Friday, September 14, 2012

GENGE LA WAHALIFU LATEKA NYARA POLISI DAR ES SALAAM, TANZANIA

Na Thobias Mwanakatwe,  NIPASHE, 11th September 2012.
  *Ni yule aliyeshiriki operesheni Bandarini
  *Latoa masharti ya kuachiwa huru wenzao


 Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova
  Katika tukio linalofanishwa na vita ya vigogo wa dawa za kulevya dhidi
  ya mamlaka za serikali nchini Mexico, limetokea nchini kwa askari wa
 Bandarini jijini Dar es Salaam, Cornel Kufaizalu, ambaye alishiriki katika operesheni
  ya kukamata watu waliovamia bandari kwa lengo la kuiba madini ya shaba
 na petroli, kutekwa nyara na watu wasiojulikana ambao pia inadaiwa
 wametishia kumuua kama masharti yao hayatatimizwa na polisi haraka.


  Askari huyo ambaye anaonekana kama shujaa kwa kujitoa muhanga kupambana
 dhidi ya askari wenzake walioamua kuasi na kujiunga na magenge ya wizi
 na uhalifu bandarini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, sasa ametekwa nyara
  na hajulikani aliko.

Askari huyo alikuwa mwiba dhidi ya watuhumiwa wa wizi wa mali bandarini
 Dar es Salaam akipambana na watu hao miongoni mwao wakiwamo askari
waliokuwa doria na taarifa kuhusiana na sakata hilo zilitolewa na Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe,wakati akizungumza na waandishi wa
 habari Jumamosi iliyopita.

Taarifa ambazo NIPASHE imezipata ambazo zilithibitishwa na viongozi wabandari hiyo pamoja na Wizara ya Uchukuzi zinasema kwamba askari huyo
 alitekwa Septemba 8, mwaka majira ya jioni na watu wasiojulikana ambao
  wamempeleka kusikojulikana.

 Waziri Mwakyembe alipoulizwa kuhusiana na tukio hilo, alisema amepewa
taarifa za kutekwa kwa askari huyo ikiwa ni siku moja tu baada ya
kukamatwa kwa watu 14 waliovamia bandari usiku wa kuamkia Jumamosi iliyopita.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na viongozi na wafanyakazi wa
 bandari,watu waliomteka askari huyo wametoa masharti kwamba
 watamuachia huru iwapotu wenzao watuhumiwa waliokamatwa
wakati wa mapambano kati yao na polisi
 wa bandarini katika tukio hilo wataachiwa huru.

  Walisema watekaji hao ambao wametuma ujumbe mfupi wa maneno katika simu
 ya askari huyo aliyetekwa, wametoa muda wa saa 24 kuachiliwa kwa watu
hao waliokamatwa katika tukio hilo na kama hawataachiwa, watachukua uamuzi
  mwingine dhidi yake.

 Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema
 taarifa walizopata ni kwamba askari huyo amepatikana Mafinga mkoani
  Iringa.

 Wakati Kova akieleza hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael
Kamuhanda, alipoulizwa alisema hana taarifa za askari huyo wa bandari
 aliyetekwa kupatikana mkoani kwake.

  Dk. Mwakyembe akizungumza na waandishi wa habari Jumamosi iliyopita
 baada ya kutokea tukio hilo, aliagiza watu wote waliohusika na wizi huo
 wakamatwe na kufunguliwa mashitaka, wakiwemo askari waliokuwa doria
 ambao baada ya kufika eneo la tukio walianza kuiba mafuta badala ya kusaidia
askari wa bandarini kupambana na wezi.

  Alisema ofisa wa bandarini aliyehusika kufunga kontena namba MSKU
 268357(6) ameshafahamika na yeye atakamatwa ili afunguliwe mashitaka.

Akielezea zaidi kuhusiana na tukio hilo, Dk. Mwakyembe alisema Jumamosi
  usiku kulitokea matukio mawili ya wizi. La kwanza lilitokea saa 9:00
ambalo injini ya treni yenye kichwa namba CK620006 ilikuwa inakwenda bandarini kwa ajili ya
kubeba mabehewa manane.

