Friday, October 22, 2010

UTAJIRI WA LUGHA YA KISWAHILI

From: Chris Mwasambili
To: list@tanzanet.org
Sent: Thu, Oct 21, 2010 3:19 pm
Subject: [tanzanet] UTAJIRI WA KISWAHILI:Maneno ni mengi, kuyatumia tunashindwa

Imeandikwa na Barnabas Maro; Tarehe: 21st October 2010 Habari Leo

LUGHA ya Kiswahili ina maneno mengi lakini wengi wetu hatuyajui, kwa hiyo tunashindwa kuyatumia.

Matokeo yake tunachanganya maneno ya Kiingereza katikati ya Kiswahili na kufanya kile nikiitacho ’Kiswangereza.’ Sababu hiyo imewafanya baadhi ya watu kusema, kwa mfano, ”wanasiasa ’wanaboa’ kwa maneno yao” badala ya chusha, chukiza, sunza, udhi.

”Wasiasa wanachusha/wanachosha/ wanasunza/wanaudhi.” Hata kuomba radhi siku hizi watu husema ’sore’ (sorry) badala ya ’samahani’ ’kumradhi’ au ’niwie radhi.’ Wengine husema ”tukutane ’hom’ (home)” badala ya nyumbani.

Majuzi nikiwa ndani ya daladala, kijana fulani akiongea na mwenziye kwa simu alimwambia: ”Jana ’nimemwambia’ mkuu kuwa leo napitia benki kuangalia kama fedha zangu za kwenda chuoni zimeingia.”

Kila alipokuwa akielezea mambo yaliyopita alitumia neno ’nime ... ” badala ya ’nili ... .’ Hata nilipomwambia aseme ’nilimwambia’ badala ya ’nimemwambia’ kwa kuwa ni wakati uliopita (jana, juzi, n.k.) hakunielewa ila aliniangalia tu kwa dharau kama sanamu.

Alirudia kosa hilo kila alipozungumza. Kama mwanafunzi wa Chuo Kikuu anakosea na anaposahihishwa haoni wala kujutia kosa lake, itakuwaje kwa mwanafunzi wa msingi?

Kumbe ndio maana wanafunzi hushindwa mitihani ya Kiswahili ingawa ni lugha ya taifa! Kosa kama hili hufanywa na wazungumzaji wengine na waandishi kama ilivyo katika habari ifuatayo: ”Wakati Poulsen akisema hayo, wapinzani wake timu ya taifa ya Morocco ”Atlas Lions” wamewasili juzi usiku ... .”

Ingekuwa: ”Wakati Poulsen akisema hayo, timu ya taifa ya Morocco, Atlas Lions, iliwasili juzi usiku ... .”

Angalizo: Timu iliwasili juzi, jana (wakati uliopita). Kama ujio wake ni siku hiyohiyo, basi husemwa imewasili leo. Naomba wazungumzaji na waandishi wazingatie mambo ya wakati uliopita, uliopo na ujao.

Wengi husema, kwa mfano, ”mimi ’naamkaga’, ’nalalaga’, ’nakulaga’, ’nakwendaga’, ’namwambiaga’, ’nasemaga’.” Kwa ufasaha wa lugha husemwa huamka badala ya ’naamkaga’, hulala badala ya ’nalalaga’, hula badala ya ’nakulaga’, huenda badala ya ’nakwendaga’, humwambia badala ya ’namwambiaga’, na husema badala ya ’nasemaga’.

Baadhi yetu hutumia maneno bila kujua maana yake kama ilivyo katika sentensi ifuatayo: ”Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Deodatus Kinawiro amenusurika kupigwa mawe na wananchi wenye hasira katika kijiji cha Mtanila, baada ya gari lake alilokuwamo lenye namba za usajili STK 3770 kukoswakoswa kuvunjwa vioo kwa madai ya kujihusisha na kampeni za uchaguzi mkuu dhidi ya Chama Cha Mapinduzi.”

Moja kwa moja sentensi hii inaonesha kuwa mkuu wa wilaya ya Chunya, Deodatus Kinawiro alinusurika kupigwa na wananchi kwa kujihusisha na kampeni zinazokwenda kinyume na Chama Cha Mapinduzi.

Hata hivyo, sentensi inayofuatia inaeleza tofauti ingawa mwandishi ni yuleyule! ”Habari ambazo ... (jina la gazeti) imezipata jana zinadai kuwa DC huyo amekuwa akifanya kampeni katika kata na vijiji kadhaa kwa kofia ya serikali ili kuhakikisha kuwa mgombea wa CCM katika jimbo la Lupa, Victor Mwambalaswa, anapita kwa kishindo.”

Kosa kubwa la mwandishi huyu ni kutumia neno ’dhidi’ ambalo bila shaka haelewi maana yake. Kwa kumsaidia, maana ya ’dhidi’ (kivumishi) ni –enye kinyume na; -enye kupingana na; kushindana na; mbalimbali na.

Mwandishi ameandika: ”Habari ambazo (jina la gazeti) imezipata jana ...” si sahihi kwani ingekuwa ” ... ilizipata jana ... ” au ” habari ilizopata gazeti hili jana ... .”

Maneno mengine yanayotumiwa kuunda sentensi huleta maana potofu au sentensi kutokamilika ingawa huwa na nukta mwisho kuashiria sentensi imekamilika.

Tusome sentensi ifuatayo: ”Inashangaza katika uwanja huu ambao mimi ndio msimamizi mkuu na mwenye jukumu la kuhakikisha kwamba mambo yanakwenda vyema kama ilivyopangwa.”

Mwandishi ametumia maneno mengi na hivyo kupoteza nafasi na kuharibu sentensi. Ifuatayo ni sentensi iliyofanyiwa marekebisho:
”Katika uwanja huu mimi ndio mwenye jukumu la kuhakikisha mambo yanakwenda kama ilivyopangwa.”

Ni sentensi yenye maneno 13 dhidi ya 20 aliyotumia mwandishi. Hebu sasa tuingie kwenye methali. “Kanga hazai utumwani” maana yake kanga hatagi ugenini. Methali hii huweza kutumiwa kwa mtu anayeshindwa kufanya jambo lolote anapokuwa katika mazingira mageni.

Tunafunzwa kuwa ugeni una shida. Kangaja simle, mchuzi kitoweo. Kangaja ni aina ya samaki ambaye huwa na harufu mbaya lakini mchuzi wake huwa kitoweo kizuri.

Methali hii hutumiwa katika mazingira ambapo mtu fulani hampendi mwengine ingawa anafaidika na matendo yake. Huweza kumshauri mtu anayekataa kitu kizuri kinachotokana na mtu m-baya au mwenye sifa mbaya.

Msi chembe wala uta si muwani. Muwani ni anayepigana au anayepambana. Chembe ni kigumba cha mshale. Maana yake mtu asiye na chembe au uta si mpiganaji. Methali hii hutumiwa kutukumbusha kwamba lazima tujiandae vizuri tunapotaka kufanya jambo fulani.

Kwa kawaida kila jambo huwa na masharti yake ya kimsingi ambayo hatuna budi kuyatosheleza. Mathalan mwanasiasa mzuri lazima awe stadi (mtu aliye na uhodari au ufundi mkubwa wa kutenda jambo fulani; bingwa, farisi, galacha) wa kusema.

Kitendawili: Ngozi ndani nyama n-nje – Firigisi ya kuku. marobarnabas@yahoo.com

No comments:

Post a Comment