Monday, May 4, 2009

WALIMU WATUHUDUMIA WANAFUNZI !

Leo nimeipata mpya toka Chuo Kikuu cha American (American University) katika kitivo chao cha Sheria (Washington College of Law) ninaposoma kwa muda wa miezi tisa sasa.

Kumbe katika Kitivo hiki, wamejiwekea utaratibu kwamba siku ya kwanza ya Mitihani ya mwisho (May 4, 2009 - yaani leo) ya kila semesta ya mwisho ya mwaka huwa walimu wanawatayarisha wanafunzi chakula wanachokiita "Twilight Breakfast". Chakula hiki ni viazi ulaya vilivyochemshwa, mikate ya aina tatu tofauti, mayai na nyama za aina mbili, bata mzinga (turkey) na nyama ya nguruwe.

Mimi nilipoona tangazo hili, kwa upweke niliokuwa nao nyumbani kwangu kwa kujificha wakati nadurusu (revision), nikaamua kwenda chuoni kujilia vya dezo. Kumbe wengi tulikuwa na wazo hilo hilo. Nilipofika saa 11 kamili jioni wakati wa kuanza msosi huo nikakuta tayari mstari mrefu na umekata kona wa wanafunzi wanasubiri kuhudumiwa na walimu wao. Nikajiunga katika mstari nami nikapata msosi murua. Nimetokea kuipenda sana nyama ya bata mzinga. Walugulu wa Morogoro wanasema ina "nzoso" (taste) ya aina yake. Pia nimeweza kusalimiana na wenzangu; ambao kama mimi walikuwa mafichoni; kila mtu anajihangaikia mwenyewe.

Kilichonishangaza katika hafla hii ni uamuzi wa walimu wetu kutuhudumia sisi wanafunzi. Utamaduni kama huu haupo Afrika. Mwalimu ni mtu mwenye hadhi kubwa na ya juu sana kiasi kwamba haitegemewi kwamba iko siku ataamua kumhudumia mwanafunzi wake wakati akiwa anamfundisha!

1 comment:

  1. Tembea uone! Wengine tunatembea humu humu mitandaoni na kujifunza kutoka kwa watu mnaokumbuka kusimulia mnayokutana nayo, basi ndiyo ikawa japo hatujaona, si haba kwa ni tunajifunza kwa kusoma na kusikia toka kwenu.
    Mila na desturi zetu tafauti ndiyo na tujifunze heshima kwa mkubwa na mdogo vile vile.
    Pole kwa kujiandaa kwa mitihani na hongera kwa kufikia hatua uliyofikia.
    Mafanikio mema Mama Mwatawala binti Mrisho!

    ReplyDelete