Tuesday, September 11, 2012

TAMKO LA COMNETA TANZANIA

 Limeingizwa hapa tarehe 11/9/2012.

Inashangaza kwamba TAMKO hili la kutoka kwa Mwenyekiti wa Mtandao wa COMNETA linashindwa kuwa sahihi kwa kutoweka tarehe aliyofia marehemu Daudi Mwangosi wala kuweka jina lake kamilifu!  Wapi misingi ya  5 Ws & 1 H? (Who, where, what, when, why and How?).  Aren't these principles getting taught in Journalism schools any more?
 
 
Ndugu wana COMNETA,
Kufuatia matukio mbali mbali ambapo waandishi wa habari wamesakamwa, kushurutiwa, kupigwa na wengine kuuliwa, kwa sasa Jeshi la Polisi nchini haliwezi kukwepa lawama kutokana kifo cha mwandishi wa habari Mwangosi.
Kwa niaba ya Mtandao wa Vyombo Vya habari vya Kijamii (COMNETA), ninaungana na waandishi wa habari wote nchini kulaani mauaji hayo na kwamba polisi wanapaswa kubeba lawama na si Chadema na kwamba lazima Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sasa akubali kuwa, wanaofanya hivyo, wanayo nia ya kuchafua jina na heshima ya Taifa letu ambalo linasifika kama kisiwa cha amani.
Taarifa zilitolewa na vyombo vya habari pamoja na kunukuu polisi ni kuwa mwandishi huyo aliuawa kwa mlipuko akiwa mikononi mwa Jeshi la Polisi hadi kusababisha askari polisi waliokuwa karibu naye kujeruhiwa na mwingine kukimbizwa hospitali.
Vurugu za kisiasa kati ya wafuasi wa vyama vya upinzani hasa Chadema na Jeshi la Polisi si la kwanza ukiacha lililotokea mkoani Arusha la kuuawa kwa watu watatu na tukio lingine la Agosti 27, mwaka huu mkoani Morogoro ambapo muuza magazeti, Ali Nzona anadaiwa kuuawa katika vurugu. Katika tukio la Morogoro polisi walidai Nzona alifariki kwa kupigwa na kitu kizito kichwani wakati Chadema wanasema ameuawa baada ya kupigwa risasi.

COMNETA tunaungana na waandishi na wafanyakazi katika tasnia ya habari nchini pamoja na Jumuiya ya Klabu za Waandishi nchini (UTPC) kulaani kwa nguvu zote matumizi ya mabavu ya polisi ambayo yamesababisha kifo cha mwandishi wa habari akiwa kazini na pia akiwa chini ya ulinzi wa Polisi.
Huu ni mwendelezo wa matumizi ya nguvu kupita kiasi yanayofanywa na baadhi katika jeshi la polisi kwa raia wa nchi hii. Ni lini polisi watasimamia ulinzi wa raia na mali zao badala ya kugeuka kuwa jeshi la mauaji kila wananchi wanapokusanyika kwa minajili ya kutimiza ndoto zao?
Kumekuwepo na mwenendo wa jeshi la polisi kutumia nguvu bila sababu maalum tangia kipindi cha uchaguzi kilichopita mwaka 2010. Utumiaji wa nguvu kupita kiasi ikiwemo kurusha mabomu ya machozi, kutumia risasi baridi na za moto kumeongezeka huku kukiripotiwa matukio kama hayo karibu kila upande mwa nchi hii. Mwaka 2010 mabomu ya machozi yalingurumishwa katika maeneo mengi kuwatawanya wananchi waliokuwa wamemaliza kupiga kura, na walisubiri matokeo yaliyokuwa yamecheleweshwa bila sababu maalum!
Kufanya hivyo kumegeuza nchi yetu iliyosifika kama kisiwa cha amani, kuwa nchi ya umwagaji wa damu vitendo hivi vikifanywa na jeshi la polisi ambalo jukumu lake kubwa ni kulinda usalama wa raia. Matukio ambapo jeshi la polisi limehusika moja kwa moja yanabatilisha dhana ya polisi ya jamii na kuharibu mahusiano kati ya raia na jeshi hilo. Zipo sababau kaadha za kulifanya jeshi la polisi liachwe kuitwa jeshi la kulinda usalama wa raia bali jeshi la kuhatarisha usalama wa raia.
Hii itazidisha chuki ya wananchi dhidi ya serikali yao kuliko kipindi kinginecho chote. Nimatumaini yangu kuwa wanajeshi la polisi waliohusika moja kwa moja wanapaswa kuadhibiwa kama walivyowafanyia wenzao, ili haki itimie.
Hata hivyo, sijui kama ni jukumu la jeshi la polisi kutoa vibari kwa wananchi wakitaka kufanya mikutano? Huenda ni suala la kikatiba kuwa jeshi la polisi linahusika kuruhusu makongamano? Kuna masuali mengi yakujiuliza.
Hapa binafsi namuomba Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, achukue mamuzi kuwadhibiti viongozi katika jeshi la polisi wanaohusika na kuamuru matumizi ya nguvu hizo zinazosababisha umwagikaji wa damu.

Matumizi ya mabavu, nguvu kupita kiasi kuzima vuguvugu za wananchi kwa kile wanachokiamini pamoja na mauaji na hasa kwa wanahabari na raia wasio na silaha hayajawahi kufanikiwa kokote kule duniani.
Ninaamini kuwa serikali yetu ni sikivu na itachukua hatua stahiki kudhibiti na kukomesha vitendo hivi. Kuna mashaka makubwa kuwa, jeshi la polisi lilohusika katika tukio hilo, haliwezi kushiriki katika tume ya kuchunguza ukweli wa mambo.
Jambo la pili ni mwenendo pia ambao umezuka wa kuzuia uhuru wa vyombo vya habari na waandishi wa habari kuwahabarisha wananchi ipasavyo. Maombe mengi yamejitokeza yanayoashiria kampeini yakuwafanya waandishi wa habari washindwe ama kwa kutishiwa au kuzuuiliwa kabisa. Natumaini wakati umefika kwa wananchi kutambua umuhimu wa vyombo vya habari katika kuwahabarisha mambo muhimu yanayohusu maendeleo yao na ya Taifa letu kwa ujumla.
 
Joseph Sekiku
Mwenyekiti
Mtandao wa COMNETA

No comments:

Post a Comment