanzania (CCMT), wameandaa mkakati wa kitaifa wa kutoa elimu kwa jamii na kupinga ukatili na mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi 'albino', kwa njia ya sanaa, michezo na burudani. Mkakati huo, utahusisha mikoa yote ya Tanzania katika kipindi cha miezi 10 na siku 15 sawa na siku 315 ambapo uzinduzi wake, utafanyika Dar es Salaam Machi 27 mwaka huu na mgeni rasmi, anatazamiwa kuwa Rais Jakaya Kikwete. Akizungumza na gazeti hili, Mratibu wa kampeni hiyo Bw. Ahmad Mwita, anasema kiasi cha sh. milioni 300 zinahitajika kufanikisha kampeni hiyo ambayo itahusisha viongozi mbalimbali wa mikoa, wilaya na wadau wengine katika mikoa husika. Anasema uratibu wa kampeni hiyo, utafanyia kwa njia ya sanaa, michezo na burudani na umepangwa kufanyika kwa awamu tatu tofauti ambapo awamu ya kwanza inatarajiwa kuanza Machi 29 mpaka Mei 5 mwaka huu. Awamu ya kwanza ya kampeni hiyo, itahusisha mikoa ya Shinyanga, Mwanza, Mara, Kagera, Kigoma, Morogoro, Rukwa na Mbeya. Awamu ya pili Tabora, Iringa, Ruvuma, Lindi, Mtwara, Pwani na Dar es Salaam ambapo awamu ya tatu ni Dodoma, Singida, Manyara, Arusha, Kilimanjaro na Tanga. "Kampeni hii, itakwenda sambamba na maandalizi ya filamu ya mauaji ya albino ambapo washiriki wa kampeni hizo, watapata fulsa ya kupiga kura za siri ili kuwataja watu wanaojihusisha na uhalifu huu pamoja na kukusanya mawazo yao juu ya sababu zinazosababisha mauaji hayo," anasema Bw. Mwita. Anasema pamoja na mkakati mzuri walionayo katika kufanikisha kampeni hiyo, changamoto waliyonayo kwa sasa ni ukosefu wa wadhamini watakaofanikisha kampeni hiyo. Anasema tokea kuanza kwa mauaji hayo, zaidi ya albino 45 wamepoteza maisha yao na wengine zaidi ya nane, wamepoteza viungo mbalimbali vya miili yao ambapo zaidi ya watoto 300, wanakosa haki ya msingi ya kupata elimu ya awali, msingi na sekondari. Katika siku za hivi karibuni, Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, ilisema zaidi ya watu 100 wanaotuhumiwa kuhusika na mauaji hayo, wamekmatwa na mashauri yao yapo katika hatua mbalimbali za kushughulikiwa kisheria. Akizungumzia aina ya uharifu huo dhidi ya watu wasiokuwa na hatia, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Bw. Laurence Masha, anasema Taifa linapata aibu kutokana na uharifu huo unaotokana na imani potofu zilizojengeka katika jamii. Anasema mauaji hayo, yameishitua Serikali ambayo imeandaa mkakati kabambe wa kuhakikisha kuwa, wahusika wa vitendo hivyo wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria. Bw. Masha anasema, tayari Wizaya yake imeziagiza Kamati za Ulinzi na Usalama katika ngazi zote za Mikoa, Wilaya, Tarafa, Kata na Vijiji, kuunda mkakati wa pamoja ili kupambana na uhalifu huo unaofanywa na watu wachache wasiozingatia misingi ya haki za binadamu. Kufanikiwa kwa kampeni hiyo, kutachochea ari na hamasa miongoni mwa Watanzania katika harakati za kutokomeza mauaji hayo na kuleta mabadiliko ya kweli miongoni mwa jamii husika. Bw. Mwita anasema, kampeni hiyo itabeba ujumbe unaosema 'Ni Mwenzetu', pamoja na kutoa elimu kwa njia ya vijarada, hotuba za viongozi wa Serikali, mikoa na vyama vya albino katika mikoa husika. Anasema kushamili kwa mauaji hayo nchini, kunaifanya jamii ya maalbino, kushindwa kushiriki katika shughuli mbalimbali za maendeleo, haki ya kuishi na kupata elimu hivyo kampeni hiyo, itawaletea mafanikio makubwa endapo itafanikiwa kwa malengo yaliyokusudiwa. Katibu wa (CCMT) Bi. Ziada Nsembo, anasema katika uzinduzi wa kampeni hiyo, Rais Kikwete atawasha tochi itayoangaza kwa kila mwananchi pamoja na kuifikisha katika vikao vya Bunge ili kuipa uzito kampeni hiyo. Anasema mauaji ya albino, yanamgusa kila mwanajamii ambapo mkakati huo ni utekelezwaji wa sera ya chama hicho katika kupiga vita vitendo vya ukatili wa mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi wasiokuwa na hatia kwa shinikizo la imani za kishirikina. "Kilio hiki ni cha taifa zima, chama kama chama bila kuungwa mkono na jamii pamoja na wadau wengine, hatuwezi kufikia malengo yanayokusudiwa ikiwa mategemeo yetu baada ya kampeni hiii ni kuona mabadiliko yaliyotokana na elimu tuliyoitoa kwa jamii pamoja na kufanya tathimini ya kile tulichokifanya," anasema Bi. Nsembo. Anasema kampeni hiyo, itaendesha semina katika kila mkoa kwa viongozi wa Vyama vya Maalbino katika mikoa husika na kuwapa jukumu la kuendeleza elimu hiyo kwa lengo la kukomesha mauaji hayo. Anasema katika siku za hivi karibuni, mauaji hayo yameonekana kushamili mkoani Kagera pasipo wahalifu wa mauaji hayo, kutotambua kuwa albino ni sehemu ya Watanzania hivyo wana haki sawa na binadamu wengine. Anasema vyombo vya habari, vimefanya kazi kubwa ya kufichua uhalifu huo na kufafanua kuwa, ni vyema taarifa zinazohusiana na mauaji hayo, zisilenge kuhamasisha biashara hiyo kwa kutaja kiasi cha fedha ambacho wahusika wa mauaji hayo, wanakipata kutokana na viungo vya albino. Kampeni hiyo inasimamiwa na CCMT na kuratibiwa na Follywood kwa lengo la kufanikisha mchakato wa kampeni hiyo kwa malengo yanayokusudiwa. Maonesho yote yatakayohusihwa katika kapeni hiyo yatafanyika bure ili kutoa nafasi kwa jamii kubwa, hushiriki na kutoa maoni yao kwa lengo la kukomesha mauaji hayo.
No comments:
Post a Comment