MKUU
wa Wilaya ya Kahama, Benson Mpesya, juzi alimkwida na kumuondoa kwenye
mstari Diwani wa Kata ya Nyihogo, Amos Sipemba (CHADEMA), wakati
akielekea kupata chakula cha mchana kilichokuwa kimeandaliwa kwa ajili
ya msafara wa Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
Tukio hilo lilitokea kwenye viwanja vya Rest House ambapo viongozi
wengi wa kitaifa hufikia, ambapo Mpesya alianza kuwakaribisha wageni wa
kimkoa kutangulia kupata chakula hicho huku akiwataka baadhi ya viongozi
na wawakilishi wa wananchi kuungana na msafara huo.
Mpesya ambaye alionekana kuwa makini zaidi na ugeni huo wa kitaifa
ambao ulikuwa wa kwanza tangu ateuliwe kushika wadhifa huo miezi minne
iliyopita, alisimamia ugawaji wa chakula kwa watu wote waliokuwa katika
msafara huo.
Baada ya kumaliza kutangaza wageni wa kimkoa aliwachagua Mwenyekiti
wa Halmashauri ya Mji, Machibya Jiduramabambasi na makamu wake, Lucas
Makulumo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya, Alfred Mahanganya na
makamu wake, Mibako Mabubu pamoja na Diwani wa Kahama Mjini waungane kwa
pamoja na wageni hao kupata chakula.
Diwani huyo wa Kahama Mjini, Abbas Omari, aliambatana na wenzake wa
Kata ya Mwendakulima (TLP), Ntabo Majabi na Sipemba wa Kata ya Nyihogo
(CHADEMA) katika msafara wa kupata chakula.
Mkuu
huyo wa wilaya baada ya kuona hivyo, alimfuata Sipemba na kumzuia
kuingia kwenye mstari huo lakini akaonekana kukaidi ndipo akanyanyuliwa
kwa kushikwa kwenye mkanda wake wa suruali maarufu kama Tanganyika Jeki
na kuondolewa katika mstari huo wa wageni na kukabidhiwa kwa polisi
waliokuwa wakilinda usalama wa eneo hilo.
Kutokana na kitendo hicho cha udhalilishaji kwa diwani huyo, baadhi
ya wenzake walianza kulalamika wakihoji kama tatizo ni kutoalikwa ni kwa
nini yule wa TLP aliyeingia naye kwenye mstari ameachwa akiendelea
kupata chakula.
Baada ya malalamiko hayo, Mpesya alikwenda tena kwenye mstari wa
wageni na kumtaka diwani wa TLP naye atoke, ambapo alitii na kuondoka
kurejea nyuma kusubiri zamu ya wageni wa wilaya.
Mkuu
huyo alisikika akizungumza kwa ukali kuwa madiwani mara nyingi wamekuwa
wakivuruga utaratibu wa itifaki katika misafara mbalimbali ya wageni wa
kitaifa, hivyo aliwataka kuheshimu.
Baadaye wakati wageni wakiendelea kupata chakula, Mpesya alimfuata
diwani huyo na kumnasua mikononi mwa polisi alikokuwa amemkabidhi na
kumpeleka ndani walikokuwa wakipata chakula wageni wa kitaifa ili
aungane nao.
“Mzazi hutakiwi kuwa na kinyongo na mtoto akifanya kosa kwani
akikunyea mkono huwezi kuukata, leo diwani huyo atapata chakula na
wakubwa humo ndani,” alisema Mpesya mbele ya wageni baada ya kumpeleka
diwani huyo.
No comments:
Post a Comment