Monday, October 1, 2012

BUHONGWA SEKONDARI YA JIJINI MWANZA, TANZANIA YANG'ARA KITAALUMA !!!

Imeingizwa hapa tarehe 1/10/2012

BUHONGWA ISLAMIC YANG’ARA MOCK KIDATO CHA PILI
Na. Harith Hussein (Gazeti la Kisiwa Na. 41; 28 September 2012)
Shule mpya [ilianza Januari, 2011] ya Sekondari ya Kiislamu ya Buhongwa iliyopo jijini Mwanza mapema mwezi huu imefanikiwa kupata nafasi ya kwanza kufuatia matokeo ya mitihani ya mock ya kidato cha pili iliyofanywa na shule zote za sekondari za Kiislamu hapa nchini.
Kwa mujibu wa matokeo rasmi yaliyotolewa hivi karibuni na Kamati ya Shule za Sekondari za Kiislamu Tanzania, (Inter-Islamic Mock Examination Committee -IIMC) jumla ya wanafunzi 2620 kutoka shule 29 walishiriki kufanya mtihani huo mwaka huu wa 2012. Mitihani hii ya pamoja ya mock inayotungwa na Kamati hiyo ina lengo la kujenga na kuinua viwango vya ufaulu vya shule hizi za Kiislamu. Kamati hii pia inajishughulisha na kusimamia na kuwakilisha mashule haya katika masuala mbalimbali ya kielimu kitaifa.
Akihojiwa na mwandishi wa habari hii, Mkuu wa Shule hiyo Bwana Hussein Kimei amesema mafanikio haya yanatokana na juhudi kubwa inayofanywa na walimu pamoja na wanafunzi wa shule hiyo katika nyanja zote za masomo, dini na nidhamu.  "hii ni juhudi kubwa ya walimu na wanafunzi katika masomo yao’’ alisema Mwalimu Kimei.
Shule ya Sekondari ya Kiislamu ya Buhongwa  yenye namba ya usajili 4561 ipo nje kidogo ya jiji la Mwanza na  ilifunguliwa na kuanza masomo rasmi mnamo Januari 2011. Ni shule ya bweni kwa wavulana na wasichana. Akimalizia mahojiano haya Mkuu wa Shule ameomba wafadhili na jamii nzima ya Kiislamu nchini kuisaidia shule hii hasa katika ujenzi wa msikiti ambao bado haujakamilika ambapo wanafunzi wanaswalia katika uwanja wa mpira shuleni hapo.
Orodha ya shule zilizofanya mitihani hii na nafasi zao inaonekana katika jedwali (limeambatanishwa).

No comments:

Post a Comment