Toleo la 257
5 Sep 2012
MOJA ya mambo yenye kushangaza katika mjadala
unaoendelea Zanzibar kuhusu Muungano wa Tanzania ni ile dhana ya kwamba
upinzani dhidi ya muundo wa sasa wa Muungano ulianza jana au kwamba umekuwa
ukichochewa na mtu fulani au kikundi fulani chenye ‘ajenda ya siri.’
Ukweli wa mambo ni kwamba Muungano uliasisiwa
katika mazingira ya kutatanisha na hivyo tangu siku ya mwanzo ya kuzaliwa kwake
ni wachache Zanzibar waliousherehekea kwa moyo mkunjufu.
Wengi walikuwa na
dukuduku na waliingiwa na wahasha lakini hawakuwa na la kufanya. Wajumbe kadhaa wa Baraza la Mapinduzi la awali
wameniambia kwamba lau suala hilo lingejadiliwa kwa uwazi katika Baraza hilo na
lau wajumbe wa Baraza wangepewa fursa ya kuamua basi wangeliupinga muundo huo
wa Muungano.
Hawasemi kwamba wangelipinga kuwapo kwa aina ya
umoja au shirikisho baina ya Tanganyika na Zanzibar, lakini wangepinga muundo
ulioibuka wa Muungano wa nchi hizo mbili. Tukumbuke kwamba wakati huo Baraza la
Mapinduzi ndilo lililokuwa na majukumu ya utungaji wa sheria za Jamhuri ya Watu
wa Zanzibar.
Wenye kuhoji (bila ya kutoa hoja madhubuti) kwamba
wenye kuupinga muundo wa Muungano wana ajenda ya siri ya kurejesha usultani
wanajikanganya na kujisuta wenyewe.
Sijui Sheikh Abeid Karume, mmoja wa waasisi wa
Muungano huu, alikuwa na ajenda gani ya siri alipokuwa akiupiga vijembe
Muungano katika siku za mwisho za uhai wake. Wakati huo alikuwa
amekwishatanabahi kwamba muundo wa Muungano kama ulivyo haukuwa na manufaa kwa
nchi yake. Ndiyo maana akatamka kwamba ‘Muungano ni kama koti likikubana
unalivua’.
Wakati mwingine siku moja tu kabla hajaiaga dunia alimwambia
Bwana Salim Rashid, katibu mkuu wa kwanza wa Baraza la Mapinduzi, kwamba
Muungano ni kama matoto ya treni na Zanzibar inashikilia shoka ambalo karibu
italitumia kuukata mnyororo unaoyaunganisha hayo matoto na ukikatika kila toto
litakwenda upande wake. Kwa hayo alikuwa na maana kwamba Tanganyika ingekwenda
upande wake na Zanzibar ingekwenda upande wake.
Wala sijui kina Kanali Seif Bakari na wenzake na
tepu zao za ‘Kiroboto’ zilizokuwa zikitangazwa Redio Zanzibar walikuwa na
ajenda gani na ya kumrejesha sultani gani Zanzibar.
Ninachojaribu kukumbusha ni kwamba upinzani dhidi
ya muundo wa Muungano haukuanza jana wala leo. Lililo muhimu zaidi ni kutambua
kwa kujikumbusha kwamba upinzani huo ulijikita pia ndani ya duru za waliokuwa
wakihodhi madaraka Visiwani Zanzibar baada ya Mapinduzi ya mwaka 1964.
Viongozi hao wa Mapinduzi walikuwa na imani thabiti
na ile sera ya kutaka kuleta umoja barani Afrika lakini kwa namna mambo
yalivyokuwa yakienda baada ya kuundwa Muungano walianza kuukosoa muundo wa
Muungano huo.
Mara kadha wa kadha katika uhai wake wa miaka 48
Muungano wetu umekuwa ukikabiliwa na mikwaruzano ya aina kwa aina.
Kwa mfano, kuna kile kisa kilichosababisha Sheikh
Aboud Jumbe kupokonywa wadhifa wake wa kuwa Rais wa Zanzibar mnamo mwaka 1984
alipojaribu kuirejeshea Zanzibar mamlaka yake kamili ya utawala. Aling’olewa
madarakani kwa nazaa na Chama cha Mapinduzi (CCM) na wala si na Baraza la
Mapinduzi kama ilivyotakiwa na Katiba ya Zanzibar.
Ni muhimu tuwe tunakumbuka kuwa Wazanzibari
hawakuanza kudai mabadiliko ya muundo wa Muungano baada ya kuanza mchakato wa
sasa wa kulitafutia taifa Katiba mpya lakini walianza kunung’unika tangu miaka
ya 1960 walipogutuka na kuona kwamba muundo wa Muungano hauwapi fursa waitakayo
ya kujiamulia mambo yao na kuyatetea maslahi yao.
Ndiyo maana kila walipopata fursa ya kutoa maoni
yao juu ya Muungano, kama kwa mfano, wakati wa Tume za Nyalali na Kisanga
Wazanzibari wengi walipendelea pawepo na mfumo wa serikali tatu katika
Muungano.Waliamini kwamba mfumo huo ungeirejeshea Zanzibar mamlaka yake
yaliohamishiwa Bara.
Tusisahau pia kwamba si zamani sana ilikuwa ni
kosa, tena la uhaini, kwa Mtanzania ‘kuujadili’ Muungano kadamnasi, seuze
kupendekeza mageuzi katika muundo wake au kupendekeza kwamba uvunjwe kabisa.
Juu ya kuwako vipingamizi hivyo Wazanzibari
wameendelea kuwa wavumilivu lakini hawakusita kuyakosoa yale mambo yenye
kuyadhuru maslahi yao ya kitaifa.
