Thursday, September 20, 2012

MTOTO APOTEA MIKONONI MWA BALOZI WA TANZANIA

 Imetoka  "NIPASHE"  TANZANIA.

Mtoto apotelea Marekani akiwa mikononi mwa Balozi


17 September 2012

Binti Anneth Joseph Mangawo (25), wa ukoo wa Owenya anayedaiwa kuchukuliwa na Balozi wa sasa wa Tanzania nchini Zambia, Grace Mujuma, amepotea katika mazingira tatanishi wakati balozi huyo akifanya kazi ubalozi wa Tanzania jijini New York, Marekani.

Balozi huyo anadaiwa kumchukua binti huyo kama msichana wa ndani na kwenda naye nchini Marekani mwaka 2004, ambapo kabla alichukuliwa kutoka kata ya Old Moshi Magharibi, ambako alikaa Dar es Salaam, na baadaye nchini Marekani.

Baba mdogo wa binti huyo, Robinson Owenya, akizungumza na NIPASHE Jumapili, anasema kwa kipindi chote waliwahi kuwasiliana na binti huyo mara moja, hadi Balozi huyo alipomaliza muda wake wa kukaa nchini humo wa miaka minne na kurejea Tanzania mwaka 2008, bila binti huyo. 

Taarifa zinadai kuwa, mwanzoni mwa mwaka 2012, Balozi Grace akiwa ameshateuliwa na Rais kuwa Balozi wa Zambia, alikuja kwenye msiba wa baba yake mzazi eneo la Old Moshi, mkoani Kilimanjaro.

“Tulimfuata kumuuliza juu ya mtoto wetu, majibu aliyotupa ni kuwa alikuwa ananyanyasa watoto wake na mama wa Anneth akamuuliza kwa nini hakumpakia kwenye ndege arudi, alidai kuwa alimpeleka shule akajifunze Kiigereza na ndipo akaiba pasi ya kusafiria na vitambulisho na akaondoka,” alisema Owenya.

Alisema walikwenda kwa baba yake mdogo, anayemtaja kwa jina la Fredy Maro, ambapo waliondoka pamoja na kwenda kwa kaka yake, Dk. Prosper Maro, ambaye alimtetea dada yake na kueleza kwamba wakifuatilia kisheria, binti yao atakamatwa nchini humo na kupelekwa gerezani na hatarudi hadi baada ya kifungo.
“Nilimweleza ninachotaka ni binti yetu apatikane akiwa hai, kama ambavyo alichukuliwa, hatuna mkataba na Mungu,” alisema.

Aliongeza, “alinipa namba za simu za Balozi Grace, ili mama wa Anneth aweze kupata fedha kidogo, nilikataa na kumueleza shida si fedha bali mtoto wetu, akasema hana la kunisaidia.”

Alisema haiingii akilini kuwa mhusika (Grace Fanuel Maro ambaye kwa sasa anaitwa Grace Mujuma), anajenga hoja ya kumhusisha binti huyo na unyanyasaji wa watoto kwenye nchi ya kigeni.

Alisema alitoa taarifa polisi mkoani Kilimanjaro, na kufungua kesi namba KR/CID/PE/03/2012 Januari 16, mwaka huu, ambapo walimtuma kwenda kuichunguza nyumba ambayo inaelezwa Balozi Grace alikuwepo, eneo la Shanty Town, na kuwapa taarifa polisi.

Alisema polisi waliambatana naye hadi eneo hilo, lakini hawakufanikiwa kumkuta kwani muda mfupi alikuwa ameshaondoka kurudi Dar es Salaam.

Alisema waliacha maagizo kwa mama yake (Grace) afike kituo cha polisi na kuandika maelezo ambapo alifanya hivyo na kuweka namba za simu za mwanaye.
“Nilikaa kwa muda, askari mmoja akatumwa Dar es Salaam kufuatilia, ambapo alikuta Grace ameshaapishwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Zambia na wakati anamchukua binti yetu alikuwa Afisa wa Ubalozi,” alisema.

Hivyo, alisema askari polisi hawana uwezo wa kumkamata kwa kuwa anakinga ya kibalozi na
kibali cha kumkamata kinatoka kwa Rais,” alisema.

Alisema alikwenda kwenye kituo cha msaada wa sheria na haki za binadamu jijini Dar es Salaam, ambao waliahidi kumsaidia ikiwa ni pamoja na kutoa kwenye vyombo vya habari lakini hatua hiyo haijafanyika.

“Nimeamua kuyasema haya nikijua kwamba hakuna mwenye mkataba na Mungu, nimefanya hivi ili ifahamike,” alisema.

