Imeingizwa hapa leo hii 29/10/2012.
Zitto amlipua Dk Hoseah wa Takukuru
Daniel Mjema, Rombo na Exuper Kachenje, Dar es Salaam, Tanzania.
MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe amemlipua Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru), Dk Edward Hoseah, akidai kuwa bosi huyo ameandikia barua Uswisi, akieleza kwamba Tanzania haina masilahi na mabilioni ya fedha yaliyofichwa katika benki za nchini hiyo.
Zitto amedai pia kwamba, atawasilisha hoja binafsi katika kikao cha Bunge kinachoanza keshokutwa Jumanne, akiiomba Benki ya Dunia (WB), kutumia kikosi chake kinachojulikana kama Asset Recovery Unit (ARU), ili kuwabaini Watanzania walioficha fedha hizo na namna gani zitarejeshwa nchini.
Hata hivyo, alipotafutwa na Mwananchi Jumapili jana jioni, huku akionyesha kushangazwa na madai hayo ya Zitto Dk Hoseah amekanusha akisema kuwa tuhuma hizo hazina ukweli wowote.
“Nashangaa, kwanza nipo hospitali naumwa, wala sijawahi kuandika barua anayodai Zitto,”alisema Dk Hoseah.
Mkurugenzi huyo wa Takukuru alisisitiza: “Anavyosema Kabwe, labda muulizeni vizuri. Huo ni uongo, mimi sijawahi kuandika barua hiyo na sifanyi biashara hiyo. Tambua kuwa hilo siyo kweli, sisi tunafanya kazi kwa mujibu wa sheria. Kama kweli mwambieni huyo Zitto aonyeshe hiyo barua.”
Hata hivyo alivyotakiwa kueleza kuhusu afya yake na mahali alipolazwa, Dk Hoseah alisita na kusema:
“Wewe jua hivyo tu kwamba ninaumwa, nimepumzika. Siyo India, nipo nyumbani.”
Zitto Kabwe alitoa tuhuma hizo dhidi ya Dk Hoseah jana (27/10/2012) eneo la Kibaoni, Kata ya Nanjara Reha, wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro katika mkutano wa hadhara, ambapo alimtaka Dk Hoseah ajitokeze hadharani na kuwaeleza Watanzania sababu za kuandika barua hiyo.
“Juzi tumeambiwa, Dk Hoseah ameandika barua kwenda Uswisi kuwaambia ya kwamba, Tanzania hatuna interest (masilahi) na hizo fedha zilizofichwa huko nje kwa sababu ni fedha binafsi…; Huyu ndiye mkurugenzi wa kupambana na rushwa nchini,” alisema Zitto.
Aliongeza: “Tunamtaka Dk Hoseah atuonyeshe barua aliyoiandika kwenye mamlaka za kule Uswisi na atuambie ni kwa nini ameandika barua kama hii kwa sababu, tunataka fedha hizi zijulikane ni za akina nani na zirejeshwe nchini.”
Zitto ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni na Naibu Katibu Mkuu Chadema, alisema kuwa Watanzania walioficha zaidi ya TSh.340 bilioni hawazidi 50 hivyo ni lazima wajulikane na fedha hizo zitaifishwe.
“Wamezificha fedha hizi nje wakati sheria za nchi zinakataza,” alisema na kufafanua kuwa sheria ziko wazi kuwa hakuna Mtanzania anayeruhusiwa kuwa na mali nje ya nchi bila kuwa na kibali cha Benki Kuu ya Tanzania (BoT), hivyo fedha hizo ziko huko kinyume cha sheria.
“Wenzetu wa Senegal wamefanya hivyo, India pia wamefanya hivyo….; Ujerumani na Marekani wao wameamua kuwatoza kodi watu wenye fedha za aina hiyo, lakini sisi tunataka kujua hizi fedha zimetokana na nini kwa sababu zipo ambazo zimetokana na wizi na ufisadi,” alisema.
Alidai kuwa sehemu ya fedha hizo imetokana na wizi katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ya BoT, ufisadi katika Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Meremeta iliyokuwa ikimilikiwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na uchimbaji wa gesi katika baadhi ya mikoa nchini.
Mbunge huyo alienda mbali akisema: “Tunataka kiongozi yeyote wa kisiasa wa Tanzania anayejijua kwamba ana mali nje ya nchi ajitangaze mapema na aseme amezipataje hizo mali, kwa sababu njia pekee ya kupambana na ufisadi ni uwazi.”
Agosti 15 mwaka huu, kambi rasmi ya upinzani bungeni, iliitaka Serikali kuwataja kwa majina viongozi na wafanyabiashara wakubwa walioficha TSh.315.5 bilioni nchini Uswisi (Switzerland)
Akiwasilisha hotuba ya kambi hiyo, Waziri Kivuli wa Fedha, Kabwe Zitto alisema endapo Serikali itashindwa kuwataja watu hao, kambi hiyo itawataja kwa majina katika Bunge linaloanza wiki ijayo.
Zitto alisema mmoja wa viongozi wa juu wa Tanzania (hakumtaja), baadhi ya mawaziri wa Serikali za awamu zilizopita na wafanyabiashara wazito ni miongoni mwa wamiliki wa fedha hizo.
Alisema taarifa ya Benki Kuu ya Uswisi ya Juni mwaka huu, inaonyesha kuwa fedha hizo TSh.315.5 bilioni zimetoroshwa na kufichwa kwenye benki mbalimbali nchini humo.
Alidai kuwa fedha hizo zinatokana na biashara zilizofanywa na watendaji wa Serikali na wafanyabiashara kadhaa kwenye sekta za nishati na madini.
Sehemu kubwa ya fedha zililipwa na kampuni za utafutaji mafuta na gesi katika pwani ya Mkoa wa Mtwara zilizopewa mikataba kati ya mwaka 2004 na 2006.
Baada ya Zitto kumaliza kuwasilisha hotuba yake, Mbunge wa Simanjiro Christopher Ole-Sendeka (CCM) aliomba mwongozo wa Spika kuhusu suala hilo.
Sendeka alisema Zitto alisema miongoni mwa walioficha fedha hizo ni kiongozi wa juu kabisa wa Tanzania, lakini akashangaa Serikali kutohoji juu ya kauli hiyo.
Naibu Spika, Job Ndugai alisema kuwa angetoa mwongozo huo baada ya kuipitia hotuba hiyo ya kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na kuona kama ina matatizo.
Hata hivyo, uchunguzi zaidi wa gazeti hili baadaye ulibaini kuwa fedha hizo zilikuwa na uhusiano na ufisadi kupitia Meremera, unaohusisha Dola za Marekani 132 milioni wastani wa Sh211.2 bilioni.
No comments:
Post a Comment