Friday, May 15, 2009

UZURI WA MALIASILI YA ROCKY GAP RESORT, USA

WAMAREKANI NA MALI ASILI ZAO

Tangu Mei 10, 2009 hadi Mei 13, 2009 tulikuwa mkutanoni; mkutano ambao ulikuwa wa kutathmini kipindi cha miezi 10 tuliyokuwa hapa Washington DC tukijifunza mambo mbalimbali kutegemeana na kila mmoja wetu jinsi alivyojiamulia. Mimi nilikuwa nasomea sheria, hasa katika masuala ya Haki za Binadamu, nikijikita zaidi katika Haki ya kila mtu ya kupata huduma ya kupata haki yake (Access to Justice).

Hivyo siku hizo tatu ilikuwa pia ni mkutano wa kuagana kwa wanafunzi wote 163 tulioanza masomo yetu Agosti 3, 2008 katika vyuo 15 mbalimbali nchini Marekani, tuliotoka katika nchi zinazoendelea katika Ufadhili wa Serikali ya Marekani chini ya Mfuko wake wa Hubert Horatio Humphrey (HHH). Ufadhili huu hutolewa kila mwaka kuanzia mwaka 1978 na hutangazwa dunia nzima kupitia kwenye intaneti, na wenye bahati ya kutimiza sifa ndio huteuliwa kuhudhuria mafunzo haya. Kundi letu; yaani wafadhiliwa wote wa Mfuko huu tuliotoka nchi zinazoendelea kwa mwaka 2008/2009; litokalo katika nchi 90 duniani linamaliza rasmi masomo haya Juni 12, 2009 na hivyo tarehe hiyo ikifika, kila mmoja wetu anatakiwa awe keshapanda ndege akielekea kwao. Tulishaarifiwa mapema kwamba hata bima ya afya tuliyokatiwa inakwisha siku hiyo. Pamoja na hayo, tumepewa siku 30 zaidi kwa anayependa kuendelea kuwepo hapa kama Mtalii. Mkataba wetu unasema, baada ya kuondoka tarehe hiyo, hutakiwi kuonekana nchi hii hadi uwe umemaliza miaka 2 nchini kwenu ili ulichokisomea huku matunda yake yaonekane kwanza; yaani kikawasaidie wananchi wa kwenu.

Kundi langu mimi, lililokuwa na wanafunzi 11 lilikuwa katika Chuo kiitwacho American University, Washington College of Law, kilichopo jijini Washington DC, Marekani. Ikumbukwe tu kwamba jiji hili ambalo ndio mji mkuu wa serikali wa nchi hii, lina idadi ya Wakazi 700,000. Katika kundi langu nipo mimi kutoka Tanzania. Wengine ni Kayum Ahmed kutoka Afrika Kusini (South Africa), Anneen De Jay kutoka Namibia, Michelle Maharajh-Brown kutoka Trinidad & Tobago, Wei na Cheng Dong kutoka China, Abdulhamid Nawaz Dilip kutoka Sri Lanka, Tarmelan Ibraimov kutoka Kirghizstan, Andrea de Souza na Flavia Pixoto toka Brazil na Roberto Moreno kutoka Panama. Katika nchi zilizowakilishwa na wanafunzi wawili wawili ni kutokana na ukubwa wa nchi hizo; yaani China na Brazil.

Hapa kwenye mkutano katika Wilaya ya Cumberland, jimboni Maryland panaitwa Rocky Gap Lodge & Golf Resort. Pana ziwa dogo liitwalo HABEEB ambamo mna samaki pia. Wapenzi wa kuendesha ngalawa na mitumbwi wanafurahia sana kutembea, kuvua na kufanya mazoezi katika ziwa hilo. Kina sisi wapenda kuendesha baiskeli kuna njia zetu pia za kupita na baiskeli kulizunguka ziwa hili. Vivyo hivyo pia kuna pia huduma za Gofu, kutembea kwa farasi, vigari vidogo vya kuendeshwa kutalii eneo hili, endapo mtu hawezi kutembea mwenyewe kwa miguu, bwawa la kuogelea ingawaje ziwa lipo hapo hapo, na kuna hao wenye afya zaidi ambao huamua kulizunguka ziwa hili kwa miguu, ambalo ukilimaliza lote ni kama wastani wa maili kati ya 6 hadi 8 hivi. Lakini njia za kutembea kwa miguu zimegawanywa katika sehemu fupi fupi pia.

