Monday, January 26, 2009

MKAPA AJUTIA UWEKEZAJI KUGEUKA UGENISHAJI

Na. Mwandishi Maalum - 26 Januari, 2009.
RAIS mstaafu, Benjamin Mkapa, amesema anajutia kitendo chake cha kuliingiza taifa katika ubinafsishaji wa rasilimali bila ya kujiandaa kikamilifu na mabadiliko hayo.
Mkapa alitoa majuto hayo katika mkutano ulioandaliwa na Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) uliofanyika Zanzibar wiki iliyopita katika Hoteli ya Zamani Kempinski na kuhudhuriwa na aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki.
Mbali ya Mbeki, viongozi wengine waliohudhuria mkutano huo ni Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Pius Msekwa na mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale - Mwiru.
Mmoja ya wajumbe waliohudhuria mkutano huo ambaye alizungumza na Tanzania Daima Jumapili kwa sharti la kutokutajwa jina lake, alisema Mkapa alikiri kuwa sera ya ubinafsishaji haijamsaidia kwa kiwango kilichotarajiwa Mtanzania na badala yake wamegeuka wageni katika rasilimali zao.
Chanzo hicho kilidokeza kuwa Mkapa alibainisha kuwa kukubali kwake sera hiyo kulikuwa na lengo zuri la kuwafanya Watanzania waondokane na lindi la umaskini kupitia uwekezaji utakaofanywa katika rasilimali zao.
“Alituambia sera ya ubinafsishaji inamuumiza mno, kwani alipoikubali hakutarajia kama ingeweza kuwafanya wageni wawe na sauti katika rasilimali za taifa kuliko wazawa kama ilivyo sasa,” kilisema chanzo hicho.
Chanzo hicho kilibainisha kuwa Mkapa alifikia hatua ya kudai kuwa kama angepata nafasi ya kuwa kiongozi tena wa taifa hili angerekebisha sera ya ubinafsishaji haraka ili walau Watanzania waanze kufaidi rasilimali za nchi yao, badala ya kuwa mashuhuda wa wageni wanaoendelea kuneemeka na rasilimali za nchi.
Alisema tatizo kubwa lililopo katika nchi za Afrika ni kutumia baadhi ya mambo wanayotakiwa kuyafanya na wafadhili au mifuko ya fedha, bila kuyafanyia tathmini ya kina ili kujua kama hayataleta madhara katika siku za usoni.
“Mkapa alionyesha kujutia uamuzi alioufanya kwenye uwekezaji na aliweka wazi kuwa kama angeruhusiwa kurudi katika nafasi hiyo, basi jambo la kwanza kulirekebisha ni ubinafsishaji,” kilisema chanzo hicho.
Mkapa katika utawala wake alibinafsisha mashirika mengi ya umma, ikiwemo Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) kwa bei ya chini, kitendo ambacho kilizua malalamiko mengi kutoka kwa wananchi, pia alibinafsisha Shirika la Ndege Tanzania (ATC) na mengine mengi, kiasi cha kuzua malalamiko mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Aidha, katika utawala wake pia alilalamikiwa kwa kuwapendelea wawekezaji wa kigeni kuliko wazalendo, hasa katika sekta ya madini na kuingia mikataba mibovu ambayo hadi sasa imekuwa mzigo mkubwa kwa taifa, sambamba na wawekezaji hao kupata misamaha ya kodi kwa kigezo cha kuwavutia.
Kuingia mikataba mibovu huku ndiko kulikomfanya Rais Jakaya Kikwete kuunda kamati ya kupitia mikataba ya madini na kutoa ushauri wa namna bora ya kushughulikia sekta hiyo.
Majuto hayo ya Mkapa yanakuja huku kukiwa na shinikizo kubwa kutoka kwa baadhi ya wabunge na wananchi wakitaka afutiwe kinga yake ili aweze kushitakiwa kwa matumizi mabaya ya madaraka yake akiwa ikulu.
Katika utawala wake, Mkapa anadaiwa kutumia madaraka yake kuanzisha miradi mbalimbali inayomhusu, ama kwa kupitia familia yake au ndugu zake, ukiwemo ule wa makaa ya mawe wa Kiwira, ambao hivi karibuni wamiliki wake wametajwa hadharani kwa mara ya kwanza.
Chagizo la kutaka kutolewa kinga limezidi kupata kasi baada ya waliokuwa mawaziri wake, Basil Mramba (Fedha) na Daniel Yona (Nishati na Madini) na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Uchumi, Gray Mgonja, kufikishwa mahakamani kwa kosa la kulisababishia taifa hasara ya sh bilioni 11 kwa kutoa msamaha wa kodi kwa Kampuni ya M/S Stewart.
Kinga ya Mkapa inaweza kuondolewa kama Bunge litapiga kura ya kutaka kutengua kinga hiyo, lakini ni lazima hoja hiyo iungwe mkono na theluthi mbili ya wabunge wote.

Source: http://freemedia.com

No comments:

Post a Comment