Waziri Mwakyembe alisema kati ya hayo, matano yalibeba mbolea na matatu
 yalikuwa tupu. Alisema katika treni hiyo kulikuwa na wafanyakazi wanne ambao ni dereva
  Abdallaham Shebe (dereva), Bakili Kitanda (muongoza treni), Polisi PC
 Abubakar mwenye namba F 8784 na msimamizi wa treni Gideon Anyona.

 Dk. Mwakyembe alisema wakiwa bandarini, walivunja kontena ambayo ilikuwa
  na shaba na kuanza kupakua na kuihamishia kwenye makontena ya treni ya
 Tazara na kufanikiwa kuhamisha vipande 19.
 Wakati wakiendelea na harakati hizo, kulizuka mapambano kati ya polisi
  wa bandarini  na wafanyakazi hao ambayo dereva pamoja na muongozaji
walifanikiwa kukimbia na kwenda eneo la Yombo na wengine wawili
walikamatwa.

  Tukio la pili lililotokea saa 10 alfajiri katika depo ya Oryx ambako
 kulikuwa na kundi kubwa la watu waliokuwa wanaiba madumu ya mafuta na
kuyatupia upande wa pili wa bandarini. Madumu yalikuwa tisa ya lita 20
  kila moja lilikuwa na petroli.
 Alisema wakati wanaendelea na harakati hizo, polisi waliokuwa doria
 walifika eneo la tukio na kukuta polisi wa bandarini wakipambana na
  kundi la wezi, lakini polisi wa doria badala ya kuwasaidia polisi wa bandarini
 kupambana na wezi hao, walianza kuiba madumu hayo ya mafuta na kuchukua
 manne na kuondoka nayo.
  Aidha, alisema bosi aliyewatuma wafanyakazi kuiba shaba kwenye kontena
 anaonekana kuwa ni mzoefu hivyo watamkamata kwa sababu wameshamfahamu.

 WATU 14 WATIWA MBARONI
Kamanda Kova jana alizungumza na waandishi wa habari na kusema kuwa
 Septemba 8, mwaka huu majira ya saa 8:00 usiku katika eneo la Shedi No.
 7, polisi waliwakamata watu 14 kwa kosa la kuvunja kontena na kuiba vipande
  19 vya madini ya shaba, mafuta ya petroli lita 360 na dizeli lita 60.

 Aliwataja waliokamatwa kwa kuiba madini ya shaba kuwa ni Askari Polisi
 kikosi cha Tazara mwenye namba F. 8774  PC Abubakar; Charles Rejino
  (49),  mkazi wa Tandika Azimio;  Range Boaz (40),  mkazi wa Kichemchem Mbagala
na Willy Mwamlima (20), mkazi wa Kiwalani.

 Wengine ni Ally Rwanda (28), mkazi wa Tandika Azimio; Said Salum (39),
mkazi wa Tandika Azimio; Shabani Matimbwa (33), mkazi wa Tandika; Salum
 Kinyama (34) mkazi wa Tandika Azimio na Gideon Anyina (35) mkazi wa
 Mbezi Louis

Kuhusu tukio la wizi wa mafuta ya petroli lita 360 na dizeli lita 60
yaliyoibwa katika yadi ya Oryx, aliwataja waliokamatwa kuwa ni MohamedSaid(18),
mkazi wa Mtoni Mtongani na Fadhili Said (18), mkazi wa Mtoni kwa
  Azizi Ally.

 Wengine ni Ailaji Bakari (19), mkazi wa Kurasini na Erasto Adam (18),
 mkazi wa Kurasini Shimo la Udongo.

 Kamanda Kova alisema kimeundwa kikosi kazi cha watu 10 kinachojumuisha
  askari polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Polisi  bandari na Polisi
 Tazara kwa ajili ya kuhakikisha kuwa matukio ya wizi  bandarini yanakomeshwa.

No comments:

Post a Comment