Mandhari ya eneo hili kwa kweli sijawahi kuona katika umri na matembezi yangu niliyowahi kuyafanya popote pale. Kwa ufupi tu ni kama bakuli hivi. Yaani eneo limezungukwa na milima ya urefu wa kiasi katika pande zake na ziwa liko katikakati. Hiyo milima iliyozunguka ni kivutio tosha maana imevikwa misitu mizuri ya kijani kwa wakati huu wa mwezi Mei, kwani majani yalishaota baada ya kipindi cha kipupwe (winter) ambapo majani huwa yanadondoka na miti huachwa pepepe. Kutembelea mahala hapa ni ushuhuda mwingine wa kuonyesha ni kiasi gani wenzetu wanavyothamini mazingira yao na kuenzi mali asili zao. Hapa ni mahali pazuri mno kiasi kwamba ukifika hutaki kuondoka. Nafsi yako inakuambia ukodoleeee tuu.

Siku tulipofika, tulikuta barua toka kwa Meneja wa zamu (Front Desk Manager) Jaime Gordon iliyotufahamisha kwamba kuna ukarabati unaondelea wa kubadilisha televisheni vyumbani. Hivyo asiyependa usumbufu huo aweke tangazo mlangoni kwake ili asisumbuliwe (Do Not Disturb). Jambo hili nimeona ni la kiungwana sana la kutoa taarifa kwa wateja juu ya nini kinachoendelea.

Katika tembeatembea yangu katika hifadhi hii, nilikutana na sungura pori ambao ni wadogo kuliko sungura wa kufugwa na pia wana rangi zinazopendeza zaidi kwani rangi yao sio moja kama vile nyeupe tu. Sungura hawa ni wa rangi ya udongo na mkiani wana mstari mweupe unaopakana na mistari miwili mieusi. Utafikiri mtu kawachora mikiani. Kumbe ndivyo walivyoumbwa na Mola.

Pia katika pitapita yangu, nilikutana na jiwe pana kiasi cha mita moja kwa mita moja lililochongwa vipepeo na kuandikwa jina la mtu. Jiwe hili halikusimamishwa kama nilivyozoea kuona mawe yakisimamishwa kwa mfano kutambulisha kitu. Jiwe hili lilikuwa limelazwa chini lakini maandishi yake yalikuwa yanasomeka vizuri. Lilikuwa linatunzwa vizuri. Nilipouliza hotelini jina lile lililoandikwa jiweni lilikuwa la nani. Nikaambiwa kwamba mmoja wa wadau wa hotelini pale aliyekuwa na Kampuni ya kuwahudumia watu katika burudani mbalimbali (Western Maryland Adventures LLP) alikuwa na mtoto alifariki. Lile lilikuwa ndio jiwe la kumbukumbu la marehemu huyo aliyekuwa akiitwa KELSEY MICHELLE MILLER amezaliwa 1987 na amefariki 2004. Hiki pia kwangu kilikuwa kitu kigeni. Tumezoea kwetu Afrika mawe ya kumbukumbu yanawekwa makaburini lakini kumbe wenzetu wanaweka popote pale wachaguapo, pamoja na lile jiwe la malaloni.

Kwa kweli ilipofika saa tano kamili siku ya tarehe 13 Mei, 2009 na basi likang'oa nanga mahala pale, kila mmoja kati yetu alikuwa anajutia nafsini mwake kwa nini hatukukaa zaidi mahali pale. Itokeapo siku nawe msomaji wangu ukatamani kufika mahala hapo, tovuti yao ni hii hapa:

www.rockygapresort.com

No comments:

Post a Comment