Binti Anneth Joseph Mangawo (25), wa ukoo wa
Owenya anayedaiwa kuchukuliwa na Balozi wa sasa wa
Tanzania nchini Zambia, Grace Mujuma, amepotea katika mazingira
tatanishi wakati balozi huyo akifanya kazi ubalozi wa Tanzania jijini
New York, Marekani.
Balozi huyo anadaiwa kumchukua binti huyo kama
msichana wa ndani na kwenda naye nchini Marekani mwaka 2004, ambapo
kabla alichukuliwa kutoka kata ya Old Moshi Magharibi, ambako alikaa Dar
es Salaam, na baadaye nchini Marekani.
Baba
mdogo wa binti huyo, Robinson Owenya, akizungumza na NIPASHE Jumapili,
anasema kwa kipindi chote waliwahi kuwasiliana na binti huyo mara moja,
hadi Balozi huyo alipomaliza muda wake wa kukaa nchini humo wa miaka
minne na
kurejea Tanzania mwaka 2008, bila binti huyo.
Taarifa
zinadai kuwa, mwanzoni mwa mwaka 2012, Balozi Grace akiwa ameshateuliwa
na Rais kuwa Balozi wa Zambia, alikuja kwenye msiba wa baba yake mzazi
eneo la Old Moshi, mkoani Kilimanjaro.
“Tulimfuata
kumuuliza juu ya mtoto wetu, majibu aliyotupa ni kuwa alikuwa
ananyanyasa watoto wake na mama wa Anneth akamuuliza kwa nini hakumpakia
kwenye ndege arudi, alidai kuwa alimpeleka shule akajifunze Kiigereza
na ndipo akaiba pasi ya kusafiria na vitambulisho na akaondoka,” alisema
Owenya.
Alisema
walikwenda kwa baba yake mdogo, anayemtaja kwa jina la Fredy Maro,
ambapo waliondoka pamoja na kwenda kwa kaka yake, Dk. Prosper Maro,
ambaye alimtetea dada yake na kueleza kwamba wakifuatilia kisheria,
binti yao atakamatwa nchini humo na kupelekwa gerezani na hatarudi hadi
baada ya kifungo.
“Nilimweleza ninachotaka ni binti yetu apatikane akiwa hai, kama ambavyo alichukuliwa, hatuna mkataba na Mungu,” alisema.
Aliongeza, “alinipa namba za simu za Balozi Grace, ili mama wa Anneth aweze kupata fedha kidogo, nilikataa na kumueleza
shida si fedha bali mtoto wetu, akasema hana la kunisaidia.”
Alisema
haiingii akilini kuwa mhusika (Grace Fanuel Maro ambaye kwa sasa
anaitwa Grace Mujuma), anajenga hoja ya kumhusisha binti huyo na
unyanyasaji wa watoto kwenye nchi ya kigeni.
Alisema
alitoa taarifa polisi mkoani Kilimanjaro, na kufungua kesi namba
KR/CID/PE/03/2012 Januari 16, mwaka huu, ambapo walimtuma kwenda
kuichunguza nyumba ambayo inaelezwa Balozi Grace alikuwepo, eneo la
Shanty Town, na kuwapa taarifa polisi.
Alisema
polisi waliambatana naye hadi eneo hilo, lakini hawakufanikiwa kumkuta
kwani muda mfupi alikuwa ameshaondoka kurudi Dar es Salaam.
Alisema
waliacha maagizo kwa mama yake (Grace) afike kituo cha polisi na
kuandika maelezo ambapo alifanya hivyo na kuweka namba za simu za
mwanaye.
“Nilikaa kwa muda, askari mmoja akatumwa Dar
es Salaam kufuatilia, ambapo alikuta Grace ameshaapishwa kuwa Balozi wa
Tanzania nchini Zambia na wakati anamchukua binti yetu alikuwa Afisa wa
Ubalozi,” alisema.
Hivyo, alisema askari polisi hawana uwezo wa kumkamata kwa kuwa anakinga ya kibalozi na
kibali cha kumkamata kinatoka kwa Rais,” alisema.
Alisema
alikwenda kwenye kituo cha msaada wa sheria na haki za binadamu jijini
Dar es Salaam, ambao waliahidi kumsaidia ikiwa ni pamoja na kutoa kwenye
vyombo vya habari lakini hatua hiyo haijafanyika.
“Nimeamua kuyasema haya nikijua kwamba hakuna mwenye mkataba na Mungu, nimefanya hivi ili ifahamike,” alisema.