“Ninamuomba Rais Jakaya Kikwete kuingilia kati suala hili, kwani aliyechukua binti yetu ni Balozi wake na kumekuwa na ubabaishaji mkubwa, familia yetu ni Maskini…”
“Mama yake hajiwezi lakini tunachangishana kupata fedha za kufuatilia suala hili, hatujui tulie msiba au tufanye nini, kama alikufa tungeona hata mwili wake au kujulishwa,” alisema.

Mama mzazi wa Anneth, Judica Owenya, alisema dada yake, Edora Maro, (ambaye ameolewa na baba mkubwa wa Grace), alikwenda
nyumbani kwake na kumuomba binti huyo kwa ajili ya kwenda kufanya kazi.

Akizungumza huku akilia, alisema mwanaye huyo ni uzao wake wa saba, na kwamba anajisikia vibaya kwani hajui kama yupo hai au la,
Hivyo kuiomba serikali kumsaidia kumtafuta mwanaye ambaye hata kwenye msiba wa baba yake mzazi hakufika.

Aidha, kwa mujibu wa barua ya Machi 16, mwaka huu, kutoka kwa kampuni ya uwakili ya Rex Attorneys, yenye kumbukumbu namba REX/GMM/171/12 ambao ni mawakili wa Balozi Grace, akijibu barua ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).
Barua ya LHRC yenye kumbukumbu LHRC/LAC.VOL.XVII/9 ya Februari 27, mwaka huu, ambapo Grace alithibitisha kumchukua binti huyo na kwenda naye Marekani kwa ajili ya kufanya kazi za ndani nyumbani kwake.

Alisema baada ya kufika alifanya kazi kwa mwaka mmoja, ambapo mnamo Desemba 2, 2005, alitoroka baada ya kuchukua hati yake ya kusafiria na vitambulisho vyake vingine, ambapo alitoa taarifakwa polisi wa nchini Marekani (New York Police Department), ambao walisema kwa mujibu wa sheria za Marekani kwa kuwa binti huyo ana umri wa mtu mzima hawana la kufanya bali wanahisi kuwa amepata mpenzi na kwenda kukaa naye.

Alisema pia alitoa taarifa za tukio hilo kwa mjomba wake, ambaye kwa sasa ni marehemu, ambapo baada ya miezi nane kupita tangu kupotea kwake alitoa taarifa kwa vyombo husika kufuta visa yake, ambapo Januari, mwaka 2012 kwa barua ya kumbukumbu namba CID/HQ/PE/16/ 2012 alitoa taarifa kwa Kitengo cha Polisi wa Kimataifa (Interpol) na mnamo Januari 13, mwaka huu, aliieleza familia ya Anneth.

Hata hivyo, Owenya alisema mnamo Julai 14, mwaka huu, aliitwa jijini Dar es Salaam na kukutanishwa na Grace akiwa na mawakili wake wawili, ambapo baada ya mazungumzo ambayo mengine yalikuwa na utata kutokana na muda mwingi walitumia lugha ya kiingireza asiyoifahamu.

Alisema walimshinikiza kuandika barua Interpol kuomba wamsaidie kumtafuta binti yake, lakini alikataa na kueleza kuwa anayemdai ni Grace kwa kuwa ndiye aliyemchukua kijijini na hata walipomuuliza aliwajibu jeuri mara baada ya kukutana kwenye msiba wa baba yake na endapo wasingeuliza asingewajulisha.

Alisema Agosti 15, mwaka huu, alitumiwa kwa njia ya mtandao makubaliano yenye maelezo ya malalamiko yake na sahihi ya Grace na wakili wake, ikiwa na makubaliano yaliyosomeka na kutakiwa kuyasoma na
kuridhika nayo na kisha kuweka sahihi.

“Grace Mujuma ambaye alikwishatoa taarifa Interpol aendelee kufuatilia kupata taarifa zitakazowezesha kupatikana kwa Anneth na ashirikiane na kitengo hicho kumtafuta na kumrudisha kwa wazazi wake mapema iwezekanavyo mara baada ya kupatikana kwake,”alisema.

Alisema anaiomba serikali kulifanyia kazi suala hilo kwani linatia utata na hakuna hatua zinazochukuliwa ili hali muhusika ni mtu mwenye kinga ya kushtakiwa na wenye mtoto ni watu wanyonge wasio na uwezo wa kifedha.

Jitihada za kuwasiliana na Grace kupitia simu za ofisi ya ubalozi wa Tanzania nchini Zambia, hazikufanikiwa kutokana na kuita mara kadhaa pasipo kupokewa.

Chanzo: Gazeti la Nipashe

No comments:

Post a Comment