MFUMKO mkubwa wa dhahabu umegundulika kuwepo kusini mashariki mwa Tanzania, katika kijiji cha Lukwika, Wilaya ya Nanyumbu, Mkoani Mtwara, nchini Tanzania.
Hatua hiyo ilitangazwa
mwishoni mwa wiki mjini hapa na Kaimu Kamishna wa Madini Kanda ya
Kusini, Aloyce Tesha, alipozungumza na waandishi wa habari walioko
kwenye ziara kutembelea miradi ya Wizara ya Nishati na Madini mkoani
hapa.
Alisema
dhahabu hiyo iligundulika wiki mbili zilizopita na tayari ofisi yake
kwa kushirikiana na Wakala wa Ukaguzi wa Madini Nchini (TMAA) imetuma
timu ya wataalamu katika eneo hilo, ili kudhibiti madini hayo ili
serikali iweze kupata kodi na ushuru unaostahili kutoka kwa wachimbaji.
“Tayari wachimbaji pamoja na watoa huduma zaidi ya 7,000 wako katika eneo hilo na kwamba tushatuma wataalamu,” alisema Tesha.
Pamoja na mambo mengine,
alisema mkoa wa Mtwara una aina mbalimbali za madini yakiwemo ya chumvi
ambayo huzalishwa kandokando ya bahari na jasi kwenye viwanda na
mengineyo.
Alisema kwa sasa kuna maandalizi makubwa ya uzalishaji wa saruji mkoani hapa.
Tesha alisema tayari kampuni ya kufanya shughuli hiyo imeshapatikana na hivi sasa iko kwenye hatua za mwisho kuanza kazi hiyo.
Msemaji wa Wizara ya
Nishati na Madini, Fadhil Kilewo, alisema lengo la ziara hiyo ni
kuwawezesha waandishi wa habari kujifunza masuala mbalimbali ya wizara
hiyo na kuihabarisha jamii kwa ufasaha.
|
|
No comments:
Post a Comment