“Ninamuomba Rais Jakaya
Kikwete kuingilia kati suala hili, kwani aliyechukua binti yetu ni
Balozi wake na kumekuwa na ubabaishaji mkubwa, familia yetu ni Maskini…”
“Mama yake hajiwezi lakini tunachangishana
kupata fedha za kufuatilia suala hili, hatujui tulie msiba au tufanye
nini, kama alikufa tungeona hata mwili wake au kujulishwa,” alisema.
Mama mzazi wa Anneth, Judica Owenya, alisema dada yake, Edora Maro, (ambaye ameolewa na baba mkubwa wa Grace), alikwenda
nyumbani kwake na kumuomba binti huyo kwa ajili ya kwenda kufanya kazi.
Akizungumza huku akilia, alisema mwanaye huyo ni uzao wake wa saba, na kwamba anajisikia vibaya kwani hajui kama yupo hai au la,
Hivyo kuiomba serikali kumsaidia kumtafuta mwanaye ambaye hata kwenye msiba wa baba yake mzazi hakufika.
Aidha,
kwa mujibu wa barua ya Machi 16, mwaka huu, kutoka kwa kampuni ya
uwakili ya Rex Attorneys, yenye kumbukumbu namba REX/GMM/171/12 ambao ni
mawakili wa Balozi Grace, akijibu barua ya Kituo cha Sheria na Haki za
Binadamu (LHRC).
Barua ya LHRC yenye kumbukumbu LHRC/LAC.VOL.XVII/9 ya Februari 27, mwaka huu,
ambapo Grace alithibitisha kumchukua binti huyo na kwenda naye Marekani kwa ajili ya kufanya kazi za ndani nyumbani kwake.
Alisema
baada ya kufika alifanya kazi kwa mwaka mmoja, ambapo mnamo Desemba 2,
2005, alitoroka baada ya kuchukua hati yake ya kusafiria na vitambulisho
vyake vingine, ambapo alitoa taarifakwa polisi wa nchini Marekani (New
York Police Department), ambao walisema kwa mujibu wa sheria za Marekani
kwa kuwa binti huyo ana umri wa mtu mzima hawana la kufanya bali
wanahisi kuwa amepata mpenzi na kwenda kukaa naye.
Alisema
pia alitoa taarifa za tukio hilo kwa mjomba wake, ambaye kwa sasa
ni marehemu, ambapo baada ya miezi nane kupita tangu kupotea kwake
alitoa taarifa kwa vyombo husika kufuta visa yake, ambapo Januari, mwaka
2012 kwa barua ya kumbukumbu namba CID/HQ/PE/16/ 2012 alitoa taarifa
kwa Kitengo cha Polisi wa Kimataifa (Interpol) na mnamo Januari 13,
mwaka huu, aliieleza familia ya Anneth.
Hata
hivyo, Owenya alisema mnamo Julai 14, mwaka huu, aliitwa jijini Dar es
Salaam na kukutanishwa na Grace akiwa na mawakili wake wawili, ambapo
baada ya mazungumzo ambayo mengine yalikuwa na utata kutokana na muda
mwingi walitumia lugha ya kiingireza asiyoifahamu.
Alisema
walimshinikiza
kuandika barua Interpol kuomba wamsaidie kumtafuta binti yake, lakini
alikataa na kueleza kuwa anayemdai ni Grace kwa kuwa ndiye aliyemchukua
kijijini na hata walipomuuliza aliwajibu jeuri mara baada ya kukutana
kwenye msiba wa baba yake na endapo wasingeuliza asingewajulisha.
Alisema
Agosti 15, mwaka huu, alitumiwa kwa njia ya mtandao makubaliano yenye
maelezo ya malalamiko yake na sahihi ya Grace na wakili wake, ikiwa na
makubaliano yaliyosomeka na kutakiwa kuyasoma na
kuridhika nayo na kisha kuweka sahihi.
“Grace
Mujuma ambaye alikwishatoa taarifa Interpol aendelee kufuatilia kupata
taarifa
zitakazowezesha kupatikana kwa Anneth na ashirikiane na kitengo hicho
kumtafuta na kumrudisha kwa wazazi wake mapema iwezekanavyo mara baada
ya kupatikana kwake,”alisema.
Alisema anaiomba serikali
kulifanyia kazi suala hilo kwani linatia utata na hakuna hatua
zinazochukuliwa ili hali muhusika ni mtu mwenye kinga ya kushtakiwa na
wenye mtoto ni watu wanyonge wasio na uwezo wa kifedha.
Jitihada
za kuwasiliana na Grace kupitia simu za ofisi ya ubalozi wa Tanzania
nchini Zambia, hazikufanikiwa kutokana na kuita mara kadhaa pasipo
kupokewa.
Chanzo: Gazeti la Nipashe