Monday, January 26, 2009

WANAKIJIJI WALIOELIMIKA KUHUSU MALIASILI

Frank Leonard, IringaDaily News; Sunday,January 25, 2009 @21:15
Asasi ya Matumizi Bora ya Malihai Idodi na Pawaga (MBOMIPA), imekataa kuingia mkataba wa uwekezaji na Kampuni ya Tandala Tented Camp and Safaris iliyokuwa inataka kuwekeza katika eneo lake lenye ukubwa wa kilomita za mraba 73. Hatua hiyo imekuja baada ya Wakili wa kampuni hiyo, Basil Mkwata kutaka vipengele kadhaa vilivyopo katika mkataba ulioandaliwa na Mbomipa kwa msaada wa Shirika la Misaada la Marekani (USAID) kwa kupitia asasi ya Wildlife Conservation Society (WCS), vifanyiwe marekebisho au kuondolewa kabisa. Kipengele kilichoombwa kuondolewa ni cha Dhamana ya Utekelezaji ambayo thamani yake ilielezwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Mbomipa, Juma Kaundama kwamba ni Sh milioni 10 na kingine kilichotakiwa kufanyiwa marekebisho ni kile kinachohusu usuluhishi wa migogoro ambacho walitaka mahakama ndiyo itumike badala ya wasuluhishi na vikao vilivyopendekezwa katika mkataba. Hafla ya kutiliana saini makubaliano ya mkataba huo ilikuwa ifanyike Ijumaa iliyopita katika Kijiji cha Nzihi baina ya Bodi ya Mbomipa na Menejimenti ya kampuni hiyo mbele ya wawakilishi wa vijiji 21 vinavyounda asasi hiyo. Vijiji 21 vya Tarafa ya Idodi na Pawaga zilizoko Iringa Vijiji vinamiliki eneo la Hifadhi la Jumuiya ya Pawaga-Idodi (PI-WMA) lililoko Kusini mwa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha na ambalo kwa upande wa Kaskazini kuna fukwe za mto Ruaha Mkuu. Pamoja na kuhifadhi wanyamapori wanaofurika kutoka Hifadhi ya Taifa ya Ruaha eneo hilo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 776, lina rasilimali ya wanyamapori ya hali ya juu na mandhari ya kuvutia kiasi cha kuifanya PI-WMA kuwa moja ya maeneo ya Tanzania yanayovutia. Tembo, nyati, simba, chui, duma, mbwa mwitu na tamaduni nyingi katika vijiji vinavyozunguka eneo hilo na mambo ya kale yaliyoko ndani ya eneo hilo ni vivutio vikubwa kwa ajili ya utalii wa wanyamapori, utamaduni na mambo ya kale. Wawekezaji wengine walioingia mkataba na Mbomipa katika eneo hilo ni Kampuni ya Malela Safaris iliyopewa kilomita za mraba 169 mwaka 2007 kwa ajili ya uwindaji, na Kilombero North Safaris waliopewa kilomita za mraba nne ndani ya eneo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 420 kwa ajili ya kujenga hoteli ya kitalii. Kukataliwa kwa Tandala Tented Camp and Safaris kumekuja baada ya Mkurugenzi wake Mkuu, John Fliakos katika vikao vya awali kudaiwa kwamba alikubali kutoa Sh milioni 10 kama dhamana ya utekelezaji, lakini juzi alikataa na hivyo kufanya hoja hiyo iwe na mjadala mkubwa na matumizi ya lugha kali. Kauli hizo ikiwamo ya mwekezaji huyo, ilichochea hasira kutoka kwa wanachama wa Mbomipa na ndipo Mwenyekiti wake, Leonard Chengula aliposimama na kutangaza kuvunjika rasmi kwa makubaliano yaliyokuwa yafikiwe na mwekezaji.

No comments:

Post a Comment