Imeingizwa humu tarehe 23/9/2012.
Lindi yaweza kuwa Sri Lanka ya Tanzania
Toleo la 259
19 Sep 2012
WATANZANIA wengi tukisikia jina Sri
Lanka jambo kubwa linalotujia kwa haraka ni ama chai au Vita ya Tamil
Tigers. Nakumbuka tulipokuwa darasa la sita Shule ya Msingi tulisoma
‘Chai Sri Lanka’ na kusoma miji kama Kolombo, Batikaloa na Trinkomalee
(Colombo, Batticaloa, Trincomalee). Lakini tulipashwa sana habari kuhusu
vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka takribani 30. Juzi
nilikuwa Sri Lanka. Vita imekwisha mwaka 2009. Chai ipo nyingi sana.
Mwaka 2010, Sri Lanka iliuza nje jumla ya tani 314,000 za chai yenye
thamani ya dola za Marekani bilioni 1.37 na hivyo kuongoza duniani
kimapato ingawa Kenya ilisafirisha chai nyingi zaidi, tani 441,000.
Hata
hivyo, kutokana na ubora wa zao hilo kuwa chini kidogo Kenya ilipata
dola za Marekani milioni 800 tu. Mwaka huo Tanzania, yenye eneo kubwa
zaidi la kulima
kuliko nchi zote hizo, iliuza nje tani 34,000 tu na kupata dola za
Marekani milioni 61 hivi. Licha ya kwamba Tanzania ni nchi ya nne kwa
kuzalisha chai Afrika baada ya Malawi, Uganda na Kenya, bado inaweza
kuwa katika nafasi ya juu duniani iwapo tukiamua kuwa makini katika
mambo tunayofanya na kupenda kufanya mambo makubwa.
Siku
hizi napenda kujua historia za nchi katika kupambana na umasikini wa
watu wao. Lengo ni kuelewa juhudi za nchi mbalimbali katika kuleta
maendeleo ya watu na kujifunza pale ambapo nchi zimefanikiwa. Ukitembea
mitaa ya Jiji la Colombo unaona mji mzuri msafi uliopangwa vema na kila
mtu anaonekana kushughulika. Njia nzuri ya kujua ukweli wa maisha ya
watu ni kuzungumza nao.
Mara
nyingi hutumia madereva wa teksi au
bajaji kwa jiji kama la Colombo. Katika mazungumzo na baadhi ya
madereva wa bajaji nilizokuwa natumia pale Colombo niliona mwelekeo
mmoja, kwamba katika kipindi cha miaka 10 iliyopita maisha yao
yamebadilika sana. Wakisifia kuisha kwa vita dhidi ya Tamil Tigers na
kuongezeka kwa mapato yao kwa watu kutumia zaidi usafiri. Dereva wa
bajaji wa Jiji la Colombo anaingiza wastani wa rupia 4000 (shilingi
45,000) kwa siku. Nilitaka kujua nini chanzo cha mabadiliko haya ya
kipato ambacho hadi wenye bajaji wanafaidika nayo. Takwimu zao zinaeleza
mengi sana. Serikali iliamua kupambana na umasikini na hasa umasikini
wa vijijini.
Mwaka
2002 asilimia 22.7 ya wananchi wote wa Sri Lanka walikuwa wanaishi
chini ya mstari wa umasikini. Ilipofika mwaka 2011, kiwango cha
umasikini kilikuwa asilimia sita tu. Umasikini ulishuka kwa kiwango
kikubwa katika maeneo ya
vijijini. Katika kipindi cha miaka mitatu kati ya mwaka 2007 mpaka 2010
umasikini wa wananchi wa Sri Lanka walio kwenye sekta ya chai (estate
sector) ulishuka kutoka asilimia 32 ya waliokuwa wanaishi chini ya
mstari wa umasikini mpaka asilimia 11.4 na wale wa vijijini nje ya sekta
ya chai umasikini ulishuka kutoka asilimia 24.7 mpaka asilimia 9.4
katika kipindi hicho. Nilipouliza zaidi kwa wanasiasa na viongozi wa
serikali nikaambiwa kuwa mabadiliko makubwa yaliyotokea miaka ya
karibuni yalitokana na serikali kufanya uamuzi mahususi wa kuelekeza
fedha nyingi zilizokuwa zinakwenda vitani kwenye uwekezaji vijijini.
Wanasema walitumia fedha nyingi kwenye ruzuku ya mbolea kwa wakulima,
kusambaza umeme vijijini na kujenga barabara za vijijini. Siku
niliyofika niliona kwenye moja ya magazeti yao ya kila siku, rais wao
akizindua mtambo wa kuzalisha umeme katika Mji wa Trincomalee uliopo
mashariki mwa nchi hiyo.
Nikajiuliza
mbona na sisi tunatekeleza MKUKUTA na tunasema kwamba tunawekeza fedha
nyingi sana vijijini? Mbona na sisi tunatoa ruzuku ya mbolea yenye
thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 60 kwa mwaka? Inakuwaje wenzetu
wafanikiwe sisi tusifanikiwe? Tanzania imeanza kutoa mbolea ya ruzuku
katika msimu wa mwaka 2006/2007 kama ilivyo kwa Sri Lanka. Wenzetu
katika miaka mitatu, kiwango cha umasikini kimepungua kwa asilimia 15
kwa wananchi walio katika sekta hiyo ya kilimo na wanaoishi vijijini.