Wale wenye kufikiri kwamba msimamo wa Wazanzibari
juu ya Muungano ni wa karibuni pamoja na kampeni inayopigwa Visiwani ya kutaka
mageuzi ya kimsingi kuhusu Muungano hawaiangalii historia ipasavyo.
Wangeitalii historia ipasavyo wangeona kwamba hata
katika vikao mbalimbali vya Baraza la Wawakilishi tokea miaka ya 1980 suala la
Muungano lilikuwa likiibuka mara kwa mara na kwamba Baraza hilo kila lilipopata
fursa lilikata maamuzi yenye kutetea maslahi ya Zanzibar. Mifano ya hivi
karibuni ni pamoja na yale maamuzi yanayohusika na masuala ya mafuta na gesi
asilia.
Tumeshuhudia pia kwamba kila siku zikisonga mbele
Baraza la Wawakilishi limekuwa likizidi kupaza sauti yake kuhusu msimamo wake
juu ya Muungano. Limekuwa likifanya hivyo hata kabla ya mchakato wa sasa wa
Katiba kuanza.
Hivyo ni kosa na upotoshaji wa hali ilivyo kudai
kwamba ni jumuiya, chama au mtu fulani mwenye kuwachochea au kuwahamasisha
Wazanzibari wawe na msimamo fulani juu ya Muungano.
Tuseme tu kuwa mazingira ya sasa yanawawezesha
Wazanzibari kutoa maoni yao kwa uwazi zaidi bila ya kuingiwa na hofu. Hii leo
sheria haitomtia nguvuni mtu anayetoa maoni ya kutaka muundo wa Muungano
ubadilishwe au hata anayetaka Muungano wenyewe uvunjwe.
Hofu hiyo ilikuwapo zamani hata pale uliporejeshwa
tena mfumo wa vyama vingi vya kisiasa kwani Mwalimu Julius Kambarage Nyerere
alisema kwamba vyama vipya vya kisiasa vinaweza kujadili masuala yote lakini
visiuguse Muungano.
Hivyo, wengi walitishika kuukosoa Muungano
wakiamini kwamba ilikuwa ni uhaini kufanya hivyo kutokana na maneno ya Mwalimu.
Si ajabu kuwaona Wazanzibari wakiwa na hofu hiyo
kwani kwa jumla Watanzania wote waliteseka chini ya mfumo wa chama kimoja cha
kisiasa kuanzia mwaka 1964 hadi 1992.
Kadhalika, kwa muda wa miaka 28 kati ya 48 ya
Muungano, CCM ikiwa na makao yake makuu mjini Dodoma, ndiyo iliyokuwa ikishika
mpini kuhusu masuala ya Muungano kama vile kwa mfano wakati wa kutungwa Katiba
ya Muungano mwaka 1977.
Sasa hali ya mambo imebadilika na ndiyo maana
wakati wa kutoa maoni yao mbele ya Tume ya Warioba kuna Wazanzibari wanaosema
kuwa wanataka pawepo Muungano wa Tanganyika na Zanzibar utaojengeka juu ya
msingi wa Mkataba na si Katiba.
Katika Muungano wa aina hiyo kila nchi itakuwa na
mamlaka kamili ya utawala wa mambo ya ndani ya nchi yake pamoja na shughuli za
kigeni au za kimataifa. Mfumo huo ni bora zaidi kushinda ule wa serikali tatu
ambao wengi wanauona kuwa umepitwa na wakati na uliokwishakataliwa na Serikali
za Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.
Kadhalika, kuna uwezekano mkubwa kwamba muundo wa
aina hiyo utaweza kuzivutia nchi nyingine katika kanda ya Afrika ya Mashariki
na ya Kati kujiunga na Muungano wetu na hivyo kuimarisha kidhati Umoja wa
Kiafrika.
Hapana shaka yoyote kwamba Muungano wa aina hiyo
utakuwa imara na wa maana zaidi kinyume na huu wa sasa ulioselelea kuwa wa nchi
mbili tu takriban nusu karne baada ya kuasisiwa na usiokwisha kukumbwa na
mikwaruzano na kero za kila aina.
Kwa hakika historia ya Muungano itapoandikwa kwa
dhati na bila ya upendeleo itaonyesha kwamba Zanzibar daima imekuwa na dukukudu
kuhusu nafasi yake ndani ya huu Muungano baina yake na Tanganyika. Historia
hiyo itaonyesha pia kwamba kuna Wazanzibari wenye kuamini kwamba wameonewa
katika mahusiano kati ya nchi yao na Tanganyika.
Ili kuondosha chokochoko zilizopo na kuondosha
ukinzani uliopo kati ya pande mbili za Muungano kuna haja ya kuwa na muundo wa
Muungano utaoziridhisha pande zote mbili na utaoweza kuzifuta kabisa na kwa
njia za amani na udugu tofauti zilizopo kati yao kwa manufaa ya Watanganyika na
ya Wazanzibari.
Kama kweli tunataka bara la Afrika liungane
kiuchumi, kisiasa na kijamii basi kuna ulazima kwamba misingi ya umoja huo iwe
madhubuti na iziwezeshe nchi zinazoungana ziungane kila moja ikiwa na mamlaka
kamili ya kujiamulia mambo yenye kuhusika na maslahi yake.
Muungano aina hiyo utafana endapo tu utakuwa ni wa
hiyari na si wa kulazimishwa na ikiwa utaipa kila nchi iliyomo ndani yake haki
ya kuwa na kauli sawa na uhuru wa kujiamulia yaliyo yake bila ya kuyadhuru
maslahi ya nchi nyingine zilizo ndani ya Muungano huo.
No comments:
Post a Comment