JAJI Mkuu wa Tanzania, Mhe. Mohamed
Chande Othman amewaapisha na kuwaasa juu ya utendaji kazi Mahakimu
Wakazi wa Mahakama za Mwanzo walioajiriwa hivi karibuni.
Akizungumza mara baada ya kuwaapisha
Mahakimu hao katika hafla iliyofanyika katika Chuo cha Uongozi wa
Mahakama (IJA) wilayani Lushoto hivi karibu, Mhe. Chande alisema kuwa
Mahakimu hao watumie fursa waliyoipata katika kutoa haki sawa na kwa
wakati stahiki.
“Mahakama imejiwekea
mkakati wa kuajiri Mahakimu wenye shahada ya Sheria, na kwa mara ya
kwanza tumefanikiwa kuajiri jumla ya Mahakimu 300 wenye shahada ya
sheria, hivyo, Mahakama na jamii kwa ujumla ina matumaini makubwa juu ya
ujio wenu katika suala zima la utoaji haki,” alibainisha Jaji Mkuu.
Alisema kuwa asilimia 70
ya mashauri yapo katika Mahakama za Mwanzo jambo ambalo linapelekea
wingi la mashauri na hivyo kuwataka Mahakimu kusikiliza na kuzitolea
maamuzi kwa wakati kesi ambazo ushahidi tayari wake umekamilika.
Aliongeza kwa kutaja
sifa za Hakimu bora na kuainisha kuwa anatakiwa kuwa anayetoa maamuzi
kwa kuzingatia haki, sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.
“Hakimu bora anatakiwa
pia kulinda heshima ya Mahakama na taaluma yake na ya Mahakimu wenzake,
pamoja na kuheshimu wajibu wake kwenye jamii husika na vilevile kufuata
maadili ya kazi katika suala la utoaji haki,” alisisitiza.
Katika hatua nyingine,
Jaji Kiongozi, Mhe. Fakih Jundu aliwaasa pia Mahakimu hao kuzingatia
haki za washitakiwa ikiwemo upatikanaji wa dhamana endapo mshitakiwa
husika anastahili.
“Ni muhimu kwenu
kuzingatia haki za washitakiwa na kuepuka matumizi mabaya ya vifungu vya
sheria, mkifanya hivyo mtajiweka katika nafasi nzuri ya kufanya
maamuzi ambayo hayakiuki misingi ya haki,” alisema Jaji Kiongozi.
Sambasamba ya shughuli
ya kuwaapisha Mahakimu hao, pia wamepata mafunzo ya wiki moja kutoka kwa
viongozi mbalimbali wa Mahakama juu ya utendaji kazi wa kila siku
hususani suala zima la utoaji haki nchini.
Jumla ya Mahakimu 372
wameapishwa na Mhe. Jaji Mkuu, kuwa Mahakimu Wakazi wa Mahakama za
Mwanzo zilizoko katika vituo mbalimbali nchini, Mahakimu 72 ambao
walikuwa tayari kazini wameapishwa pia kuwa Mahakimu Wakazi baada ya
kupata Shahada ya Sheria.
|
No comments:
Post a Comment