Sisi katika kipindi cha muongo mmoja, 2001 mpaka 2011, umasikini
umepungua kwa asilimia mbili tu. Moja ya sababu ya sisi kushindwa ni
kwamba mfumo wa mbolea ya ruzuku umegubikwa na ufisadi wa hali ya juu
sana. Mfumo huu umedhihirisha namna ambavyo kazi ya kupambana na ufisadi
ni ya kimfumo zaidi maana kwa namna viongozi wa vijiji wanavyoiba
mbolea ya ruzuku, unaweza kiurahisi kabisa kusema rushwa
ni sehemu ya utamaduni wa Mtanzania. Siamini hivyo. Ninaamini kwamba
mfumo wetu unazalisha wala rushwa, walafi na watawala wenye tamaa na
wasiotosheka kama nilivyoeleza katika makala zangu zilizotangulia. Je,
tukiondoa ufisadi wa mbolea ya ruzuku tunaweza kupata mafanikio ambayo
wenzetu wameyapata? Sina jibu wala jawabu la swali hili. Hata hivyo,
ninaamini kwamba kutofanikiwa kwetu ni zaidi ya ufisadi. Ni kutofanya
kazi kwa bidii? Ni kukosa umakini? Ni kutofurahia mafanikio? Ni kukosa
uongozi thabiti unaoweza kusimamia mchakato wa maendeleo kuanzia ngazi
ya kijiji mpaka Taifa?
Hebu
tutazame pamoja takwimu hizi. Sri Lanka ina ukubwa wa kilometa za mraba
65,000. Mkoa wa Lindi una ukubwa wa kilometa za mraba 66,000. Sri Lanka
ina Pato la Taifa la Dola za Marekani bilioni 60 mwaka 2011, Tanzania
Pato lake la Taifa ni dola za Marekani bilioni 24. Sri
Lanka ina jumla ya watu milioni 20, Tanzania ina jumla ya watu milioni
45, Mkoa wa Lindi una jumla ya watu 750,000 hivi. Sri Lanka na Tanzania
zote zina bajeti ya dola za Marekani bilioni tisa hivi. Uchumi wa Sri
Lanka unategemea sana zao la chai na utalii kwa fedha za kigeni. Mkoa wa
Lindi una eneo kubwa zaidi la Kilimo kuliko Sri Lanka nzima hasa
ukizingatia katika hekta milioni 5.2 zinazofaa kwa kilimo ni hekta
500,000 tu ndio zinalimwa. Zao la korosho laweza kuwa chai ya Lindi.
Kilometa za mraba 18,000 za Mkoa wa Lindi ni Selous Game Reserve, Kilwa
ni kivutio kikubwa cha utalii wa kila namna na Mkoa wa Lindi una fukwe
ambazo hazijawahi kuguswa tangu dunia iundwe na Mola.
Sri
Lanka hawana gesi asilia. Lindi na hasa Wilaya ya Kilwa ndio mzalishaji
mkubwa wa gesi asilia hapa nchini. Pia sehemu kubwa ya gesi
iliyogunduliwa hapa nchini ipo katika
Mkoa wa Lindi ingawa wengi wetu hudhani kwamba ipo Mkoa wa Mtwara.
Lakini Lindi na Mtwara sawa tu. Mtwara ina kilometa za mraba 16,000
(chini ya eneo la Lindi lililopo Selous). Tufanye Lindi na Mtwara kwa
pamoja ndiyo Sri Lanka ya Tanzania. Tunaweza kujenga uchumi wa dola za
Marekani bilioni 60 kwa Lindi na Mtwara? Tunaweza kufanya mikoa hii iwe
na kiwango cha umasikini chini ya asilimia tatu ya wananchi wake?
Tunaweza kuingiza watalii 800,000 kwa mwaka kwa mikoa hii tu? Tunaweza
kuuza nje korosho yenye thamani ya dola za Marekani angalau milioni 600?
Tunaweza kutumia sehemu ya mapato yatokanayo na gesi asili kujenga
miundombinu ya barabara, umeme, reli na maji kwenye wilaya zote za hii
Sri Lanka yetu? Tunaweza kuwekeza kwenye elimu kuhakikisha kila mtoto
anapata elimu bora? Tunaweza kuhakikisha kuwa asilimia 97 ya wakazi hii
Sri Lanka yetu wanapata huduma za afya?
Majibu ya maswali yote haya ni NDIO.
Utashi. Utayari. Uthubutu. Hebu tuthubutu kuiweka Sri Lanka Tanzania.
Lindi na Mtwara ni zaidi ya Sri Lanka. Nikipata fursa ya kuandika tena
nitaandika kuhusu uwekezaji kwenye elimu nchini Sri Lanka na kwamba haki
ya kupata elimu mpaka Chuo Kikuu ni haki ya kikatiba yenye kuweza
kudaiwa mahakamani.
Mwandishi
wa makala haya Kabwe Zitto ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Mwenyekiti wa
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma, Naibu Katibu Mkuu wa
CHADEMA na Naibu Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni.
No comments:
Post a Comment